Kufuatia matokeo hayo, viongozi wa chama cha AfD, Alice Weidel na Tino Chrupalla, wanataka wapatiwe nafasi kwenye serikali za majimbo hayo, wakidai kupewa idhini na wapiga kura kwa ajili ya kuunda serikali ya mseto inayokijumuisha chama chao na chama cha kihafidhina cha CDU. Yenyewe CDU imekataa uwezekano wowote wa kuingia kwenye serikali na AfD.
Hata kabla ya uchaguzi huo, tayari vyama vya wafanyakazi na wawakilishi wa wafanyabiashara walishaelezea wasiwasi wao juu ya uwezekano wa kuporomoka kwa uchumi endapo AfD ingelishinda, kwani wawekezaji wanaweza kuogopa kuwekeza mitaji yao kwenye mazingira ya uhasama na yasiyo utulivu.
Soma pia: Wajerumani weusi wahofia ushindi wa AFD majimbo ya mashariki
Olaf Zachert, mwekezaji aliyejikita kwenye kuyaokowa makampuni yenye hali mbaya, alionya kwamba mitaji ni kama paa mwenye haya, na wawekezaji huwa hawawekezi kwenye maeneo ambayo wanajihisi hawakaribishwi. Aliiambia DW kwamba kuongezeka kwa uungwaji mkono wa AfD kunawafanya wawekezaji wengi kufikiria mara mbili kabla ya kuelekeza mitaji yao kwenye majimbo ya Saxony na Thuringia.
Makundi ya ushawishi wa kibiashara na wachumi washtushwa
Siku moja baada ya uchaguzi kufanyika, rais wa chama cha waajiri cha Ujerumani, alizungumzia mafungamano yaliyopo baina ya uchumi na siasa, akisema kwamba kuimarika kwa AfD kunaakisi wasiwasi mkubwa wa jamii na kupotea kwa imani kwamba Ujerumani imeshika njia sahihi.
Kwa rais huyo wa waajiri, kwa kiasi fulani sera za sasa za Kansela Olaf Scholz zimechangia kuwafanya Wajerumani waelekee zaidi kwenye siasa za mrengo wa kulia na alimtolea wito kuwa lazima serikali yake ya mseto wa vyama vitatu ipitie upya sera zake, kwani “serikali yoyote inapaswa kuzingatia utangamano wa kijamii.”
Matokeo ya uchaguzi huu yanatazamiwa na wachumi kuwa yataongeza upungufu wa wafanyakazi na vibarua katika maeneo ya mashariki mwa Ujerumani, na hilo litapelekea makampuni mengi kuhamisha shughuli zao.
Soma pia: Scholz akiri matokeo yaliyokipa ushindi chama cha AfD yanatia wasiwasi
Monika Schnitzer, anayeongoza Baraza la Wataalamu wa Uchumi la Ujerumani, anasema makampuni yanayotokea Thuringia na Saxony yanaweza kupoteza fursa kwenye ushindani wa kilimwengu panapohusika suala la wafanyakazi wenye sifa.
Taasisi za kiserikali na za kielimu tayari zinakabiliana na upungufu mkubwa wa wafanyakazi, ambao utaongezeka kutokana na msimamo wa AfD dhidi ya wahamiaji wenye maarifa ya kazi.
Uwekezaji muhimu kwenye hatari?
Wasiwasi kama huu umetajwa pia na rais wa Taasisi ya Utafiti wa Uchumi ya Ujerumani, Marcel Fratzscher, ambaye ametabiri kupunguwa kwa ajira na uwekezaji wa kigeni. Anahoji kwamba sera za AfD zinazopigia chapuo ulinzi wa biashara na upunguzaji wa wahamiaji, uwazi na mchanganyiko, zitapelekea moja kwa moja ukimbiaji wa makampuni na wafanyakazi wenye uwezo. Matokeo ya hayo na makampuni kufilisika na kuhamia mahala kwengine.
Kwa maneno ya Fratzscher, raia vijana na wenye uwezo zaidi watayakimbia majimbo haya mawili na kuelekea kule ambako wanajihisi kuwa wanathaminiwa.
Soma pia: Vyama rafiki na Urusi Ujerumani vyapata mafanikio
Mkurugenzi wa Taasisi ya Uchumi ya Ujerumani, Michael Hüther, anasema kuja juu kwa AfD si ishara njema kwa sababu wafanyabiashara daima huhitaji utulivu wa kisiasa na kitaasisi.
Anahoji kwamba sera za kijamii pekee hazitoshi kuwafanya wapiga kura kuacha kuunga mkono siasa za hamasa, badala yake ni kuwa na uwekezaji wa kimkakati ambao unaweza kuzuwia kuporomoka uchumi.