Dar es Salaam. Wakati Serikali ikihimiza bima ya afya kwa wote, taasisi zinazosaidia utoaji wa huduma hiyo kwa unafuu, zimetakiwa kufikisha elimu hiyo ngazi ya chini ya jamii ili waweze kuzifahamu.
Wito huo umetolewa na Mratibu wa Tiba na Magonjwa yasiyoambukiza Manispaa ya Kinondoni, Dk Omar Mwangaza kwenye uzinduzi wa uchangiaji wa kadi ya afya inayotolewa na Shirika la Kimataifa lisilo la Kiserikali la Arthshakti Foundation Tanzania, Septemba mosi 2024 .
Dk Mwangaza amesema hilo linapaswa kufanywa kwa kuwa ugonjwa hauna hodi na hauchagui mtu awe tajiri au masikini, hivyo kila mmoja anapaswa kujiandalia mazingira ikiwamo kuwa na bima za afya.
“Bado elimu haijafika kwa jamii vile vya kutosha, kwa kuwa magonjwa huja ghafla inaweza kumgaharimu sio yeye tu bali hata familia.
“Tayari Serikali imejitahidi kujenga miundombinu ya utoaji huduma hizo, hivyo ni wajibu wa kila mwanajamii kuona namna gani anakuwa na bima ili kupata huduma hizo kirahisi,”amesema Dk Mwangaza.
Amesema kwa Kinondoni hadi sasa wenye bima ya afya ya jamii ni 18,465 kati ya watu 982,328 wanaoishi katika wilaya hiyo, jambo linaloonyesha bado mwitikio sio mzuri.
Akizungumzia Kadi ya Afya inayotolewa na Arthshakti Foundation, Dk Mwangaza amesema imekuja wakati mzuri ambao Serikali inasisitiza bima ya afya kwa wote, hivyo kwa kufanya hivyo ni kuiunga mkono katika kutekeleza suala hilo.
Mwanzilishi wa Arthshakti Foundation, Somesh Kulshrestha, amesema shirika lao lilianzishwa nchini mwaka 2022 na wamekuwa wakijishughulisha na mambo mbalimbali ikiwamo uwezeshaji wanawake kiuchumi, kuweka kambi za utoaji huduma za afya, utoaji elimu kuhusu magonjwa yasiyoambukiza hasa afya ya akili.
Akizungumzia kuhusu kadi hizo, amesema zimelenga zaidi kuwafikia watu wa hali ya chini na muhusika atatabiwa hospitali binafsi kwa kupata punguzo la bei.
Dk Mwangaza amesema ili kuzipata mtu atapaswa kuwa mwanachama kwa kulipia kati ya Sh5,000 hadi Sh50,000 kwa mwaka huku akitaja hospitali ambazo mwanachama atapata huduma kuwa ni pamoja na Agha Khan Health Center, Tanzania, Hitech Sai Hospital, Rally Polyclinic, SD Dental na Hospidio.
Naye Rais wa Arthshakti Foundation Tanzania, Kelvin Mshana akifafanua zaidi kuhusu gharama, amesema kwa wanachama wa kadi ya afya ya kiuchumi wao watapata punguzo la asilimia 20 kwa bili za hospitali, asilimia 50 ya mchango kwenye bili ya X ray na asilimia 20 ya punguzo kwenye maduka ya dawa.
“Nyingine ni kupelekewa dawa hadi nyumbani, huduma ya gari la wagonjwa kwa dharura, na michango ya hadi Sh200,000 katika kesi za ajali za barabarani.
“Huku wale kadi za afya za malipo watapata punguzo la asilimia 20-30 kwa bili za hospitali, mchango wa asilimia 100 kwenye bili ya X ray pamoja na punguzo la asilimia 30 la maduka ya dawa,” amesema Mshana.