Papa ahimiza kujikinga na misimamo mikali – DW – 04.09.2024

Papa amesema jambo hilo linapotosha imani za kidini za watu kupitia kile alichokitaja kama “udanganyifu na vurugu”. 

Akizungumza katika hotuba yake mbele ya wanasiasa 300 na viongozi wa kidini katika Ikulu ya Merdeka mjini Jakarta, Papa Francis amesema Kanisa Katoliki litaongeza juhudi katika mazungumzo baina ya dini kwa matumaini ya kusaidia kukomesha itikadi kali.

Soma pia: Papa Francis awasili Indonesia

“Ili kukuza maelewano ya amani na matunda ambayo yanahakikisha amani na kuondoa kukosekana kwa usawa na mateso ambayo bado yanaendelea katika baadhi ya maeneo ya nchi, Kanisa Katoliki linataka kuongeza mazungumzo kati ya dini.”

“Kwa njia hii, ubaguzi unaweza kuondolewa, na hali ya kuheshimiana na kuaminiana inaweza kukua. Hili ni la lazima ili kukabiliana na changamoto zinazofanana, ikiwa ni pamoja na kukabiliana na misimamo mikali na kutovumiliana, ambayo kupitia upotoshaji wa dini hujaribu kulazimisha maoni yao kwa kutumia udanganyifu na vurugu.”

Indonesia ina idadi ya watu wapatao milioni 280 na inakadiriwa kuwa asilimia 87 ni Waislamu na uhuru wa kuabudu umehakikishwa katika katiba ya nchi.

Ghasia za itikadi kali

Indonesia | Papa Francis
Papa ahimiza kujikinga dhidi ya misimamo mikali ya kidini katika ziara yake nchini Indonesia.Picha: INDONESIA PAPAL VISIT COMMITTEE

Hata hivyo, taifa hilo limekuwa na matukio kadhaa ya ghasia za itikadi kali katika miaka ya hivi karibuni, ikiwa ni pamoja na mashambulizi ya mabomu ya kujitoa muhanga mwaka 2021 na 2022 kutoka kwa kundi lenye mafungamano na kundi linalojiita Dola la Kiislam la Jamaah Ansharut Daulah (JAD).

Katika hotuba ya kumkaribisha papa nchini Indonesia, Rais Joko Widodo amesema Indonesia inathamini mtazamo wa Vatikani ambao unaendelea kutoa sauti na wito wa amani na juhudi za kutaka kusitishwa mapigano katika vita vya Israel na Gaza.

“Vita havitamnufaisha mtu, vita vitaleta mateso na taabu kwa watu wa kawaida tu. Kwa hiyo, tusherehekee tofauti tulizo nazo. Tukubaliane na tuimarishe uvumilivu ili kutambua amani. Kutambua ulimwengu bora kwa wanaadamu wote.”

Soma pia: Indonesia yaweza kutuma vikosi vyake Gaza iwapo itahitajika

Baadaye leo, Papa Francis anatarajiwa kukutana na Maaskofu wa Kikatoliki wa Indonesia katika Kanisa Kuu la Jakarta. Siku ya Alhamisi, atashiriki katika mkutano wa dini mbalimbali katika Msikiti wa Istiqlal, msikiti mkubwa zaidi katika Asia ya Kusini-Mashariki. Katika ziara hii ya siku 12 PapaFrancis anatarajiwa kuzitembelea Papua New Guinea, Timor ya Mashariki na Singapore.

 

//Reuters, AFP

Related Posts