Balozi Karume afichua kwanini hawezi kufukuzwa CCM

Miezi 14 baada ya kuvuliwa uanachama, mwanadiplomasia, Balozi Ali Karume ameendelea kusisitiza kwamba yeye ni mwanachama halali wa Chama cha Mapundizi (CCM) na hawezi kuvuliwa uanachama na “mdandia reli”.

Mwanasiasa huyo amekuwa kimya katika kipindi chote hicho tangu alipovuliwa uanachama wa CCM, kwa kile kilichoelezwa kuwa ni ukiukaji wa maadili na misingi ya chama kwa kumkosoa hadharani Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Rais Hussein Mwinyi.

Uamuzi wa kumfukuza uanachama ulitolewa Juni 8, 2023 saa 9:00 usiku na kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Kusini Unguja, chini ya Katibu wa Mkoa huo, Amina Mnacho.

Hatua hiyo ilifikiwa zikiwa zimepita siku 23 tu tangu Balozi Karume alipopewa barua ya onyo Juni 15, 2023 kabla ya kuibuka tena akisisitiza kauli zake kwamba hakuna demokrasia ndani ya CCM.

Kabla ya hatua hiyo, Karume alihojiwa na kamati ya maadili ya CCM tawi la Mwera, akahojiwa na kamati ya maadili ya CCM Jimbo la Tunguu na alihojiwa na kamati ya maadili ya CCM Wilaya ya Kati na kupewa barua ya onyo, akiwekwa chini ya uangalizi wa miezi mitatu.

Mwananchi limefanya mahojiano maalumu na Balozi Karume nyumbani kwake Maisara na amezungumzia mambo mbalimbali, ikiwemo hatima ya uanachama wake wa CCM, Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) na ushauri wake kwa Rais Mwinyi.

Akizungumzia uanachama wake, Balozi Karume anasema yeye ni mwanachama halali wa CCM na hakuna mtu wa kumfukuza katika chama hicho kwa sababu yeye ni miongoni mwa waasisi wake.

Anasema aliwaeleza kuwa utaratibu uliotumika kumfukuza kwenye chama hautambuliki.

“Mtu anafukuzwa kwenye chama kwa kuandikiwa barua na kuambiwa ‘rejesha kadi yetu’, lakini siyo kutangaza kwenye vyombo vya habari. Mimi sijawahi kupata barua na kadi yangu ninayo,” anasema Balozi Karume.

Anasisitiza kwamba: “Mimi ni mwasisi wa Chama cha Mapinduzi, siwezi kufukuzwa kwa utaratibu huo.”

Mwanadiplomasia huyo anasema chama hicho kina wanachama wa aina mbili, wanachama waasisi na wadandia reli, hivyo yeye kama mwasisi, hawezi kufukuzwa na mdandia reli.

“Mdandia reli hawezi kunifukuza kwenye chama kwa sababu mimi ni mwasisi wa Chama cha Mapinduzi.

“Wakati tunaunda chama hiki kutoka Afro Shiraz (ASP) kwenda CCM, wanaotaka kunifukuza walikuwa na umri wa miaka 10 na mwezi mmoja, sasa atakuja vipi kunifukuza chama?” anahoji Balozi Karume.

Kutofikiwa malengo ya SUK

Kutokana na ghasia zilizokuwa zikitokea kila baada ya uchaguzi, hususan uchaguzi wa mwaka 2000, Rais wa wakati huo, Amani Abeid Karume alianzisha mazungumzo na kiongozi wa upinzani, Maalim Seif Sharif Hamad ambayo baadaye yalizaa SUK.

Katiba ya Zanzibar ilifanyiwa marekebisho mwaka 2010 kuruhusu kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa inayokihusisha chama cha upinzani kilichopata kura zaidi ya asilimia 10 katika kuunda serikali.

Kwa sasa, CCM na ACT Wazalendo vimeunda Serikali na ACT Wazalendo wamepata nafasi ya Makamu wa Kwanza wa Rais na nafasi mbili za mawaziri katika serikali hiyo, huku kukiwa na mvutano wa mara kwa mara kuhusu uendeshaji wa serikali hiyo.

Akizungumzia uendeshaji wa SUK, Balozi Karume anasema malengo ya kuanzishwa kwake bado hayajafikiwa, akidai bado kuna mambo ya kikatiba hayajakaa sawa na wapinzani wanataka yamalizwe badala ya kuipalilia SUK.

Balozi Karume anasema Waingereza waliunda serikali ya mseto wakati wa vita, lakini waliheshimu makubaliano yao na wakajiondolea dhana ya upinzani kwa sababu wote wapo kwenye serikali moja.

Lakini kwa Zanzibar, anasema licha ya kuwa ni SUK kwa makubaliano yaliyomo kwenye Katiba na sio sheria kama ilivyokuwa Uingereza, bado wapinzani hawathaminiwi na kuheshimika kama sehemu ya Serikali.

“Jambo lililotiwa kwenye Katiba na inaeleza kwamba chama ambacho kimepata kura asilimia 10 au zaidi ndiyo kinamtoa Makamu wa Kwanza na viti vya uwakilishi angalau kimoja.

“Iwapo CCM wakishinda kwa asilimia 81, wapinzani watalalamika, lakini watakuwa hawaingii tena katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa kwa sababu Katiba inasema isiwe chini ya asilimia 10,” anasema.

Balozi huyo mstaafu anasema ilani ya CCM itekelezwe kwa kushirikiana na wapinzani kwa kuwa tayari wapo serikalini, wakipinga jambo wasikilizwe, lakini siyo kuwaona hawana maana.

Katiba na siasa za kufariji

Balozi Karume anasema masuala ya uchaguzi ni mambo ya siasa na yanakwenda na Katiba, hata hivyo anasema yeye siyo muumini wa Katiba mpya.

Anasema anapendelea zaidi siasa za kufariji ili watu wajisikie vizuri kuliko watu kujiona wapo kwenye hatari.

Hivyo, anasema ni vema Katiba ikafuatwa badala ya kutumia nguvu na mabavu, huku akisema wakati mwingine huwaweka wagombea ambao hawana sifa, ila ni kwa sababu ya utashi wa watu fulani.

Katika hilo anakiomba chama chake, CCM kubadilika na kuzingatia matakwa ya wanachama badala ya kuacha uwe ni uamuzi wa watu wachache.

Anasema kuna haja ya kuwa makini wanapoteua wagombea wanaokubalika kwa wananchi. Anasema imeshuhudiwa wakati mwingine CCM ikiteua wagombea wasiokubalika kwenye baadhi ya maeneo, lakini wanabebwa na mifumo.

“Siyo tu tunakwenda na fulani, toa sababu zako kwa nini unaona huyu unayemsema anafaa,” anasema Balozi Karume.

“Kama anajitokeza mtu kwamba alikuwepo kwenye shughuli hizo lakini alikatwa jina na hajui alikatwaje, ni vema akapewa fursa waende wakazungumze kwenye kamati kuu. Wakisema fulani naye kachukua fomu wamjadili wakubali kila mmoja apewe fursa na apewe haki ya kikatiba.

Balozi Karume anasema akipata nafasi ya kukutana na Rais Mwinyi atamshauri kupunguza kukopa kwa sababu hakuna nchi iliyoendelea kwa mikopo, bali ni mzigo kwa wananchi wanaokwenda kuulipa.

“Kama ningekuwa na uwezo wa kumshauri Rais, ningesema hebu kwa kipindi hiki cha miezi sita tusichukue mkopo wa aina yoyote, kwanza tuangalie mikopo tuliyochukua tutafika wapi,” anasema.

Hata hivyo, anasisitiza kuwa bado ni mazungumzo ya kitaifa kuhusu mikopo hiyo, haijafikia kuwa mjadala wa kitaifa, ukifikia huko, anasema lazima wakumbuke kwamba hakuna nchi hata moja duniani imeendelea kwa mikopo.

Ametolea mfano uchumi wa Marekani unaoelekea dola 29 trilioni lakini wanadaiwa dola 30 trilioni, maana yake Wamarekani wote kwa mwaka mzima wanafanya kazi, lakini mapato yao yanaishia kwenye kodi na itawachukua mwaka mmoja na miezi minne kulipa mkopo wote.

Balozi Karume anasema nchi haiwezi kuendesha miradi yake kwa mgongo wa wawekezaji, akidai hakuna nchi hata moja duniani inayoweza kusema kwamba uchumi wake umejengwa na wawekezaji.

“Uwekezaji wote ule ni wa kwao, wanaendesha na kusimamia wao na sio ya Serikali tena na mkilala usingizi ndio mmekwisha,” anabainisha.

Kwa mantiki hiyo, anasema wawekezaji siyo watu wa kutegemea kwamba watakuletea maendeleo ya uchumi, bali ni maendeleo yao na katika balance sheet wanazidi kuwa matajiri na matajiri zaidi.

“Utajiri wao unaongezwa kwa ardhi yenu mliyowapa bure, mnampa mwekezaji ekari 80 za ardhi afanyie biashara, jiulize.

“Mimi siyo muumini wa uchumi wa nchi kujengwa na wageni na pia kwa mtaji wa kigeni, hiyo siyo strategy ya Economic Development (mkakati wa maendeleo ya uchumi),” anasema Balozi Karume.

Tathmini miaka mitatu ya Mwinyi

Balozi Karume, ambaye ni mtaalamu wa uchumi, anakiri kwamba yapo mambo makubwa yaliyofanywa katika serikali ya awamu ya nane, lakini zimetumika gharama kubwa, tena kwa fedha za mikopo, jambo analosema kitaalamu halina afya njema kwa uchumi.

“Mtu akija akiniambia amejenga nyumba 10 kwa gharama ndogo kuliko aliyejenga nyumba 20 kwa gharama kubwa zaidi ya mara tatu, bora huyo aliyejenga nyumba kidogo lakini kwa gharama za chini,” anasema.

Anasema bajeti ya Zanzibar ya mwaka 2024/25 imefika Sh4.9 trilioni, fedha zinazoweza kufanya mambo mengi lakini kwa mizigo ya mikopo, yeye haamini katika hilo kwa sababu mkopo ni harusi, lakini kulipa ni matanga.

Balozi Karume anafafanua kuwa ikifika wakati wa kulipa, vizazi vijavyo vinaweza kulalamika kudai walikuwa wapi wakati mikopo hiyo inachukuliwa.

Kwa mujibu wa mwanadiplomasia huyo, unaangalia uwezo wako wa kulipa kabla ya kuchukua mikopo na wachumi wengi wanaamini kwamba kwa kuwa watu wanafanya kazi katika nchi na uchumi unazidi kukua, unakopa kwa kuwa utaweza kulipa, lakini ni tofauti. “Mimi simo katika kundi la wachumi hao, mimi nasema walipaji wa mikopo ya Taifa ni wananchi walipakodi, siyo mzigo wa Taifa, ni mzigo wa wananchi.

“Ni kweli yapo maendeleo tumeyaona na nia nzuri ipo sikatai, lakini mimi sipendelei maendeleo makubwa kwa gharama kubwa ya kupindukia,” anasema

Katika kulifafanua hilo, ameeleza aina ya mikopo, ikiwemo inayotoka katika mashirika ya kimataifa, nchi na nchi ambayo ukishindwa kulipa unazungumza nao kidiplomasia na wanaweza wakatoa ruzuku.

Kadhalika, anataja mikopo mingine ni ile ya benki za biashara ambazo zinahitaji riba kubwa kwa sababu zinataka faida kujiendesha kibiashara.

“Mchumi kama mimi naamini kwamba huwezi kwenda kuweka rehani pato la serikali la mwaka ujao kwenye bajeti, kwenda kufanya shughuli mbalimbali. Wakati unapata mkopo, bajeti yako ikipata nakisi unazidi kukopa, kwangu mimi hili naona sio rai nzuri,” anasema.

Balozi Karume anasema licha ya kwamba anayakubali yote kwenye 4R za Rais Samia, lakini ustahimilivu (Resilience) ni kitu ambacho anakikubali hata katika maisha yake binafsi, kwani ni mstahimilivu.

“Ukiona watu wapo kwenye msimamo fulani na wakakupa sababu zao unatakiwa kuwa resilient (mstahimilivu) ili usiwavunje moyo,” anasema.

Kwake yeye, anasema hayo mambo mengine ni ya kawaida, lakini hili la ustahimilivu analikubali zaidi na yeye ni muumini wake.

Related Posts