Hii ni ziara ya kwanza ya Rais Abdel Fattah el-Sissi nchini Uturuki tangu alipochaguliwa kuwa rais mwaka 2014. Vyombo vya habari vya Misri vimesema anaambatana na ujumbe mkubwa wa maafisa na wafanyabiashara.
El-Sissi anatarajiwa kufanya mazungumzo na mwenyeji wake, Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan kuangazia masuala kuanzia uhusiano baina ya mataifa yao, mzozo katika Ukanda wa Gaza hadi kusambaa kwa hali ya wasiwasi katika eneo zima la Mashariki ya Kati miongoni mwa mengineyo.
Wanatarajiwa pia kushuhudia utilianaji saini wa mikataba kadhaa ya ushirikiano unaolenga kuimarisha uhusiano baina ya mataifa hayo, katika maeneo ya nishati, ulinzi na utalii.
Mwezi Februari, Rais Erdogan alifanya ziara yake ya kwanza nchini Misri, baada ya kama muongo mmoja tangu mataifa hayo yalipokubaliana kurekebisha uhusiano na kuteua tena mabalozi. Erdogan alisema mataifa hayo yanataka kuimarisha uhusiano wa kibiashara utakaofikia dola bilioni 15 kutoka bilioni 10 za sasa.
Uhusiano kati ya Misri na Uturuki ulivurugika baada ya jeshi la Misri kumuondoa madarakani aliyekuwa Rais Mohammed Morsi katikati ya maandamano makubwa kabisa ya kumpinga, baada ya kutawala kwa mwaka mmoja tu.
Ikumbukwe Morsi alitokea kundi la Udugu wa Kiislamu ambalo lilipigwa marufuku nchini Misri na limeorodhesha kama kundi la kigaidi. Lakini Uturuki ni muungaji mkono mkubwa na wa muda mrefu wa kundi hilo.
Soma pia:Al sisi apitisha sheria ya kupambana na Ugaidi
Katika kurejesha hali ya maelewano, hivi karibuni, Ankara imejizuia kuikosoa serikali ya El-Sissi, ikilenga sio tu kuondoa doa lililopo la kimahusiano na taifa hilo, bali pia na mataifa mengine ya Kiarabu, huku pia ikiangazia uwekezaji kwenye mataifa hayo, katikati ya anguko la kiuchumi nchini humo.
Novemba, 2022, Erdogan na El-Sissi walipigwa picha wakipeana mikono katika michuano ya soka ya Kombe la Dunia huko Qatar.
Kisha, Waziri wa Mambo ya Nje wa Misri Sameh Shoukry alikwenda Uturuki mwaka 2023 kwa lengo la kuonyesha mshikamano na taifa hilo wakati tetemeko kubwa kabisa la ardhi lilipopiga kusini mwa Uturuki na Syria.