Dodoma. Jumla ya Sh1.29 bilioni zitatumika kuwalipa fidia wakazi 724 wakiwamo wa Muhambwe mkoani Kigoma wanaotakiwa kupisha ujenzi wa barabara kutoka Kibondo hadi Mabamba.
Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amesema hayo leo Septemba 3, 2024 wakati akijibu swali la msingi la mbunge wa Muhambwe (CCM), Dk Florence Samizi.
Mbunge huyo amehoji ni lini Serikali itawalipa fidia wananchi wa Muhambwe waliopisha ujenzi wa Barabara ya Kibondo hadi Mabamba.
Akijibu swali hilo, Bashungwa amesema Serikali imekamilisha tathimini ya mali za wananchi zitakazoathiriwa na mradi wa ujenzi wa Barabara ya Kibondo – Mabamba yenye urefu wa kilometa 47.925.
“Katika tathmini hiyo jumla ya wananchi 724 wakiwamo wa Muhambwe wanastahili kulipwa fidia yenye jumla ya Sh1.29 bilioni,” amesema.
Bashungwa amesema sasa Serikali inakamilisha taratibu za malipo ya fidia kwa wananchi hao.
Amesema baada ya shughuli hiyo kukamilika wananchi hao watalipwa fidia.
Katika swali la nyongeza, Dk Florence amesema ujenzi wa barabara hiyo umeshaanza na kuhoji ni lini Serikali itaharakisha ulipaji wa fidia hiyo ili wananchi hao wapate stahiki yao.
“Ujenzi wa barabara ya Kilometa 25 wa Kibondo mjini unasuasua mno kwa madai kuwa, mkandarasi hajalipwa fedha na ameshatoa mitambo site amepumzika anasubiri malipo,”amesema Dk Florence.
Amehoji ni lini Serikali itamlipa malipo yake aweze kurejea site.
Akijibu swali hilo, Bashungwa amesema wamewasilisha malipo hayo Hazina na kwamba wizara yake itaendelea kufuatilia ili kuhakikisha wananchi hao wanalipwa.
Kuhusu kuchelewa kwa ujenzi wa barabara, Bashungwa alimuagiza mkandarasi kutosimamisha ujenzi huo na kwamba wameshawasilisha mahitaji ya mkandarasi huyo hazina.
“Namuagiza mkandarasi aendelee na kazi wakati akisubiri malipo,” amesema.