Serikali yaondoa kifungu kuwabana wafanyabiashara kubandika bei za bidhaa

Dodoma. Serikali imekubali hoja za wabunge na kukiondoa kifungu kinachotaka wafanyabiashara kuweka bei ya bidhaa zao ili mteja ajue badala ya kutamkiwa bei.

Uamuzi huo umefikiwa baada ya wabunge wengi kuona kifungu hicho kitawaumiza wafanyabiashara wadogo, hasa wamachinga na mama na baba lishe na kushauri kiangaliwe upya.

Awali, Serikali ilipendekeza marekebisho ya sheria ya ushindani ambayo ingelazimisha wafanyabiashara wote, wakiwamo machinga, mama na baba lishe pamoja na wauza mchicha kubandika bei kwenye bidhaa zao.

Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Ushindani wa Mwaka 2024 umewasilishwa bungeni leo Jumanne Septemba 3, 2024 na Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Selemani Jafo.

Dk Jafo amesema miongoni mwa marekebisho ni wauzaji wa bidhaa na huduma watalazimika kuanza kuonyesha bei ya bidhaa na huduma.

“Ibara ya 13 inafuta kifungu cha 17 cha sheria na kukiandika upya kwa lengo la kuweka masharti ya wauzaji wa bidhaa na huduma kuonyesha bei za bidhaa na huduma, badala ya bei husika kutamkwa na muuzaji.

“Vilevile imeelezwa kuwa, kosa la kukiuka masharti hayo kwa watu wa kawaida ni kutozwa faini isiyopungua Sh300,000 na isiyozidi Sh1 milioni,” amesema Dk Jafo.

Licha ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo kuunga mkono marekebisho hayo, imetoa maoni kuhusu adhabu ikishauri iwe Sh10,000 kiwango cha chini na cha juu kiendelee kuwa Sh1 milioni.

Akiwasilisha maoni ya kamati hiyo, Mwenyekiti wake, Deo Mwanyika amesema: “Kuhusu Ibara ya 13 inayofuta kifungu cha 17 cha sheria na kukiandika upya kwa lengo la kuweka masharti ya wauzaji wa bidhaa na huduma kuonyesha bei za bidhaa na huduma, badala ya bei husika kutamkwa na muuzaji, kamati ina maoni tofauti kuhusu adhabu.

“Vilevile imeelezwa kuwa, kosa la kukiuka masharti hayo kwa watu wa kawaida ni kutozwa faini isiyopungua Sh300,000 na isiyozidi Sh1 milioni.

“Kamati katika uchambuzi wake ilipata wasiwasi kuhusu utekelezaji wa kifungu hiki, hasa kwa wajasiriamali wadogo ikiwemo wauzaji wa chakula katika maeneo yasiyo rasmi maarufu mama lishe, watembeza bidhaa maarufu machinga, bodaboda na wauzaji wa bidhaa ndogondogo magengeni.”

Amesema, “wasiwasi zaidi ulionekana kwenye faini inayopendekezwa kwa kuona inaweza kuwaondoa sokoni wafanyabiashara wadogo, badala ya kuwalinda na kuwakuza.

“Kamati ilishauri kwamba kwa wauzaji wa bidhaa au huduma wenye mtaji usiozidi shilingi milioni nne, adhabu yao kwa kosa la kutokuonyesha bei ya bidhaa au huduma iwe ni faini isiyozidi Sh50,000.

“Serikali ilikubali ushauri huo kwa kuahidi kufanya marekebisho kupitia jedwali na kuweka kiwango cha adhabu kuwa faini isiyopungua Sh10,000 na isiyozidi Sh1 milioni,” amesema.

Amesema kamati imeishauri Serikali kuwa tume yenyewe ndiyo ihusike katika usimamizi wa kifungu hicho kutokana na kuwa na utalaamu wa kipekee katika masuala ya ushindani.

“Vilevile imeshauri katika kutekeleza kifungu hiki, wizara itunge kanuni au mwongozo kuhusu utekelezaji wake, ili kuepusha matumizi mabaya ya mamlaka yanayoweza kutendeka na baadhi ya watumishi wasio waaminifu kwa kuwatoza wafanyabiashara wadogo faini kubwa kinyume cha ushauri wa kamati,” amesema.

Mwanyika amesema kuhusu sharti la kuonyesha bei ya bidhaa na huduma, kamati ilielezwa kuwa madhara ya kutokuonyesha bei ya bidhaa ni makubwa kwa walaji, ukiwianisha na manufaa ya kuonyesha bei yake.

“Kwa msingi huo, ni vyema kuanza kuliko kuacha hali kama ilivyo sasa. Ni rai ya kamati kuwa elimu ya kutosha itatolewa kabla ya kuanza kutekelezwa kwa kifungu hiki,” amesema.

Katika mapendekezo mengine, Dk Jafo alisema kifungu cha 10A kinapendekezwa kuongezwa kuweka masharti yanayozuia makubaliano baina ya watu walio katika ngazi tofauti katika mnyororo wa uuzaji wa bidhaa.

Amesema madhumuni ya marekebisho yanayopendekezwa ni kuhakikisha kuwa washindani wanashindana kwa haki na watumiaji wananunua bidhaa au huduma kwa bei shindani.

“Kifungu cha 11A kinapendekezwa kuongezwa, ili kuiruhusu Tume ya Ushindani kuidhinisha muungano wa kampuni wenye manufaa makubwa kwa umma.

“Vilevile, sehemu inayopendekezwa inatoa vigezo vinavyounda manufaa hayo ya umma. Madhumuni ya marekebisho yanayopendekezwa ni kuhakikisha kuwa nchi inanufaika kutokana na muungano wa kampuni kwa masilahi mapana kwa umma,” amesema.

Mbunge wa Viti Maalumu, Salome Makamba akichangua muswada huo amesema: “Tujiulize leo machinga aweke bei, yaani anauza mikanda, vitochi, sijui betri ataziweka wapi hizo bei uweze kuziona, atazibandika kwenye mwili wake, pale anapotembeza bidhaa zake?” amehoji Makamba.

Mbunge wa Babati Mjini, Pauline Gekul aliingilia kati akisema: “Serikali imezingatia adhabu ilikuwa Sh300,000 kwenye muswada wa awali, lakini sisi kamati tulivyochakata ilishusha ikazingatia hao machinga unaowataja ikashusha adhabu mpaka Sh10,000 kwa hiyo kima cha chini kimezingatiwa,” amesema akifafanua mchango wa Makamba.

Naibu Spika, Mussa Zungu alitoa maelezo kwa mchango wa Gekul akisema: “Hoja sio hiyo, machinga anatembea na varieties 20 (aina ya bidhaa 20) mkononi, bei anaziwekaje? mtu ana machungwa tenga, kuna vitu wana- negotiate (wanajadiliana), unakwenda kwa machinga una-point nataka hiyo una-negotiate pale, that is the issue na watu wa chini.

“Nilikuwa sipendi kuingilia haya mambo, nendeni pale machinga Kariakoo au nendeni machinga pale Ilala kwa wauza vitu. Mimi nafikiri kuna level ya scope (upeo) ya biashara. Lifikirieni upya hili suala,” amesema.

Makamba aliendelea kuchangia akisema kamati ilipendekeza adhabu ianze Sh10,000 na isizidi Sh50,000 lakini Serikali inasema Sh10,000 mpaka Sh1 milioni, ambayo alisema bado ni kubwa.

Mbunge wa Viti Maalumu, Dk Christine Ishengoma amesema sheria hiyo ni nzuri na kwamba faini walikubaliana na Serikali kima cha chini kiwe Sh10,000 na cha juu kisizidi Sh1 milioni.

Dk Ishengoma amesema pia walikubaliana na Serikali kiwepo kifungu kitakachowabaini wafanyabiashara wako kwenye uwezo upi, ili kanuni iwekwe kuwatambua wajasiriamali kutokana na kiwango chao cha biashara.

“Serikali wameipenda kwa sababu itapunguza majadiliano kwenye bei. Kwa sababu bei utaiona hapo huwezi kuomba upunguziwe. Tusonge mbele, tulisema ni vigumu, lakini tuanze tuone tutafika wapi,” amesema.

Mbunge wa Viti Maalumu, Yustina Rahhi ameunga mkono wafanyabiashara kuweka bei za bidhaa, akisema Watanzania wengi wameibiwa na wafanyabiashara.

Amesema wafanyabiashara wengi siku hizi wanauza kwa kuangalia hali ya mtu.

“Sisi ni mashahidi, ukifika dukani kama suti inauzwa Sh100,000, akiingia mteja mkurugenzi au mbunge kwa kweli suti ya Sh100,000 itauzwa Sh400,000 hadi Sh500,000,” amesema.

Katika hatua nyingine, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza Johari amewasilisha bungeni muswada wa sheria wa marekebisho ya sheria mbalimbali namba mbili wa mwaka 2024 wenye sheria kuu nane.

Miongoni mwa sheria hizo ni marekebisho ya Sheria ya Uhamiaji, Sura ya 54.

Mbali ya hiyo, Serikali imeondoa marekebisho kuhusu hadhi ya kumiliki ardhi kwa Watanzania wenye uraia wa nchi nyingine.

Mbunge Gekul akichangia muswada kuhusu Sheria ya Uhamiaji, Sura ya 54 amesema: “Mimi ni mjumbe wa kamati niunge mkono maoni ya kamati kuhusu hoja ya hadhi maalumu ambapo kamati imeshauri hata hao watu tunaotaka kuwapa hadhi maalumu ya kumiliki ardhi, kwanza wako wangapi.

“Na hizi sera ya ardhi za biashara zikiangaliwa na tukajua kama nchi tunataka kuwapa hadhi maalumu Watanzania wenzetu ambao wako nje ya nchi ni wangapi?” “Na hizi sera ya ardhi za biashara zikiangaliwa na tukajua kama nchi tunataka kuwapa hadhi maalumu Watanzania wenzetu ambao wako nje ya nchi ni wangapi?

“Lakini, wana kitu gani ambacho wangetamani kufanya ambacho wataka kumilikishwa, sio tu idadi… lakini pia ni thamani gani wanataka kuongeza ambayo imeshindikana kwenye dirisha la uwekezaji.

“Ukifahamu idadi, sio wote wanaostahili kupewa hiyo hadhi maalumu, ni kitu gani muhimu wanataka kuongeza.”

Related Posts