WIZARA YA AFYA TANZANIA BARA, ZANZIBAR, CDC, WADAU WAJADILI UHARAKISHAJI WA UTEKELEZAJI WA MPANGO JUMUISHI WA WAHUDUMU WA AFYA NGAZI YA JAMII

Na. Elimu ya Afya kwa Umma.

KATIKA utekelezaji wa Mpango Jumuishi wa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii, Wadau wa sekta ya Afya kutoka Tanzania Bara na Tanzania Visiwani kwa kushirikiana na Shirika la Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa la Afrika (Africa CDC) pamoja na Wadau wengine leo tarehe 3, Septemba, 2024 wamekutana Jijini Dar es Salaam kwa ajili ya Kikao Kazi cha Kuandaa Mpango wa Kuharakisha Utekelezaji wa Mpango Jumuishi wa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii nchini.

Akizungumza wakatika wa ufunguzi wa Kikao hicho, Mkurugenzi wa Huduma za Kinga Wizara ya Afya kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Dkt. Salim Slim , amesema lengo la Kikao hicho ni kujadili masuala ya Uratibu kwa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii na kupendekeza utaratibu ambapo wadau wanaotekeleza afua zinazohusiana na Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii wataweka Mipango ya Utekelezaji.

“Tumekuja kuwekeza kwa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii katika kubadilisha mwenendo wa utoaji wa huduma, lazima tuwafundishe, tuwawezeshe, na tuhakikishe wanapata Stahiki nzuri ili watusaidie, kwa kweli Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na kule Zanzibar Dkt. Hussein Mwinyi wamejizatiti katika mstari wa mbele kulipeleka gurudumu la afya maana yake matatizo yote yanaanzia kulekule kwa jamii na kuyamaliza kulekule kwa jamii kupitia Wahumu wa Afya Ngazi ya Jamii” amesema.

Aidha, Dkt. Slim amesema dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kuwa maradhi yote ambayo yanaweza kuondolewa kwa chanjo yaondolewe na kikubwa ni kuhakikisha Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii wansaidia katika jamii.

“Chanjo zile za awali za mtoto na chanjo zingine kama vile Saratani ya Mlango wa Kizazi na afua zote za afya watakaosaidia katika utekelezaji wa afua hizi ni Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii na hivyo, tuhakikishe kuwa wanafika kila nyumba” amesema.

Kwa wake Afisa kutoka Mpango wa Taifa wa Huduma za Afya Ngazi ya Jamii Dkt. Meshack Chinyuli amesema kikao hicho kitaleta ufanisi katika utekelezaji wa Mpango Jumuishi wa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii.

“Kupitia Kikao hiki tutakuja na Mpango utakaoharakisha utekelezaji wa Mpango Jumuishi wa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii sambamba na kuongeza ubora na tija ambapo Wahudumu wa Afya watasaidia kwenye eneo la Afya, Lishe na Ustawi wa Jamii” amesema Dkt. Chinyuli.

Mwakilishi kutoka Africa CDC Dkt. Barnabas Yeboah amesema wanashirikiana na Serikali ya Tanzania katika kuhakikisha Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii wanatekeleza majukumu ipasavyo kwani wamekuwa na mchango mkubwa kwenye jamii katika kutoa huduma mbalimbali za afya ikiwemo mapambano ya magonjwa ya mlipuko huku akichukulia mfano namna Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii walivyojizatiti katika mapambano dhidi ya Mlipuko wa Ugonjwa wa Mpox .

“Sisi kama CDC tupo hapa kwa lengo la kusaidiana na Serikali ya Tanzania Bara na Visiwani na tafiti zinasema afya inaanzia ngazi ya kaya hivyo Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii wanapita kaya hadi kaya kutoa elimu ya Afya hivyo tunahakikisha kuwa tunaweka kipaumbele kwenye eneo la Afya Ngazi ya Jamii” amesema.

Mwakilishi kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto Duniani – UNICEF Dkt. Ulrika Baker amesema Shirika linafanya kazi na Serikali kulingana na vipaumbele vya Serikali. Aliongeza kusema kuwa, katika Ngazi ya Jamii mipango mbalimbali inaendelea kutekelezwa ikiwemo mapambano dhidi ya Malaria, Nimonia, Usafi wa Mazingira na usafi binafsi hivyo ni wakati mwafaka kwa Tanzania kuwa na Mpango Jumuishi wa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii.

“Hawa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii wamekuwa na msaada mkubwa katika masuala mbalimbali ya afya ikiwemo afya ya uzazi, Malaria, UKIMWI hivyo hatuwezi kukosa fursa ya watu hawa muhimu katika uboreshaji wa Huduma za Afya Ngazi ya Jamii” amesema.

Ikumbukwe kuwa, Mpango Jumuishi wa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii ulizinduliwa tarehe 31, Januari, 2024 na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Isdor Mpango. Kikao kazi hiki cha Kuandaa Mpango wa kuharakisha Utekelezaji wa Mpango Jumuishi wa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii kinahusisha Watalaamu kutoka Wizara ya Afya (Bara na Visiwani), Ofisi ya Rais TAMISEMI, Africa CDC, UNICEF, USAID, IRISH AID, Wawakilishi kutoka Umoja wa Afrika (AU) na Wadau mbalimbali ambapo kimeanza leo Septemba 3, 2024 hadi Septemba 6, 2024 Jijini Dar es Salaam.

Related Posts