Huyu ndiye Babu Duni usiyemjua

Zanzibar. Septemba 4, 2024, Juma Duni Haji, maarufu Babu Duni ametangaza kustaafu siasa.

Ameagwa kwa heshima na chama chake cha ACT-Wazalendo.Katika hafla hiyo ya kumuaga, mwanasiasa mkongwe wa chama hicho, Ally Saleh maarufu Alberto amesoma wasifu wa Babu Duni ambaye kwenye safari yake ya kisiasa imekuwa ya kupanda na kushuka.

Unajua Babu Duni amewahi kuwa mchezaji wa mpira, undani wa jina la Duni katika ukoo wake. Akiwa mwalimu amewafundisha wengi akiwamo Rais Samia Sulu Hassan.

Soma wasifu huo kama ulivyoandikwa na Alberto na kuusoma yeye mwenyewe.

Si rahisi kwa usiku mmoja kwa mtu yeyote yule kuweza kuandika na kuwasilisha kwa ufasaha wasifu wa mtu na mtu mwenyewe ni mwanasiasa, mwalimu, mtu wa watu, mtu mwenye ushawishi, mwenye haiba na ambaye amejaa ndani ya nyoyo za watu aliokuwa sehemu ya kuwaongoza kwa miongo mingi-kupitia siasa, ualimu na uongozi kwa jumla.

Juma Duni, Wazungu husema, amekuwa ni household name hapa kwetu Zanzibar na Tanzania nzima na jina la Babu linamiliki ya brand yake hivi sasa.

Ukitaja jina Babu katika shughuli inayohusu siasa kwa chinjo au nukta moja basi kinachokuja akilini ni Juma Duni, jina la ukoo Duni humaanisha ni yeye.

Babu Duni ataacha alama kubwa katika historia ya nchi hii na njia aliyopitia hadi leo kwa hakika haitaota majani maana itaendelea kupitiwa kwa miaka mingi mno.

Na kitendo hiki cha kumuenzi na kumshukuru kwa michango yake kwenye siasa, kitaacha alama kubwa na wazo hili la kumuenzi kwa hakika litakuwa ni halali yake kwa jinsi alivyojitoa na Wazungu husema ni a very selfless person na mtu wa watu yaani man of the people.

Mwaminifu, mpenda haki, mkweli, asiye na kinyongo – siku zote japo amekuwa na kauli thabiti na sauti kali na ya kishindo lakini hakuwa na makeke katika utendaji wake wa siasa.

Na ndio maana unaweza kumkusanyia Duni sifa za wanasiasa wakubwa duniani, kati hakuwa mjivuni kwa karma kuwa na uwezo wa kujenga hoja, kushawishi na hata kuburura watu kama yule Mpiga Filimbi wa Hamalin.

Uwezo wake wa kushawishi na kujenga hoja. Uwezo wa kuzungumza na kila rika. Uwezo wa jambo gumu kulieleza kwa urahisi. Na akiona mnapotea hukurudisheni katikati ya kilenge kwa msemo wake maarufu wa Ohaaa!

Babu Duni (73) ni mtu wa stori na mikasa. Humfaidi mpaka uwe karibu nae.

Muda wote, hata katika wakati ambao hakueleweka, alibaki katika msimamo wake na hakuhitaji kujitetea bali alijaribu kujenga hoja ili aeleweke. Na imekuwa ni vigumu kutomuelewa Babu Duni, na itakuwa wewe ndio hueleweki. Na matukio ya kutoeleweka hayakuwa haba.

Kwa mfano kuna wakati alipata msukosuko akiwa serikalini, kwa kuamuru mchele upelekwe Pemba kwa kuwa kulikuwa na uhaba uliokuwa ukipelekea kuwepo na njaa.

Na bahati mbaya jahazi moja kupotea. Alichowaambia wakubwa wake ni kuwa alilazimika kufanya hivyo ili kufanikisha mambo mawili.

Kwanza kuwaokoa wakazi wa Pemba na njaa kwa vile usafiri wa meli za Serikali ulikuwa na ugumu, lakini pili kuiepusha Serikali na lawama hasa ya kisiasa. Alieleweka.

Uamuzi mwingine mkubwa alioufanya alipokuwa sekta ya biashara miaka hiyo na kwa maneno ya mjini na wala hajisifu…ni pale alipomkabili Waziri Kiongozi Maalim Seif na kumpa fikra kuwa wakati umefika kwa Serikali kuruhusu wafanyabiashara na watu wenye fedha waruhusiwe kuleta bidhaa na vyakula…na YUMKINI hii ndio ilojenga Sera ya Uwazi wa biashara yaani LIBERALIAZATION chini ya Rais Ali Hassan Mwinyi.

Pia, alihusika kuiokoa Serikali kukwama katika uuzaji wa karafuu alipokuja na fikra ya kubadilishana bidhaa na Serikali kununua magari kwa kubadilishana na karafuu. Magari hayo yalihitajika kuimarisha huduma za kilimo.

Kuna mara kadhaa Babu Duni alitumia kipawa chake akichanganya pamoja na nyota ya kuaminiwa kwenda exra mile kutimiza wajibu wake.

Kama kwa mfano palipokuwa na shida ya maji hospitali ya Mnazi Mmoja na akapiga hodi kwa Bwana Said Salim Bakhressa kwenda kuomba fedha ili atengeneze mfumo kuikoa hospitali hiyo isiwe kaburi la vifo kwa uchafu.

Na bila ya kuwa anamjua Bakhressa alimuamini na akapewa Sh100 milioni. Na huwezi kuamini fedha zilizotumika zilikuwa ni Sh5 milioni tu. Kiasi kilichobaki kikatumika kununulia dawa.

Au pale aliposimamia kujengwa kitengo cha dharura ICU hapo Hospitali ya Mnazi Mmoja na Waziri wa Fedha wakati huo Omar Yussuf Mzee alipompiga danadana hata baada ya kauli ndani ya Baraza la Wawakilishi kutoa fedha…Babu Duni alipeleka barua ya kujiuzulu, lakini Maalim Seif akaizuia isimfike Rais…. Fedha zikatolewa.

Au tukio la Chama cha Wananchi (CUF) kukaribia kushindwa kupata fedha za kufanya Mkutano Mkuu.

 Ilifika siku Babu alimuelekea Mola wake kwa sala za usiku…na siku ya pili akapata rai iliyopelekea chama hicho kupata Sh300 milioni za mkopo.

Na bahati iliyoje kwa njia zake Maalim Seif akatia kapuni Sh200 milioni kutunisha na kufanikisha mkutano huo.

Ni rahisi kusema kuwa Duni kwa siasa za Zanzibar na Tanzania ….AMEKUWA ni GIANT. Kama mwanamuzki angekuwa MAESTRO na kama ni kabumbu angekuwa ni GOAT.

Yeye si dictionary au kamusi la siasa ile ni THESAURUS.

Mambo ambayo ameyafanya wakati mwingine unaweza kusema aliishi maisha zaidi ya mamoja. Ukitizama nafasi ambazo amehudumia na uzoefu alokusanya ni CHUO KAMILI CHA UONGOZI.

Historia yake imejaa misukosuko na misokotano na ukinzani wa mambo kadhaa. Bila shaka mtoto huyo aliyepata fursa ya kusoma kwa bahati tu kuwa alitakiwa amsindikize jamaa yake Almarhum Jecha Salim Jecha kwa kuwa alikuwa ni mdogo zaidi na skuli ilikuwa mbali.

Na aliyetapia maisha yake kutokana na kuanguka kutoka mpapaini na kuzima kwa dakika kadhaa, kisha akaangukiwa na ndizi iliyoongoka na kumtisa vibaya mwili wake wa kitoto.

Alikuwa mtundu mtundu kwa kiasi chake…japo sote utoto wetu ulikuwa na visa na mikasa

Duni, ambaye alizaliwa (Novemba 26, 1950) kutoka familia masikini, alijua mapambano ya maisha mapema sana kwani alikuwa akibeba sinia ya maandazi ya mama yake ili kutafutwa kijio cha kila siku na kwenda na maandazi hayo mpaka skuli…mengine akapangiwa kuwa ni lunch yake.

Lakini alikuwa hodari na ikawa rahisi kuingia sekondari huko Gamal Abdul Nasser – Beit El Ras na kisha Skuli ya Lumumba Darasa la 13 na 14.  Na akarudi tena baadaye kusomesha Lumumba na katika watu maarufu aliowasomesha ni pamoja na Haroun Ali Suleiman – Waziri wa Katiba na Sheria- Samia Suluhu Hassan, Rais wa Tanzania,  Ismail Jussa – Makamu Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo na Dk Naufal Kassim ambaye mchango wake wa utabbu ni mkubwa sana… kati ya wengi wengine.

Kwa faida ya vijana wetu, Babu Duni alikuwa mpiga ngozi mzuri na alichezea timu ya Daraja la Kwanza, sawa na ligi kuu ya sasa ya Mwembeladu maarufu kama kubwa lijalo… na alikuwa mkata mawasiliano mzuri sana.

Pengine kwa sasa Yanga na Simba zingemuwania lakini naamini angechagua Yanga…. Kama Uingereza angewakataa wajivuni wa Manchester na pia wanaojiita miamba ya London Arsenal na Liverpool…angechagua New Castle United.

Ni katika kipindi cha masomo yake ya Sekondari ndipo aliposhawishika kuingia katika siasa na kugombea na kushinda uongozi wa Afro Shirazi Party Youth League na kukulia katika harakati za Mapinduzi na akawa ni muumini mkubwa wa itikadi ya ASP na Mapinduzi ya 1964 kwa sababu yalidhamiria kutetea haki, umoja na mashiirkiano  na kuundwa kwa Serikali ya Wakwezi na Wakulima.

Lakini Duni amekuwa mkosoaji mkubwa wa Mapinduzi kuendewa kinyume.

Babu Duni alibahatika kuwa katika kundi kubwa la Wazanzibari waliopelekwa kwenda kusoma Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Rais Aboud Jumbe ambapo alikuja na utaratibu wazi zaidi ya kuongoza nchi na alipenda wasomi washike nafasi kinyume kabisa na Father K au Rais Abeid Karume.

Kundi lao lilikuwa na kina marehemu Abubakar Khamis, marehemu Maalim Seif Shariff Hamad, Waziri na Mwanasheria Mkuu marehemu Idd Pandu Hassan, Balozi Muhammed Mwinyi Mzale na wengine.

Babu Duni siku zote katika maisha yake amekuwa mtu ambaye ni committed katika misimamo yake katika kundi ambalo yuko pamoja nalo, kama kwenye vyama vya siasa- ambavyo hadi leo ni CUF na ACT na husimamia maamuzi ya pamoja. 

Aliwahi kukataa ofa ya kupewa ubalozi aliyopewa na mjomba yake Salmin Amour ili awachane na upinzani. Akakataa.

Babu Duni amekaa jela mara mbili. Katika kesi ya uhaini na ya kudaiwa kumuua askari Pemba. Na hilo limemsumbua sana maana hata baba yake alikaa jela kwa madai ya kutaka kumdhuru Rais Karume wa mwanzo kwa njia za kilozi kama wasemavyo Wakongo yaani kichawi.

Alhmdullila Babu Duni amekuwa mgombea mwenza mara kadhaa kwa kufuata matakwa ya chama hata ilipobidi kuumiza masilahi yake kwa sababu siku zote amekuwa mtii wa chama chake na muumini wa maamuzi ya pamoja.

Amekwepa na anakwepa tashwishi kadhaa za kusaliti wenziwe kama vile alivyofuatwa ili ajitangaze kuwa mgombea dhidi ya Maalim Seif wakati wa Rais Mkapa na akakataa kwa sababu ya uaminifu unaotembea ndani ya damu yake….na sasa naamini hatakubali ushawisi wowote wa kuipa mgongo ACT maana nafsi yake haitakubali hata kidogo.

Tanzania political history itamkumbuka na kumuenzi kwa uamuzi huo, ambao naamini ulikuwa mgumu lakini aliufanya kwa sababu ACT sio imo ndani ya moyo wake, bali ACT ni moyo wake yaani ACT is his beating heart.

Leo tunaandika historia kubwa nchi hii kwa tukio hili…tunajenga utamaduni mpya na kigezo kipya. We are writing history and setting a new landmark.

Zitto Kabwe, kiongozi mstaafu wa chama katika makala kwenye THE CHANZO kushereheke maisha ya Babu Duni anamtaja kuwa na MOYO MKUBWA aliporidhia Bwana Othman Masoud apitishwe kuwa mrithi wa Hayati Maalim Seif.

Nilivyotiririka itaonekana kama namjua Babu Duni sana. Hapana. Nilianza kumjua kwa undani nilipojiunga kwenye kampeni ya uchaguzi wa chama kujaza nafasi ya Maalim Seif tena nikawa mshauri wake.

Kisha tukaja kampeni ya Uchaguzi Mkuu wa mwezi Machi, ambapo nataka nitoe ushuhuda wa MOYO MKUBWA tena wa Babu Duni baada ya tishio la kuonekana kutakuwa na mpasuko kwa sababu ya joto la uchaguzi.

Aliamua kujitoa na kumpisha Bwana Othman siku tano kabla ya uchaguzi na kututaka timu yake ya kampeni tutayarishe barua na hotuba.

Tulipomuuliza kwa nini asitoe jina lake mapema alisema, kwanza alitaka autumikie uenyekiti wake miaka mwisho lakini pili alisema, “wacha chama kijenge uzoefu wa mitikisiko ili tujenge uimara wake.”

Hivyo ndivyo alivyo Duni muumini wa mjenzi wa taasisi imara. Akatuvusha. Tuko salama na tunajipanga kwa ushindi.

Ndio maana leo tukimuenzi tunamchukulia Juma Duni Haji maarufu Babu Duni kuwa mmoja wa wanasiasa wetu ambao wataishi milele na vizazi kwa vizazi vitamtaja  kumuenzi na kumuimba.

Ila Babu haondoki. Yupo kwenye Kamati ya Uongozi na Bado yupo yupo kwenye mapambano nasi.

Natamani kusoma kitabu chake mwaka huu au mwakani Inshallah. Tuone utajiri wa maisha yake, si wa fedha bali wa moyo mwema, Imani, utu na uzalendo uliotukuka…Tuseme amin.

Namaliza kwa kipande cha shairi ya nyimbo iloimbwa hapa:

Related Posts