ZRA yatoa sababu kuvuka lengo makusanyo ya kodi Agosti

Unguja. Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA), imevuka lengo la makusanyo ya kodi kwa asilimia 102.34 kwa Agosti, 2024.

Kaimu Kamishna Mkuu wa ZRA, Said Ali Mohammed amesema leo Jumanne, Septemba 3, 2024 kwamba mamlaka hiyo imefanikiwa kukusanya Sh71.11 bilioni kati ya malengo ya kukusanya Sh69.49 bilioni.

Amesema makusanyo hayo yameongezeka jumla ya Sh13.87 bilioni sawa na asilimia 24.24 kutoka mwaka jana hadi kufikia mwaka huu.

“Ni wajibu wetu kutoa taarifa kwa wananchi ili kuona jitihada zao za kulipa kodi bila kushurutishwa na kuona fedha hizo zipo salama,” amesema Said.

Pia, amesema kuwepo kwa mazingira bora ndio sababu kuu ya kuongezeka kwa mapato katika mamlaka hiyo kwa kuwa,  bila ya mazingira wezeshi yaliyokuwepo wasingefanikisha hilo.

Amesisitiza kuwa, kwa wale wafanyabiashara ambao hawatoi risiti, wananchi wanapaswa kutoa taarifa kwa lengo kuchukuliwa hatua.

“Bado baadhi ya wafanyabiashara hawatoi risiti ni vizuri kutoa risiti kwa lengo la kufanikisha ulipaji kodi,” amesema.

Amesema Julai, mamlaka hiyo ilipangiwa kukusanya Sh50.49 bilioni na ilikusanya Sh53.32 bilioni ikiwa sawa na asilimia 105.

Mfanyabiashara eneo la Darajani, Ahmed Juma amesema faida ya ulipaji kodi inaonekana kutokana na maendeleo makubwa yanayofanyika ikiwamo kuboreshwa kwa miundombinu ya nchi.

Hata hivyo, amesema watu ambao hawatoi risiti wanapaswa kuchukuliwa hatua ili kila mmoja alipe kodi bila kushurutishwa.

Related Posts