Kamera,ubao zabeba makipa Simba | Mwanaspoti

MASHABIKI wa Simba ghafla wamejikuta wakichanganyikiwa kwa mzuka wa furaha baada ya kuona kiwango cha timu hiyo katika mechi kadhaa iliizocheza hadi sasa zikiwamo mbili za Ligi Kuu Bara.

Kushinda mechi hizo mbili mfululizo za ligi na kukaa kileleni, huku ikiwa imefunga mabao saba na kutoruhusu bao lolote, kumewapa mzuka zaidi mashabiki na hasa ubora na viwango walivyo navyo makipa wa timu hiyo akiwamo Moussa Camara aliyesajiliwa dirisha lililopita.

Pia kurejea kwa Aishi Manula naye kathibitisha kwamba yeye ni bora, lakini nyuma ya viwango hivyo kuna siri nzito ya makipa hao.

Tuanze na Camara ambaye ndani ya mechi nne alizocheza zikiwemo mbili za Ngao ya Jamii na mbili za ligi amesimama imara langoni akiruhusu bao moja pekee alilofungwa na Yanga.

Wakati Simba ikichekelea kiwango hicho Manula naye akarejea kazini ambapo akatumia dakika 45 dhidi ya Al Hilal kuwafikishia mashabiki wa wekundu hao kuwa havumi, lakini yumo akionyesha kiwango bora.

Makipa hao wawili nje ya vipaji vyao kuna kocha mpya Msauzi Wayne Sandilands ambaye amekuja na mambo mazito kuwaboresha makipa wa timu hiyo.

Fuatilia mechi za Simba utaona Sandilands kabla ya mchezo kuanza na kila Simba ikibadilika kwenda goli lingine jamaa amekuja na kamera maalumu inayomsaidia kuchukua matukio yote ya makipa wa timu hiyo wanapokuwa langoni.

Kamera hiyo ya kisasa inayoitwa Go pro toleo 12 ambayo huwezi kuipata chini ya Sh1 milioni ikiwa mpya, inamsaidia kujua wapi makipa hao wanafanya vibaya lakini pia kujua ubora wao ambapo anaporudi mazoezini anakuwa na nafasi kuwafanyia marekebisho.

Video hizo zinakuwa na upana mkubwa ukimpa kocha nafasi ya kujua mambo mengi kupitia matukio yanayotokea uwanjani kwenye mechi husika

Kocha huyo amekuwa na darasa maalumu la kumrekebisha kila kipa anayepata nafasi ya kucheza mara mechi inapomaizika kupitia mikanda ya mechi inayotokana na kamera hiyo.

Sandilands pekee ndiye anayekwenda kuiweka na kuhamisha kamera hiyo kila kipindi kinapoanza na kumalizika, lakini uongozi wa Simba nao ukaongeza kitu.

Simba imewatega walinzi maalumu wawili wanaokaa pembeni ya kamera hiyo kwa mechi ambazo zinachezwa Uwanja wa KMC, Mwenge kutokana na nyuma ya goli kuwa karibu sana na sehemu ya kukaa mashabiki ambapo walinzi hao maarufu kwa jina la Steward wanahakikisha hakuna shabiki anayeweza kuisogelea.

Timu hiyo inapocheza Uwanja wa Benjamin Mkapa walinzi hao hawahitajiki kwa kuwa kamera hiyo inakuwa mbali na eneo la mashabiki.

Hajaishia hapo Sandilands ameshuka na kifaa kingine ambacho anakitumia anapowanoa makipa wake ambacho ni ubao mmoja mgumu mweupe wa plastiki.

Muangalie wakati Simba ikipasha misuli, kocha huyo atamwambia kipa mmoja akae pembeni mithili kama anapiga krosi au kona kisha atamtaka kupiga krosi kali za aina tofauti baadaye yeye mwenyewe anatumia ubao huo kupiga kama shuti au kichwa ambao unafanya mpira kuelekea langoni kwa nguvu.

Sandland aliwahi kuja na ubao huo hapa nchini wakati akiwa na kikosi cha Orlando Pirates ya huko Afrika Kusini akimnoa kipa wa timu hiyo wakati huo, Mghana Richard Offori ilipokuja kucheza na Simba.

Ubao huo umewapa ubora makipa wa Simba ambapo Camara kwenye mechi nne amekuwa na ufanisi mkubwa wa kucheza krosi akiwa hana bao aliloruhusu lililotokana na mipira ya aina hiyo.

Related Posts