Vijiji vilivyoathirika na maporomoko Hanang kunufaika na mradi wa maji 

 Babati. Vijiji vitano vilivyoathirika na maporomoko ya matope  kutoka Mlima Hanang Desemba 2023 mkoani Manyara, vinatarajiwa kunufaika na mradi wa maji wenye thamani ya Sh1.7 bilioni.

Lengo ni kuboresha maisha ya wakazi wa vijiji hivyo vilivyoathirika kutokana na maporomoko ya mawe, miti na matope na kusababisha vifo, majeruhi na kuharibika miundombinu.

Hayo yamebainishwa leo Jumanne  Septemba 3, 2024 mjini Babati na Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga kwenye hafla utiaji saini mikataba baina ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Vijijini (Ruwasa) na makandarasi.

Amewataka makandarasi watakaotekeleza miradi hiyo katika maeneo yaliyoathiriwa na maafa hayo kutekeleza kwa muda uliopangwa, kwa ubora unaotakiwa na kuishirikisha jamii ambayo ndiyo wanufaika.

“Tunatarajia mtafanya kazi nzuri kwa kuhakikisha inakamilika kwa wakati kwani Ruwasa mtawasimamia ipasavyo,” amesema Sendiga.

Ameishukuru Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa Sh9.4 bilioni za kuendelea kuwezesha urejeshwaji wa miundombinu na huduma za maji Hanang.

Meneja wa Ruwasa, Walter Kirita amesema kampuni mbili zimeshiriki kwenye miradi hiyo ya maji.

Amesema mkandarasi wa ujenzi ni Kampuni ya M/s Jisham & Construction na wa kutengeneza mabomba ni M/s Zongii.

Mkazi wa eneo la Jorodom wilayani Hanang’, Ezekiel Samo ameishukuru Serikali kwa namna ilivyowajali wakazi wake na kugharamia miundombinu hiyo ya maji.

“Baada ya kutokea maafa ya mwaka jana yaliyosababisha vifo na majeruhi, tunaona Serikali inavyotujali kwa kujipanga kutupatia maji kwani maji ni uhai,” amesema Samo.

Amesema wanatarajia mradi huo ukikamilika utakuwa na manufaa makubwa kwa jamii ya eneo hilo.

Related Posts