KIUNGO mshambuliaji wa zamani wa Azam FC, anayekipiga kwa sasa MC Alger ya Algeria, Kipre Jr, amesema ili matajiri wa Chamazi waweze kuonyesha ushindani kimataifa wanahitaji miaka mitatu na zaidi kuingia kwenye mfumo.
Kipre aliyeitumikia kwa mafanikio Azam kwa misimu miwili kabla ya kuondoka hivi karibuni, aliliambia Mwanaspoti, timu hiyo inakua kila msimu hivyo uongozi huwa wana kitu unakitarajia kutoka kikosi hicho kutokana na namna wanavyofanya uwekezaji.
“Sijashangaa Azam kuondolewa mapema kimataifa nachofurahishwa nacho ni namna ambavyo timu inaendelea kuimarika na nguvu mpya zinazoongezwa kikosini naiona ikifanya vizuri msimu huu na kupata uwakilishi kimataifa,” alisema Kipre aliyefunga mabao tisa na kuasisti tisa msimu uliopita na kuongeza:
“Azam ina timu nzuri ambayo inatopa ushindani mkubwa kwa timu za ndani huku ikiendelea kujiimarisha zaidi kimataifa ipo siku wadau wa mpira wataizungumza kwa mafanikio makubwa ndani na kimataifa.”
Kipre Jr alisema amecheza misimu miwili Azam na mengi amejifunza na anatambua wachezaji wanavyopambana kusaka mafanikio hivyo anaamini ipo siku watakuwa bora.
“Viongozi wanawekeza nguvu kuhakikisha wanafanya usajili mkubwa ambao umekuwa kutoa matunda msimu hadi msimu nilipokuwa ndani ya timu hiyo mipango ilikuwa ni kutwaa mataji yote ya ndani lakini tulikwama sehemu ndogo na kujikuta tunamaliza nafasi ya pili Ligi Kuu na kucheza fainali Kombe la Shirikisho, hivyo naamini msimu huu pia watafanya vizuri,” alisema Kipre na kuongeza:
“Ongezeko la wachezaji ndani ya timu na mipango ya wachezaji wenye uzoefu wakiungana kwa pamoja wanaweza kuipambania timu hiyo na kufikia mafanikio, Azam ina wachezaji wengi bora na wenye uchu wa mafanikio hivyo kila kitu kinawezekana.”