Wananchi 62,000 kuwezeshwa kiuchumi Tanzania

Mbeya. Wakazi 62,000  wanatarajiwa kuingizwa kwenye mfumo rasmi na kuwezeshwa kiuchumi kupitia Programu ya Imarisha Uchumi na Mama Samia (Imasa).

Hatua hiyo imeelezwa kuyagusa makundi ya kijamii wakiwapo wazee, vijana na makundi maalumu ya watu wenye ulemavu watakaoingizwa kwenye mfumo rasmi wa kidigitali.

Katibu Mtendaji wa Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), Beng’i Issa amebainisha hayo leo Jumanne Septemba 3, 2024 wakati akiitambulisha programu hiyo katika ofisi ya mkuu wa Mkoa wa Mbeya ambayo iko chini ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa ya Serikali za Mitaa (Tamisemi).

“Mbeya ni miongoni mwa mikoa 14 ambayo imefikiwa na programu ya Imarisha Uchumi na Mama Samia, yenye lengo na kuwezesha makundi ya wazee, wanawake vijana na walemavu  kujikwamua kiuchumi ikiwa ni kutekeleza malengo ya Rais Samia Suluhu Hassan kuwafikia,” amesema Issa.

Amesema ili kufikia malengo yaliyokusudiwa, wanafanya tathimini za hali ya kiuchumi kuanzia ngazi za kata, vitongoji na vijiji kwa kulenga uwekezaji, urasilimashaji wa ardhi, bidhaa kupitia mwongozo wa mkakati wa kitaifa.

Issa amesema mwongozo huo utaleta tija katika utekelezaji wa programu hiyo sambamba na kushawishi Mkoa wa Mbeya kuanzisha vituo vya uwezeshaji wananchi kiuchumi.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera, Katibu Tawala wa Mkoa, Rodrick Mpogolo ameagiza wakurugenzi wote wa halmashauri kuanzisha vituo vya uwezeshaji wananchi kiuchumi.

“Majukwaa hayo yalenge kuwezesha wananchi katika nyanja mbalimbali ikiwamo sekta ya kilimo kwa kuanzisha viwanda na mitambo ya kuongeza thamani mazao ya kimkakati na mikopo rahisi kwa walengwa,” amesema.

Amesema programu ya uwezeshaji wananchi kiuchumi ikawe chachu ya uwekezaji kwenye viwanda vya kuchakata mazao ya kilimo na biashara ili kuleta matokeo mazuri na kufikia malengo ya Serikali ya awamu ya sita.

Mshiriki wa programu hiyo, Daudi Mrisho kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya ameishauri Serikali kuona namna bora ya kuwezesha vituo vya uwezeshaji wananchi kiuchumi.

Related Posts