Tanimu: Kutua Ulaya ni kama zali tu

ALIYEKUWA beki wa Singida Black Stars, Benjamin Tanimu ambaye amejiunga na Crawley Town FC ya Ligi Daraja la Pili England ‘EFL League One’, amesema ni kama zali tu kwake kutoka Ligi Kuu Bara hadi kupata nafasi ya kwenda kucheza soka la kulipwa katika moja ya mataifa makubwa barani Ulaya.

Kitasa huyo ambaye alikuwa akiitwa na kucheza timu ya taifa ya Nigeria, alisema wakati akitua Bongo alijiwekea malengo ya kuifanya Ligi Kuu ya Tanzania kuwa daraja la kupiga hatua zaidi jambo ambalo kwa sasa limetimia.

“Kiukweli nawashukuru sana Singida Black Stars kwa kuwa sehemu ya kupiga kwangu hatua, nilikuwa na wakati mzuri nikiwa Tanzania, nilifurahia fursa niliyopata ya kucheza Ligi Kuu Bara, ni moja ya ligi nzuri na yenye ushindani, hakika sikufanya makosa juu ya uchaguzi ambao niliufanya,” alisema na kuongeza;

“Sasa ni wakati wa kutazama maisha mapya pamoja na kwamba sitakuwa Tanzania lakini nitaendelea kuwa balozi mzuri kwa Singida na nawatakia kila la kheri katika msimu huu naamini utakuwa bora zaidi.”

Siku chache zilizopita, Singida Black Stars kupitia mitandao yao ya kijamii ilitangaza kumuuza mchezaji huyo kwa ada ya zaidi ya Sh2.3 bilioni.

Kwa upande wake, Kocha wa Singida Black Stars, Patrick Aussems amemtakia kila la kheri nyota huyo akisema: “Ni mchezaji mzuri ambaye bado ana umri wa kukua zaidi na kuwa bora, sidhani kama kutakuwa na pengo lake kwa sababu Singida ina wachezaji wengi wazuri ambao tayari wameanza kuonyesha ubora wao.”

Tanimu mwenye miaka 22, ameingia kwenye vitabu vya historia kwa kuwa mchezaji wa kwanza kwa timu hiyo kuuzwa barani Ulaya.

Related Posts