Polisi laeleza uchunguzi tuhuma za mauaji dhidi ya mganga wa kienyeji 

Dar es Salaam. Msemaji wa Jeshi la Polisi, David Misime amesema mganga wa kienyeji, Nkamba Kasubi anayetuhumiwa kwa mauaji ya watu 10 anatarajiwa kufikishwa mahakamani muda wowote kuanzia sasa.

Mganga huyo alikamatwa Agosti 26, 2024 akidaiwa kutenda makosa hayo katika mikoa ya Singida na Dodoma.

Kasubi anashikiliwa pamoja na watuhumiwa wengine saba.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumatano Septemba 4, 2024 amesema uchunguzi umekamilika na muda wowote wanatarajia kumfikisha mahakamani kusomewa mashitaka yanayomkabili.

“Mganga wa kienyeji atafikishwa mahakamani wakati wowote kuanzia sasa kujibu tuhuma zinazomkabili,” amesema.

Wakati huohuo, Jeshi la Polisi linaendelea kuwashikilia watu watatu, akiwamo mganga wa kienyeji Mtila Ausi, maarufu Shehe Mtila, mkazi wa wilayani Tunduru akituhumiwa kwa mauaji ya wafanyabiashara wawili wa Songea, mkoani Ruvuma.

Watuhumiwa wengine ni Omary Abdallah na Amini Sanga wanaodaiwa kuwanyeshwa dawa ya maji iliyowalegeza wafanyabiashara waliokwenda kwa mganga huyo kupata dawa za kuwezesha biashara zao kufanya vizuri zaidi.

Taarifa iliyotolewa na Misime imesema wafanyabiashara waliouawa ni Raymond Hyera, maarufu Ray (25), mkazi wa Msamala, Manispaa ya Songea na Riziki Mohamed (30), mkazi wa Mjimwema, Songea.

Misime amesema taarifa za kupotea kwa wafanyabiashara hao walipokea Agosti 3, baada ya ndugu wa wafanyabiashara hao kwenda kuripoti Kituo cha Polisi Songea kuhusu kupotea kwao tangu Julai 31, 2024.

“Jeshi la Polisi linaendelea kuwashikilia Shehe Mtila (mganga wa kienyeji), Omary Abdallah na Amini Sanga (huyu ndiye aliyeonekana na hawa wafanyabiashara wawili mara ya mwisho)” amesema.

Misime amesema taarifa za uchunguzi wa awali baada ya ufuatiliaji zilibaini wafanyabiashara hao mara ya mwisho walionekana na mfanyabiashara mwenzao Amini Sanga (26), ambaye alitafutwa lakini hakupatikana kwa wakati huo.

“Askari Polisi wataalamu wa kufuatilia matukio makubwa, waliweza kupata taarifa kuwa wafanyabiashara hao walielekea kwa mganga wa kienyeji Shehe Mtila huko wilayani Tunduru,” amesema. 

Amesema polisi walipofika nyumbani kwa mganga huyo hawakumkuta, walijulishwa aliondoka na baba yake mdogo, Omary Abdallah.   

“Katika ufuatiliaji ilibainika walipoondoka walielekea Mbinga kwa mganga mwingine lakini askari walipofika huko, hawakuwakuta,” amesema.

Amesema taarifa walizopata zilifanikisha kumkamata Shehe Ausi na Omary Abdallah wakiwa jijini Dodoma ndani ya chumba walichopanga, eneo la Makole.

“Baada ya mahojiano, walikiri wafanyabiashara hao kufika nyumbani kwao wakiambatana na mfanyabiashara mwenzao Amini Sanga kwa lengo la kupata dawa za kuwawezesha biashara zao kufanya vizuri zaidi.

“Kilichofanyika, waliwanywesha wafanyabiashara hao wawili maji ambayo yaliwafanya walegee na kusababisha kupoteza maisha,” amesema.

Taarifa hiyo imesema baada ya wafanyabiashara hao kufariki dunia, waliwachukua na kwenda kuwazika katika pori la Mdinguli, Kijiji cha Mtangashari wilayani Tunduru.

Amesema pia walichukua fedha walizokuwa nazo wafanyabiashara hao Sh20 milioni na kugawana.

“Septemba 3, 2024, Mtila Ausi na Omary Abdallah waliwaongoza askari Polisi hadi walipowazika wafanyabiashara hao wawili. Ufukuaji ulifanyika na miili yao ilikutwa. Uchunguzi unaendelea kukamilishwa ukiwamo wa kisayansi ili taratibu nyingine zifuate,” amesema.

Related Posts