Dar es Salaam. Hali ya afya ya shahidi wa pili wa upande wa madai katika kesi ya mgogoro wa malipo ya mkopo iliyofunguliwa na Kampuni ya Continental Reliable and Clearing (CRC) (mkopaji) dhidi ya benki za Equity Tanzania (EBT) na Equity Kenya (EBK), imekwamisha usikilizwaji wa kesi hiyo.
Kesi hiyo ilipangwa kuendelea kwa siku nne mfululizo kuanzia Jumatatu Septemba 2, 2024, lakini jana ilikwama kuendelea kwa kuwa jaji anayeisikiliza Profesa Agatho Ubena alikuwa na dharura.
Hivyo ilitarajiwa kuendelea leo, Septemba 3, 2024 na shahidi huyo wa pili upande wa mdai, Alexander Gombanila alitarajiwa kufika mahakamani kwa ajili ya kuhojiwa maswali ya dodoso na mawakili wa utetezi, kuhusiana na ushahidi wake wa msingi aliokwishautoa mahakamani hapo.
Hata hivyo, kesi hiyo ilipoitwa Wakili wa mdai, Frank Mwalongo ameieleza Mahakama shahidi wake aliyekuwa akitarajiwa kufika kuendelea na ushahidi wake katika hatua hiyo ya madodoso ni magonjwa.
Wakili Mwalongo amesema jana Jumatatu alikuwa anaendelea vizuri lakini ilipofika usiku hali yake ilibadilika, hivyo ameenda hospitali kwa ajili ya matibabu zaidi.
“Jana, alikwenda hospitalini na hali yake ilikuwa inaendelea vizuri hadi naongea naye, lakini ilipofika usiku hali yake imebadilika na amesindikizwa na mkewe hospitalini. Na hivi ninavyoongea bado yupo hospitalini,” amesema Mwalongo.
Kutokana na hali hiyo ya ugonjwa wa shahidi huyo, ameiomba Mahakama ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kuendelea na usikilizwaji wa kesi hiyo katika hatua hiyo.
Baada ya maelezo hayo, Jaji Ubena ameutaka upande wa wadai wawasiliane na mgonjwa ili kuangalia hali yake inavyoendelea kama ataendelea vizuri kesi hiyo itaendelea Alhamisi, Septemba 5, 2024 na kama atakuwa bado hajapona, itaendelea Novemba 11 mpaka 14, 2024.
Katika kesi hiyo ya kibiashara namba 16 ya mwaka 2023, CRC inapinga kudaiwa kurejesha mkopo huo wa zaidi ya Dola10.13 milioni za Marekani ilizokopeshwa na benki hizo, ikidai kuwa ilisharejesha mkopo wote na hivyo haina deni kwa benki hizo.
Kampuni hiyo (CRC) ilifungua kesi hiyo baada ya EBK kupitia wakala wake, EBT kuiandikia barua ikiipa siku 21 kurejesha mkopo wake uliotolewa kwake kwa nyakati tofauti kuanzia mwaka 2013 wa Dola 10.13 milioni za Marekani (Sh26 bilioni).
Kesi hiyo ni miongoni mwa kesi kadhaa zilizofunguliwa na kampuni mbalimbali zikipinga kudaiwa na benki hizo na zile zilizofunguliwa na benki hizo dhidi ya kampuni kadhaa zikizidai kampuni mbalimbali pesa ambazo zinadai zilizikopesha mabilioni ya fedha, lakini zimeshindwa au zimepuuza kurejesha mikopo hiyo.
Mara ya mwisho Mahakama hiyo iliikatalia kampuni hiyo kupokea nyaraka muhimu katika utetezi wake kutoka na kutotimiza matakwa ya kisheria.
Kampuni hiyo kupitia shahidi wake huyo wa pili, Gombanila akiongozwa na wakili wa kampuni hiyo, Mwalongo, iliiomba Mahakama hiyo ipokee nyaraka hiyo iliyodaiwa kuwa ni jedwali la malipo ya mkopo wote ambao kampuni hiyo ilipewa na benki hizo.
Hata hivyo, mawakili wa benki hizo, Emmanuel Saghan anayeiwakilisha EBT ( mdaiwa wa kwanza) na Mpaya Kamala, anayeiwakilisha EBK (mdaiwa wa pili) walipinga nyaraka hiyo kupokewa wakidai haijakidhi matakwa ya kisheria.
Mahakama katika uamuzi wake ilikubaliana na hoja za pingamizi la mawakili wa utetezi ikaitupilia mbali nyaraka hiyo.
Baada ya hatua hiyo mawakili hao wa utetezi walianza kumhoji shahidi huyo maswali ya dodoso kuhusiana na ushahidi wake aliokwishauwasiliaha mahakamani hapo kwa njia ya maandishi pamoja na nyaraka mbalimbali wanazokusudia kutumika kama vielelezo vya ushahidi.
Pamoja na mambo mengine katika mahojiano hayo, alidai kuwa yeye hakuwepo wakati mkopo huo inatolewa kwa kuwa alikuwa bado hajaajiriwa katika kampuni hiyo, bali ni kupitia taarifa alizozisikia kwa wafanyakazi wenzake na alizozikuta ofisini.
Katika kesi hiyo kampuni hiyo inaomba nafuu mbalimbali ikiwamo Mahakama itoe amri dhidi ya wadaiwa kuwa wamevunja mikataba ya mikopo na kuvunja wajibu wa kibenki dhidi ya mdai kama mteja.
Pili, Mahakama itamke kuwa mdai amelipa mikopo yake yote na hadaiwi.
Tatu, Mahakama itamke ya kuwa Dola 10.13 milioni za Marekani ambazo wadaiwa kwa pamoja wamemtaka mdai alipe kama kiasi cha mkopo ambacho hakijalipwa sio halali na hakijawahi kuwepo.
Nne, Mahakama itamke kuwa mikopo inayodaiwa kutolewa Mei 29, 2018, Novemba 3, 2021 na Februari 19, 2022 ni batili.
Tano, Mahakama itamke kuwa mikopo iliyotolewa Februari mosi, 2019 na Septemba 17, 2020 haijawahi kutekelezwa na mdaiwa namba mbili (EBK) isipokuwa kwa kiasi fulani ilitekelezwa na mdaiwa namba moja, EBT.
Sita, Mahakama itamke kuwa mikataba ya dhamana zote (mali) zisizohamishika zilizowekwa kwa wadaiwa kudhamini mikopo na mdai ni batili.
Saba, Mahakama itoe amri ya kuziondoa dhamana hizo kwenye mikopo na kuzikabidhi kwa mdai.
Nane, Mahakama itoe tamko la kutaka wadaiwa walipwe fedha za mkopo na mdai ni batili.
Tisa, Mahakama itamke kuwa mdaiwa wa pili, EBK hana leseni ya kuendesha shughuli au biashara ya kibenki au biashara yoyote Tanzania, hivyo amefanya biashara kinyume cha sheria tofauti na matakwa ya kanuni na miongozo inayohusiana na biashara za kibenki nchini Tanzania.
Kumi, Mahakama itamke kwamba EBK hajawahi kutoa au kumpatia mkopo mdai.
Kumi na moja, Mahakama iamuru mdai alipwe fidia, gharama za kesi na nafuu nyinginezo ambazo Mahakama itaona zinastahili kwa mdai.
Kwa mujibu wa hati ya madai iliyowasilishwa mahakamani hapo, kati ya mwaka 2013 mpaka 2017 mdai (CRC) alikuwa ni mteja wa EBT.
Kwa kipindi chote hicho, mdaiwa alipatiwa mikopo mbalimbali iliyofikia minane kwa ajili ya kuendesha biashara zake miongoni mwake ni biashara ya usafirishaji wa mizigo na mafuta kwa kutumia magari.
Uhusiano baina ya mdai na mdaiwa wa pili EBK ulianza Mei 2018, alipoanza kumpa mikopo mdai kwa kushirikiana na EBT.
Mikopo inayohusika katika mgogoro huo ni ile inayodaiwa kutolewa na wadaiwa wote wawili kwa mdai iliyosainiwa na pande zote mbili, mdai na wadaiwa wote wawili Mei 29, 2018, Novemba 3, 2021 na Januari 19, 2022, inayofikia Dola 10.13 milioni za Marekani ambazo wanadaiwa wanadai kuwa mdai hajalipa.
Hivyo, wadaiwa nao wanamtaka mdai alipe pesa hizo kama alivyokopa kulingana na mikataba ya mikopo.
Hata hivyo, mdai anapinga madai ya kulipa pesa hizo kwa akidai kuwa ingawa wakopeshaji wametajwa wote wawili kwenye mikopo hiyo, lakini mdaiwa hajawahi kuingiziwa fedha zozote EBK, wala kulipa pesa zozote kwa EBK.
Kuhusu fedha alizokopeshwa na EBT mdai anadai kuwa aliendelea kuzilipa na ulipaji huo ulithibitishwa kila mara na mdaiwa wa kwanza.
Wadaiwa katika majibu yao ya utetezi yaliyowasilishwa mahakamani kwa pamoja, wanapinga madai na hoja yaliwasilishwa mahakamani na mdai, hivyo wanaiomba Mahakama iyatupilie mbali kwa kuwa mdai alikopa kihalali kutoka kwa wadaiwa wote wawili.
Wanadai kuwa kwa nyakati tofauti kati ya Mei 27, 2020, Januari 19, 2023, Januari 26 2023 na Februari 26, 2023 mdaiwa kupitia mawasiliano kwa njia ya barua pepe na barua nyingine zilizoandikwa kwenda kwa wadaiwa alithibitisha kutolewa kwa fedha hizo za mikopo.
Hivyo, wanadai kuwa hawezi kuitaka Mahakama kubatilisha mikataba ya mikopo hiyo baada ya kushindwa kuilipa au kurejesha.