Che Malone, Hamza kuna kitu

WANASEMA nyota njema huonekana asubuhi. Hiyo imejitokeza mapema sana ndani ya kikosi cha Simba kinachonolewa na Kocha Msauzi, Fadlu Davids. Unajua imekuwaje? Soma hapa.

Simba ambayo imeuanza msimu huu kwa ushindi wa asilimia 100 ndani ya Ligi Kuu Bara, kuna kitu bado kinaonekana hakijamridhisha Fadlu kiasi cha kumfanya akune kichwa.

Ukiangalia katika mechi hizo mbili ambazo Simba imecheza dhidi ya Tabora United na Fountain Gate, timu hiyo imeondoka na clean sheet zote kwa maana ya haijaruhusu nyavu zake kutikiswa.

Hicho ni kitu kizuri lakini Fadlu hajaridhika licha ya kwamba safu yake ya ulinzi ikiongozwa na Che Malone Fondoh na Abulrzack Hamza ikipambana kwa kushirikiana na viungo anapocheza Fernandes Mavambo na wenzake.

Kinachomuumiza zaidi kichwa Fadlu ni namna uchezaji wa timu yake ambapo anaiona haijawa na nidhamu ya kukaba kiasi cha kumpa wasiwasi mbele ya safari itakuwaje kama hali hiyo itaendelea.

Wakati Fadlu akiyasema hayo, rekodi zinaonyesha kwamba Simba tangu katika Tamasha la Simba Day mpaka sasa, imecheza jumla ya mechi sita, nne za kimashindano na mbili za kirafiki ikiruhusu mabao mawili na kufunga 11.

Katika mechi hizo sita, Mwanaspoti limebaini kwamba Fadlu anapowatumia Che Malone Fondoh na Abdulrazack Hamza huku Fernandes Mavambo akiwa kiungo cha chini timu hiyo haijaruhusu bao, lakini ikiwa tofauti kuna shida inaonekana.

Ipo; Pacha ya Che Malone, Hamza na Mavambo imecheza mechi tatu na zote imeondoka na clean sheet, ilikuwa hivi; Simba 1-0 Coastal Union, Simba 3-0 Tabora United na Simba 4-0 Fountain Gate.

Katika mechi ambazo Simba imeruhusu bao, mabeki wa kati wamecheza Che Malone na Chamou Karaboue, lakini pia ipo waliocheza Chamou Karaboue na Abdulrazack Hamza. Katika kiungo anakuwepo Mzamiru Yassin.

Mchezo ambao Simba ilifungwa bao 1-0 na Yanga katika Ngao ya Jamii, alikuwepo Che Malone aliyecheza sambamba na Karabou huku Mavambo akiwa kwenye kiungo. Bao hilo lililofungwa na Maxi Nzengeli dakika ya 44, zilipiga pasi za haraka eneo la kati huku wachezaji hao wakishindwa kuzuia shambulizi hilo.

Lakini pia katika mchezo wa hivi karibuni wa kirafiki ambao Simba ilitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Al Hilal, Fadlu alianza na Chamou, Che Malone kisha Mavambo akiwa kwenye kiungo. Kipindi cha kwanza Simba ikamaliza ikiwa mbele kwa bao 1-0.

Kipindi cha pili, Fadlu alifanya mabadiliko kadhaa ambapo Mavambo alitoka na kuingia Mzamiru, kisha Che Malone akampisha Hamza, dakika ya 76 wakajikuta wakiruhusu bao likionekana tatizo ni kushindwa kukaba.

Bao hilo lilitokana na kupigwa pasi mbili pekee kutoka eneo la Al Hilali kwani Simba ilikwenda kushambulia, wapinzani walipoupata mpira wakatumia udhaifu waliouona na kufunga. Hiyo inatoa picha kwamba mpaka sasa Che Malone, Hamza na Mavambo wakicheza pamoja Simba inakuwa salama zaidi, lakini akikosekana hata mmoja shida inatokea.

Akizungumzia maendeleo ya kikosi chake, Fadlu amesema: “Tunatakiwa kuwa timu inayopeleka presha kubwa kwa wapinzani wanapokuwa na mpira, hili bado halijakaa sawasawa kwetu, kuna wakati tunafanya vizuri na wakati mwingine tunafanya makosa.

“Ukiona lile bao ambalo tuliliruhusu dhidi ya Al Hilal utapata picha halisi ya kipi nakizungumza, Simba haitakiwi kufanya makosa kama yale ili tuwe salama.”

Katika hatua nyingine, Fadlu amesema licha ya kwamba wamefunga mabao mengi, lakini wanashindwa kuzitumia vizuri nafasi wanazotengeneza.

“Mpaka sasa bado kikosi hakijafanya sawasawa kwenye matumizi ya nafasi ambazo tunatengeneza kwenye mechi zetu ili kupata matokeo makubwa, kama tungekuwa vizuri eneo hilo tungepata mabao mengi zaidi.

“Tunahitaji pia kufunga mabao ya kutosha, naelewa kuna mechi ambazo tutakuwa na nafasi chache lakini kuna mechi ambazo kama tunatengeneza nafasi za kutosha tunatakiwa kutamani ushindi mkubwa wakati wowote.

“Hili linaenda sambamba na kumaliza mechi mapema, kama tutatumia nafasi hizo mapema, mechi ambazo tunakwenda kucheza ni za mtoano unatakiwa kutengeneza ushindi mzuri ugenini na nyumbani, haya yote lazima tujiandae nayo haraka sasa,” alisema Fadlu.

Simba kwa sasa inajiandaa na mechi mbili za Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Al Ahli Tripoli ya Libya ambapo mchezo wa kwanza utapigwa ugenini Septemba 13, mwaka huu kisha marudiano nyumbani Septemba 20.

Related Posts