Majaliwa akutana na bosi mteule wa WHO kanda ya Afrika

Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema Serikali itaendelea kujiimarisha kidiplomasia na itaongeza nguvu zaidi ili kuwawezesha Watanzania wengi kupata fursa mbalimbali katika jumuiya za kimataifa.

Amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, imefanikisha kuimarisha ushirikiano baina ya nchi washirika na sasa mafanikio yanaonekana.

Majaliwa amesema hayo leo Jumatano, Septemba 4, 2024 alipokutana na Mkurugenzi mteule wa Shirika la Afya Duniani (WHO) kanda ya Afrika, Dk Faustine Ndungulie, ofisini kwake Mlimwa jijini Dodoma.

“Rais wetu ameonyesha nia njema katika kipindi chake cha miaka mitatu na nusu, amefanya kazi kubwa ya kujenga diplomasia na mahusiano katika sekta mbalimbali na nchi nyingi duniani,” amesema.

Ameeleza jitihada hizo za Serikali zimeiwezesha Tanzania kuendelea kupaa kidiplomasia na kuiwezesha nchi kupata viongozi wakubwa ndani ya taasisi za kimataifa.

“Tunaamini kazi kubwa tulizozifanya katika kipindi hiki cha miaka mitatu ya kumpata Spika wa Umoja wa Mabunge duniani (IPU) haikuwa kazi ndogo na tena tumepata Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani kanda ya Afrika.”

Aidha, Majaliwa amesema Serikali itaendelea kumuunga mkono mkurugenzi huyo katika utekelezaji wa majukumu yake mapya.

“Wakati wote Waziri wa Afya atakuwa karibu nawe kuhakikisha sera zetu zinaenda sambamba na malengo ya WHO, kwa uwepo wako sisi lazima tuwe mstari wa mbele kuhakikisha tunakuunga mkono kwa mipango yetu ya afya ndani ya nchi.”

Mkurugenzi mteule wa WHO Afrika, Dk Faustine Ndungulile amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kumuunga mkono na kufanya ushawishi wa kidiplomasia ili kufanikisha ushindi huo.

“Kwa upekee sana ninamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake kubwa katika kufanikisha ushindi huu, kwa ushawishi wake kwenye jumuiya za kimataifa pia nawashukuru viongozi wengine wa Serikali, Bunge na wadau wote,” amesema Dk Ndugulile.

Dk Ndugulile ambaye pia ni Mbunge wa Kigamboni, Dar es Salaam alichaguliwa katika mkutano wa 74 wa Kamati ya Kanda ya Afrika ya WHO, uliofanyika Brazzaville, Jamhuri ya Kongo Agosti 27, 2024.

Jina la Dk Ndugulile litawasilishwa kwa uteuzi na kikao cha 156 cha Bodi ya Utendaji ya WHO, ambacho kitafanyika Februari 2025, Geneva, Uswisi na likithibitishwa anatarajia kuanza kazi mwishoni mwa Februari ama mwanzoni mwa Machi 2025.

Related Posts