NGO’s zatakiwa kuhamasisha wananchi kushiriki uchaguzi

Geita. Wakati Watanzania wakitarajia kushiriki kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa Novemba 27, 2024 kwa kupiga kura na Uchaguzi Mkuu 2025, mashirika yasiyo ya kiserikali (NGO’s) mkoani Geita yametakiwa kutoa elimu kwa jamii juu ya umuhimu wa wananchi kupiga kura.

Pia, mashirika hayo yametakiwa kutoa elimu kwa jamii juu ya umuhimu wa kumchagua kiongozi mwenye uwezo wa kusimamia na kutekeleza majukumu kwa maslahi ya jamii na sio kwa maslahi yake binafsi.

Hayo yamesemwa na Katibu Tawala Msaidizi Mkoa wa Geita, Charles Chacha anayeshughulikia biashara na viwanda wakati wa mkutano mkuu wa mashirika hayo mkoani Geita, ukiwa na kauli mbiu; ‘Mashirika yasiyo ya kiserikali ni wadau muhimu washirikishwe kuimarisha utawala bora’.

Chacha amesema mashirika yasiyo ya kiserikali yana nafasi kubwa ya kuhamasisha jamii kushiriki kwenye uchaguzi, ili kupata viongozi watakaozingatia maadili na taratibu za nchi, lakini wakiweka maslahi ya jamii mbele.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti baaadhi ya wakurugenzi wa mashirika hayo yasiyo ya kiserikali wamesema kazi yao ni kuhamasisha jamii katika mambo mbalimbali ikiwemo haki ya uraia pamoja na suala la uandikishaji wa daftari la kudumu la wapiga kura sambamba na kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali.

Mkurugenzi wa Shirika lisilo la Kiserikali la Brightlight Organization, Mathew Daniel anasema wamelenga kuyafikia makundi ya pembezoni ambayo mara nyingi husahaulika, hususan vijana waliopo shuleni ambao wamefikia umri wa kupiga kura.

Amesema vijana wengi kutokana na wao kutoshirikishwa, huamini suala la kupiga kura linawahusu wanasiasa na kusahahu kuwa katika mchakato wa kura ndiko wanakopatikana viongozi watakaotunga sera kwa ajili ya maendeleo ya Taifa.

“Tunawaeleza vijana kuwa kura ni kwa ajili ya maendeleo ya nchi, unapokaa pembeni na kuacha watu wakuchagulie kiongozi ndivyo unavyopoteza haki yako ya msingi ya kumchagua kiongozi atakayeleta maendeleo na mwisho wa siku ndio hao wanaolalamika kuwa viongozi hawafanyi kazi wanasahau kuwa wao hawakupiga kura,” amesema Daniel.

Amesema wajibu wa NGO’s ni kuhakikisha wanatoa elimu kwa jamii kuchagua kiongozi mwenye uzalendo, ueledi atakaesimamia misingi ya waasisi wa Taifa akiangalia maslahi mapana ya ya nchi.

Amesema kama NGO’s wanafanya uchechemuzi wa kuwataka watu wakaboreshe taarifa kwenye daftari la kudumu na kwa wale ambao hawajajiandikisha wakajiandikishe, ili waweze kuchagua kiongozi wanayemtaka.

Hata hivyo, ili kuwafikia vijana zaidi ambao ndio wengi nchini ameishauri Tume Huru ya Uchaguzi (INEC) ,wadau wa maendeleo na Mashirika yasiyo ya kiserikali kuandaa vipindi maalumu vya umuhimu wa upigaji kura na kuviweka kwenye mitandao ya kijamii, ili waweze kuwafikia vijana kwa wingi zaiid.

“Ili tuwanase vijana ambao wapo kidijitali zaidi, hatuna budi kuwafuata wanakopatikana, maana hawa ukiwaita kwenye mikutano hawashiriki, lakini kama tutaandaa vipindi na kuviweka mtandaoni watasoma na kusikiliza na kujua thamani ya kura zao katika kufanya mabadiliko,” amesema Daniel.

Naye Ayoub Bwanamad kutoka shirika lisilo la kiserikali la marafiki wa elimu kutoka Mkoa wa Geita, amesema asasi za kiraia katika Mkoa wa Geita wamejipanga kuhamasisha jamii kuelekea kwenye uchaguzi wa serikali za mtaa na Uchaguzi Mkuu 2025, lengo likiwa kuwapata viongozi bora.

“Asasi za kiraia tumejipanga kutoa elimu kwa ajili ya kuhamasisha jamii kuelekea kwenye uchaguzi, tayari tumetoa elimu watu wakajiandikishe kwenye daftari la kudumu la wapiga kura, tuwaeleze jamii pia ijue kuna maisha baada ya uchaguzi, ili waendelee kushikamana kwa kuwa baada ya uchaguzi watu wataendelea kuwa familia na kuishi kwa umoja,” amesema.

Amesema changamoto kubwa bado iko kwa kundi la vijana ambalo mara zote huharibiwa na wanasiasa na sasa wanawahamasisha wajitokeze kugombea na wale ambao hawagombei, watumie haki yao kuchagua kiongozi wanayemtaka badala ya kulalamika.

“Tunawahamasisha vijana wajiandikishe kwenye daftari la kudumu la wapigakura na wapige kura, wasikubali kutumiwa na wanasiasa kwa maslahi yao binafsi, waangalie masuala mapana ya nchi,” amesema Bwanamadi.

 Sophia Njete kutoka Shirika la Nelico lililopo mkoani Geita, amesema wanaendelea kuhamasisha jamii kuitumia demokrasia vema kwa kumchagua kiongozi wanayemtaka.

“Tunahamasisha watu kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura na wale wenye vitambulisho waende kuboreshe taarifa zao, ili wamchague kiongozi wanayemtaka,” amesema.

“Vijana wengi huamini wazee ndio wanaopaswa kupiga kura na wao haiwahusu, lakini sisi tumekuwa tukiwaelimisha na kuhamasisha jamii kutambua kuwa kura yao moja ina thamani kubwa ya kuleta mabadiliko, hivyo wasikubali kubaki nyuma,” amesema.

Jenipha Joseph kutoka shirika la Shdepha+, amesema kwenye utekelezaji wa miradi huhamasisha jamii kujitokeza kupiga kura, ili kuchagua kiongozi wanayemtaka.

Mwenyekiti wa mashirika yasiyo ya kiserikali Mkoa wa Geita, Paulina Alex amesema ili NGO’s itoe elimu kwa mpiga kura, inatakiwa kuomba kibali kutoka INEC na tayari amehamasisha waombe na baadhi wamefanikiwa.

Nini kimefanywa kukuza ushiriki

Serikali imechukua hatua kadhaa za kuimarisha ushiriki wa makundi maalumu katika siasa na uongozi.

Hatua hizo ni pamoja na kutenga nafasi maalumu kwa ajili ya wanawake na vijana katika mabaraza ya uongozi, hatua ambayo imechangia kuongeza idadi ya wanawake na vijana katika uongozi wa serikali za mitaa.

Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), katika uchaguzi wa serikali za mitaa 2019, asilimia 33 ya wagombea walikuwa wanawake, huku asilimia 37 walikuwa vijana.

Hata hivyo, bado kuna haja ya kuongeza juhudi zaidi ili kuhakikisha makundi yote maalumu yanapata nafasi sawa katika uongozi.

Hii ni pamoja na kuanzisha programu za elimu ya uraia zinazolenga kuelimisha makundi maalumu kuhusu umuhimu wa kushiriki katika uongozi na haki zao za kisiasa.

Vilevile, Serikali na wadau mbalimbali wanapaswa kutoa msaada wa kifedha na kiufundi kwa makundi hayo, ili kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika mchakato wa uchaguzi.

Kwa maana nyingine, asasi za kiraia zinapaswa kuhakikisha zinashiriki katika uchaguzi wa serikali za mitaa kwa kutoa elimu zaidi kwa wananchi ili waelewe kuna kuchagua na kuchaguliwa.

Ushiriki wa asasi hizi katika uchaguzi wa serikali za mitaa ni muhimu kwa maendeleo endelevu ya Taifa.

Kwa kupata nafasi ya kutoa elimu, zitakuwa zinajenga uelewa na uaminifu kwa jamii kwamba zipo kwa masilahi ya kila kundi.

Hivyo, utoaji elimu kuelekea uchaguzi ni jukumu la serikali, vyama vya siasa, asasi za kiraia hadi jamii kwa ujumla, kuhakikisha kila mtu mwenye sifa anapata fursa ya kushiriki kikamilifu katika uchaguzi wa serikali za mitaa.

Hii itawezesha kujenga Tanzania yenye usawa, haki na maendeleo kwa wote.

Related Posts