Wakulima walia bei ya kakao ikiporomoka

Mbeya. Wakati wakulima wa kakao Wilaya ya Kyela mkoani Mbeya wakishtushwa kushuka kwa bei ya zao hilo, wameiombwa Serikali kuboresha Mfumo wa Soko na Bidhaa (TMX) ili kumsaidia mkulima kunufaika.

Bei ya kakao ilikuwa imepanda hadi kufikia Sh32,171 kwa kilo moja kwa msimu wa kilimo 2023/24 na kwa mnada uliofanyika jana Jumatatu Septemba 2, 2024 kwa msimu wa 2024/25 imeshuka hadi kufikia Sh18,620 kwa kutumia mfumo wa TMX.

Awali, wakulima walionekana kufurahia bei hiyo lakini kwa sasa imeonekana kuwa tofauti baada ya mnada huo namba 40 uliofanyika wilayani humo kuwashtua wengi.

Mmoja wa wakulima hao, Zabron Mwakalukwa amesema ni mshtuko mkubwa kwa bei hiyo tofauti na matarajio yao kwa kuwa waliamini wanaweza kuuza zao hilo kwa zaidi ya Sh25,000 kwa kuwa walishafikia kiwango hicho.

“Tunaomba kama itawezekana turudi katika mfumo wa boksi, wanunuzi waweke bei yao kimyakimya, tuletewe aliye na bei ya juu, tumuuzie mzigo. Hii ya mnada wa watu kuonana ni kama wanategeana,” amesema mkulima huyo.

Naye Anna Wilbard amesema msimu huu wameuanza kwa ugumu na haikuwa matarajio yao huku akiitaka Serikali iangalie namna ya kuboresha zaidi ili kumsaidia mkulima kunufaika na kilimo.

“Inashtua na kusikitisha, lakini Serikali wanaweza kutoa msimamo kuhusu bei hii, tulijua tunapanda kumbe tunashuka zaidi, tunatumia gharama kubwa kuzalisha,” amesema Anna.

Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa Chama Kikuu cha Ushirika wilayani humo (Kyecu), Nabii Mwakyenda amesema zipo sababu kadhaa za kushuka kwa bei ya zao hilo ikiwamo uzalishaji wa kiwango cha juu kwa nchi za ukanda wa Afrika Magharibi.

Amesema pamoja na Tanzania kuwa na uzalishaji mzuri na zao kuwa bora, Serikali inaweza kuboresha mfumo wa TMX, badala ya wanunuzi kutumia mnada kutaja bei ana kwa ana wakaweka bei kimya kimya.

“Afrika Magharibi wamekuwa na uzalishaji mkubwa, hali iliyoathiri kwetu Tanzania, wateja wanaona bora kuchukua huko mzigo mkubwa na kiasi kidogo kutoka kwetu,” ameeleza.

“Serikali iliona faida kubwa katika mfumo huu wa TMX, wanachoweza kufanya ni kuboresha,  wateja wanaweza kuja na bei kimyakimya kuliko hii ya kusikilizana ana kwa ana,” amesema Mwakyenda.

Kaimu huyo ameongeza kuwa pamoja na changamoto hiyo, Kyecu wanaendelea kutekeleza maelekezo ya Serikali kwa kulipa malipo ya wakulima ndani ya saa 48 au pungufu yake na kufuatilia wanunuzi kuhakikisha wanalipa madeni yote.

“Kuhusu uzalishaji tunazidi kupiga hatua kwa sababu hadi sasa tumefikia tani 12,000 tunaendelea kuhamasisha wakulima kulima kwa tija na ubora na sisi Kyecu ni kuhakikisha wanapata haki yao,” amesema Mwakyenda.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyela, Florah Angelo amesema kushuka kwa bei ya zao hilo ni kutokana na uchache wa wanunuzi, akieleza kuwa, mkakati ni kutafuta wateja wengi ili kuleta ushindani.

Kuhusu kubadili mfumo huo, amesema hilo haliwezekani kufanya ununuzi nje ya mfumo kutokana na kuisaidia Serikali kujua kiwango kilichouzwa na kwamba atazungumza na Kyecu kuona namna bora ya kuboresha bei kwa kuongeza idadi ya wanunuzi kuweka ushindani wa bei.

“Ni kweli bei imeshuka na Serikali tunao mkakati wa kutafuta wanunuzi wa ndani hata nje ili kuwa wengi na kuweka ushindani, hatuwezi kufanya manunuzi nje ya mfumo huo kwa kuwa inasaidia kujua tumeuza kiasi gani, kikubwa ni kuweka wateja wengi kuliko kutegemea watu wawili,” amesema Florah.

Related Posts