TCU yafungua udahili awamu ya pili

Dodoma. Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) imefungua dirisha la udahili kwa awamu ya pili kwa wanafunzi wa shahada ya kwanza mwaka wa masomo 2024/2025 utakaoanza leo Jumanne, Septemba 3  hadi 21, 2024.

Dirisha hilo linafunguliwa wakati ambao waombaji 98,890 sawa na asilimia 79.6 ya waombaji walioomba udahili katika awamu ya kwanza wamepata udahili kwenye vyuo walivyoomba.

Katibu Mtendaji wa TCU, Dk Charles Kihampa amesema hiyo ni fursa kwa waombaji ambao hawakuweza kutuma maombi ya udahili au hawakuweza kupata nafasi ya kudahiliwa katika awamu ya kwanza kutokana na sababu mbalimbali.

“Watumie fursa hii vizuri kwa kutuma maombi yao ya udahili kwenye vyuo wanavyovipenda. Tume inaelekeza vyuo vya elimu ya juu nchini kutangaza programu ambazo bado zina nafasi,” amesema Dk Kihampa, leo Jumanne, Septemba 3, 2024 jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Pia, waombaji wameombwa kuzingatia utaratibu wa udahili wa awamu ya pili kama ilivyooneshwa kwenye kalenda ya udahili iliyoko katika tovuti ya TCU.

“Waombaji udahili wa shahada ya kwanza wanakumbushwa masuala yote yanayohusu udahili au kujithibitisha katika chuo kimoja yawasilishwe moja kwa moja kwenye vyuo husika.

“Kwa wale ambao watapata changamoto katika kujithibitisha, vyuo vyote vimeelekezwa kupokea taarifa zao na kutafuta ufumbuzi wa haraka kwa kuzingatia miongozo na taratibu zilizowekwa,” amesema.

Profesa Kihampa amesema kwa waombaji ambao wamepata chuo zaidi ya kimoja wanapaswa kuthibitisha udahili wao katika chuo kimoja na mwisho ni Septemba 21, 2024.

“Nitoe wito kwa waombaji ambao wamepata vyuo zaidi ya kimoja, kuwa watapokea ujumbe mfupi wa kupitia simu walizotumia wakati anaomba au watatumiwa code (namba maalumu ya siri) na pia itatumwa kwenye email (anuani ya barua pepe) ambayo wanatakiwa kuitumia kujithibitisha. Sasa amepata chuo X na amepata chuo Y achakuge anakwenda chuo gani,” amesema.

Amesema kwa wale ambao hawatakuwa wamepata ujumbe mfupi lakini wamepata udahili kwenye vyuo zaidi ya kimoja wanapaswa kuingia kwenye mfumo wa udahili wa vyuo vilivyomdahili na kuomba kutumia ujumbe mfupi wenye namba maalumu ya siri ili kuweza kujithibitisha katika chuo husika.

Kwa mujibu wa TCU, awamu ya kwanza ya udahili wa wanafunzi imekamilika na majina ya waliodahiliwa katika awamu hiyo yanatangazwa na vyuo husika.

Awamu ya kwanza ya udahili, jumla ya waombaji 124,286 walituma maombi ya kujiunga katika vyuo 86 vilivyoidhinishwa kudahili wanafunzi katika shahada ya kwanza.

Hata hivyo, kati ya waliotuma maombi ni 98,890 sawa na asilimia 79.6 ndiyo wamepata udahili kwenye vyuo walivyoomba ikiwa na maana nafasi takribani 100,000 bado ziko wazi kwani wanafunzi 198,986 ndiyo wanaohitajika.

Idadi ya nafasi zilizopo katika mwaka wa masomo unaotarajiwa kuanza mwaka huu ni ongezeko la asilimia 6.8 ikilinganishwa na nafasi 186,289 mwaka uliopita zilizokuwapo kwa ajili ya shahada ya kwanza.

“Idadi ya waombaji wa udahili watakaodahiliwa inatarajia kuongezeka katika awamu ya pili ya udahili,” amesema Profesa Kihampa.

Mbali na kuongezeka kwa nafasi za masomo, pia programu zinazotolewa na vyuo zimeongezeka hadi kufikia 856 ikilinganishwa na programu 809 mwaka 2023/2024, ikiwa ni ongezeko la programu 47 za masomo.

Mkazi wa Nkhungu, Stella Theonest amesema ongezeko la nafasi za udahili uende sambamba na kuangalia jinsi gani ya kuwasaidia wanafunzi wasiokuwa na uwezo kulipia ada katika vyuo hivyo.

“Kupata nafasi ni sehemu moja, lakini ukishapata nafasi unaanza kufikiria kuhusu ada utapata wapi kama hujapata mkopo. Serikali ifikirie jinsi ya kusaidia hizi familia ambazo hazina uwezo wa kumudu ada za taasisi za elimu ya juu wapate asilimia 100 za mikopo,” amesema.

Related Posts