WAKATI vyama vya kikapu nchini vikiandaa uzinduzi kwa kushindanisha timu viwanjani moja kwa moja, Mkoa wa Pwani umeanza kwa wachezaji kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo Kaole wilayani Bagamoyo.
Katibu wa Chama cha Kikapu mkoani humo, Abdalah Mpongole amesema baada ya kutembelea vivutio hivyo wachezaji walishiriki katika bonaza lililofanyika katika Uwanja wa Sekondari ya Bagamoyo.
“Katika bonaza tulilofanya wanafunzi walijitokeza pia kujifunza kuhusu mchezo wa mpira wa kikapu,” alisema Mpogole.
Alizitaja timu zizoshiriki katika bonanza hilo kuwa ni Kibaha Centipedes, Tumbi Survivors, Termites Kings, Bagamoyo Sanaa Ballers na Kibiti Warriors.
Akizungumzia ligi, alisema imepangwa kuanza mwezi huu.
Hata hivyo, Mpogole alisema tarehe ya kuanza itatajwa baada ya kamati ya mashindano kukutana hivi karibuni.
Alizitaja timu zilizothibitisha kushiriki kuwa ni Kibaha Centipedes, Tumbi Survivors, Kibiti Warriors na Termites Kings, huku zingine zikiwa ni Bagamoyo Sanaa ilhali upande wa wanawake ni Termites Queens na Kibaha Centipedes.