Mirerani. Mamia ya wakazi wa mji mdogo wa Mirerani, wilayani Simanjiro mkoani Manyara wamejitokeza kumzika mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Endasak, wilayani Hanang’, Lidya Saitoti, aliyefariki dunia pamoja na wenzake wawili na dereva wa basi dogo walilokuwa wakisafiria kutoka Endasak kwenda jijini Arusha.
Ajali hiyo ilitokea Agosti 31, 2024, eneo la Gajal, wilayani Babati, basi dogo aina ya Toyota Coaster lililobeba wanafunzi 33, mwalimu mmoja, kondakta na dereva liligongana na lori aina ya Scania na kusababisha vifo vya watu wanne.
Waliofariki dunia ni wanafunzi watatu akiwamo Lidya Saitoti, Samira Halidi na Aisha Rahim pamoja na dereva Ally Ramadhan huku wanafunzi 30 wakijeruhiwa katika ajali hiyo.
Akizungumza kwenye ibada ya maziko leo Jumatano Septemba 4, 2024, Askofu wa Kanisa la Pentekote, Sommy Severua amesisitiza umuhimu wa wanadamu kumgeukia Mungu ili kujiandaa na mwisho mwema.
“Tunashiriki kwenye mazishi ya binti huyu ambaye ametwaliwa ghafla, hivyo mimi na wewe tunapaswa kujiandaa na safari kwa kuwa na mwisho mwema,” amesema.
Mkuu wa Shule ya Endasak, Rogate Munisi amesema wanafunzi na walimu walijiandaa kwa sala na maombi kabla ya safari, ikiwamo kuandika orodha ya majina ya wazazi na namba za simu ili kuwasiliana pindi watakapofika Arusha.
“Wanafunzi walijiandaa kiroho kwa sala na maombina kutokana na hofu ya wizi wa watoto, tulikuwa na orodha ya namba za simu ili wazazi na walezi waweze kuwasiliana na watoto wao pindi wakifika Arusha,” amesema Munisi.
Amesema basi hilo lilikuwa na jumla ya abiria 36, wakiwamo wanafunzi 33, mwalimu mmoja, dereva mmoja na kondakta mmoja.
Kati ya wanafunzi 30 waliojeruhiwa na kupelekwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara, 16 waliruhusiwa kurudi nyumbani, 11 walipewa rufaa na watatu walibaki hospitalini.
Munisi amesema wakati Lidya akizikwa leo Jumatano, mazishi ya Samira yatakuwa Kata ya Terrat jijini Arusha na Aisha atazikwa eneo la Minjingu, wilayani Babati.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Andrew Method amesema majeruhi watatu waliokuwa wamelazwa Hospitali ya Rufaa ya mkoa huo kwa matibabu wamesharuhusiwa.
Amesema mwanafunzi Yusta Masawe amepewa rufaa kwenda Hospitali ya Kanda ya KCMC mjini Moshi na majeruhi wengine, Careen Peter Moshi na Eliwini Martin, wameruhusiwa pia.
Kwa upande wake, Abubakari Saidi, baba mzazi wa Sabrina aliyejeruhiwa, amesema mtoto wake amelazwa Hospitali ya KCMC mjini Moshi.
Massawe amesema Sabrina amevunjika miguu yote miwili na usoni alikatwa na kioo na kushonwa, lakini anaendelea vyema baada ya kupatiwa matibabu.
“Tunamshukuru Mungu, Sabrina anaendelea vyema na matibabu akiwa na mama yake hospitalini. Tunamshukuru Mungu kwa yote yaliyotokea,” amesema Massawe.