Singida yampa Mwenda saa 24 kuripoti kambini

UONGOZI wa Klabu ya Singida Black Stars umetoa saa 24 kwa beki Israel Mwenda kujiunga haraka kambini kwa mujibu wa mkataba wake na endapo atashindwa kufanya hivyo anatakiwa kulipa Sh500 milioni.

Mwenda amejiunga na Singida Black Stars kwa mkataba wa miaka miwili mwanzoni mwa msimu huu, lakini hajawahi kuripoti kambini kwa kile kinachodaiwa kuwa hajalipwa stahiki zake zote za mkataba.

Ofisa Habari wa Singida Black Stars, Hussein Masanza ameiambia Mwanaspoti kuwa kutokana na mchezaji huyo kuchelewa kujiunga na kambi wametoa misimamo miwili.

“Uongozi wa klabu leo umeshamtumia barua mchezaji Israel Mwenda na menejimenti yake yote (nakala kwa TFF pia) kwa mambo mawili,” amesema.

“Kwanza tumemtaka mchezaji aripoti kambini haraka ndani ya saa 24 baada ya kupokea barua ya wito tuliyomtumia.”

Amesema endapo atashindwa kufanya hivyo anatakiwa ailipe klabu hiyo Sh500 milioni ambazo ni gharama ya kuvunja mkataba.

Juhudi za kumpata Mwenda kuzungumzia wito huo hazijazaa matunda, lakini Mwanaspoti inaendelea kumtafuta.

ENDELEA KUFUATILIA MITANDAO YA MWANASPOTI

Related Posts