Yametimia, Dabo afungishwa rasmi virago Azam

Bodi ya wakurugenzi ya Azam FC imefikia makubaliano ya pande mbili na aliyekuwa kocha wa Azam Fc Youssouph Dabo ya kutoendelea kufanya kazi naye kuanzia Septemba 3, 2024.

Taarifa iliyotolewa na idara ya habari na mawasiliano ya klabu hiyo imeeleza Dabo aliyehudumu kwenye kikosi hicho kwa mwaka mmoja na kuifanya timu hiyo kumaliza katika nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu Bara 2023/24 hadi kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika, ataondoka na benchi lake la ufundi ambalo lilikuwa na wasaidizi watano.

Dabo ataondoka na wasaidizi wake watano ambao ni kocha msaidizi Bruno Ferry (Ufaransa), kocha wa makipa Khalifa Babacar Fall (Senegal), kocha wa utimamu wa mwili Jean Laurent Geronimi (Ufaransa), mchambuzi wa video na wapinzani Ibrahim Diop (Senegal) na mchua misuli Ebrima Saine (Gambia).

“Dabo aliyehudumu kwa mwaka mmoja anaondoka na wasaidizi wake wa benchi ufundi aliokuja nao,” imesema taarifa hiyo na kuongeza kuwa Azam FC inamshukuru Dabo kwa muda wote aliokuwa kwenye klabu hiyo na pia inamtakia kila la kheri

“Klabu pamoja na wadau wake inapenda kumshukuru Dabo kwa weledi na moyo wake wa kutokata tamaa katika kipindi chote alichokuwa nasi, na tunamtakia kila la kheri.”

Aidha, bodi hiyo imesema wakati ikiwa kwenye mchakato wa kutafuta kocha mpya, timu ya Azam FC itakuwa chini ya makocha wa timu za vijana.

“Wakati bodi ikiwa kwenye mchakato wa kutafuta kocha mpya, programu za timu zitakuwa chini ya makocha wa timu za vijana.”

Related Posts