Biharamulo. Viboko waliopo Mto Mwiruzi wamegeuka tishio kwa wananchi kwa kuharibu mashamba ya mpunga mtama, mahindi na miwa zaidi ya ekari 2,000, huku wakihatarisha maisha ya wananchi.
Wakizungumza na Mwananchi leo Septemba 3, 2024 baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Msekwa wilayani Biharamulo, Kasiri Mabula wamesema adha ya viboko imekuwa ikiwakumba kwa zaidi ya miaka saba sasa.
Mabula amesema kwa sasa amekata tamaa ya kuendelea kulima eneo hilo maana tangu mwaka 2016 amekuwa akijishughulisha na kilimo cha mpunga na mtama ila kila mwaka anaambulia mabaki ya mazao kutokana na kuharibiwa.
Mabula amesema wanyama hao wanahatarisha usalama wao hasa watoto wanapokwenda shule, kwa kuwa sasa wanalazimika kuwasindikiza.
Mwenyekiti wa Kitongoji Kikonya Kijiji Msekwa Kata ya Kalenge, Magina Saguda amesema wananchi wameacha kujishughulisha na kilimo badala yake wanashinda nyumbani jambo ambalo limekuwa hatari kwa uchumi wa kata hiyo.
Amesema licha ya kutoa taarifa kwa viongozi wa kijiji, hakuna hatua zinazochukulia, hivyo kwa sasa wanakabiliwa na hatari ya njaa.
“Viboko wanasafiri zaidi ya kilometa 10 kufuata mazao ya wakulima katika vijiji vyote vya kata hiyo ya Kalenge, wanaharibu uchumi wetu mahindi, mpunga, mtama, hata mboga mboga tukilima wanakula, mwisho tumechoka sasa,” amesema.
Akizungumzia kero hiyo, Diwani wa Kalenge, Erick Method amesema taarifa za viboko hao ameishazifikisha kwenye Baraza la Madiwani Wilaya ya Biharamulo ila juhudi za kuwadhibiti wanyama ni ndogo sana.
Method amesema kila saa moja asubuhi na saa 12 jioni wanyama hao husambaa mitaani na mashambani.
Ofisa Maliasili Wilaya Biharamulo, Thomas Mahenge amekiri ongezeko la wanyama hao aliosema wanatoka Bonde la Mto Mwiruzi lililopo kati ya Biharamulo na Wilaya Kakonko mkoani Kigoma.
Thomas, amesema viboko hao walikuwa ni familia moja ila kwa sasa wameongezeka na kutengeneza familia zaidi ya tano.
Amesema wamewasiliana na Mamlaka ya Usimamizi wa wa Wanyamapori (Tawa) ili kuwadhibiti kwa kuwafukuza au kuwafurusha kwa kuwabeba.
“Wameongezeka ni wengi na maamzi yetu kwa sasa tulipofikia lazima tuwaondoshe kwa kuwafurusha au kuwabeba wazima wazima,” amesema.