Mbunge ataka wanaobaka watoto waondolewe uume

Dodoma. Hoja ya adhabu kwa wanaobaka watoto chini ya miaka 10, imeibuka bungeni mmoja wa wabunge akitaka wanaotiwa hatia wanyongwe hadi kufa, huku mwingine akitaka waondolewe uume.

Wabunge hao wa viti maalumu, Rita Kabati na Najma Murtaz Giga, wamesema hayo leo Jumatano Septemba 4, 2024 wakati wa kipindi cha maswali na majibu bungeni jijini Dodoma.

Katika swali la msingi, Najma amehoji iwapo Serikali haioni haja ya kuleta muswada wa sheria itakayotoa adhabu ya kifo kwa wabakaji wa watoto chini ya miaka tisa.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Jumanne Sajini amesema kifungu cha 131(1) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 imeainisha adhabu ya makosa ya kubaka kuwa ni kifungo kisichopungua miaka 30, viboko na Mahakama inaweza kutoa amri ya kumlipa fidia muathirika wa tukio.

Amesema kifungu 131(3) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu kimeainisha ikiwa muathiriki wa tukio ni mtoto mwenye umri chini ya miaka 10 adhabu pekee iliyokuwapo ni kifungo cha maisha jela.

Amesema adhabu ya kifungo cha maisha kwa mujibu wa sheria za nchi ni muda wote wa uhai wa mkosaji ambayo ni adhabu ya pili kwa ukubwa ukiacha adhabu ya kifo inayotolewa kwa makosa ya uhaini na kuua kwa kukusudia.

Hata hivyo, Sajini amesema Serikali inalichukua swali la mbunge huyo kama sehemu ya maeneo ya kufanyiwa kazi na kuona kama ipo haja ya kuongeza adhabu kwa wanaobaka watoto chini ya miaka 10 au waendelee na adhabu iliyopo ya kifungo cha maisha jela.

Mbunge Kabati amesema ubakaji umeshika kasi hasa katika Mkoa wa Iringa ambako imetokea kwa vijana walio chini ya umri wa miaka 18, kubakana wenyewe kwa wenyewe.

“Je sheria inasemaje kwa vijana wanaobakana wenyewe kwa wenyewe kwenye shule huko? Lakini pia hili tatizo limekuwa ni kubwa sana hapa nchini na tumeona hadi wauawe?” amehoji.

Amesema yeye anaona wanaokutwa na hatia kwa makosa hayo watolewe uume maana ndiyo umekuwa tatizo kubwa.

Sajini amesema kutokana na mmomonyoko wa maadili, baadhi ya matukio ambayo hayakuzoeleka kusikika awali, yameongezeka kwa kasi ikiwamo ubakaji.

“Na sasa amesema kwa watoto ipo mashuleni, kosa hata kama limefanywa na mtoto ni kosa lakini kwa maana sheria zetu mtoto atahukumiwa kwa mujibu wa sheria za watoto,” amesema.

Amesema ikitokea mtoto amemfanyia mwenziwe vitendo vya uvunjifu wa maadili kama hivyo na taarifa zikitolewa katika vyombo vya dola, kisha kupelekwa mahakamani mtoto atahukumiwa kwa mujibu wa sheria.

Amesema ikiwa kama atahukumiwa kifungo basi atafungwa katika Mahakama za watoto.

Kuhusu kuondolewa uume, Sajini amesema ni kweli jambo hilo linaudhi lakini hicho anachokisema hakipo katika sheria za nchi.

“Kama tutafika hatua hiyo ni pale ambapo Bunge litakuwa limebadilisha sheria na kuruhusu alichosema mbunge,” amesema.

Related Posts