Ripoti wafanyabiashara soko la Kariakoo yatua kwa RC Chalamila

Dar es Salaam. Baada ya kazi ya takriban miezi miwili, hatimaye kamati iliyoundwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam (RC), Albert Chalamila kupitia orodha ya wafanyabiashara wanaopaswa kurudishwa katika Soko la Kariakoo, imekabidhi ripoti yake.

Kamati hiyo iliundwa na Chalamila katikati ya Julai 2024, baada ya malalamiko ya baadhi ya wafanyabiashara waliodai majina yao hayakujumuishwa katika orodha ya wanaopaswa kurudishwa katika soko hilo.

Wafanyabiashara hao ni kati ya wale 1,662 waliokumbwa na janga la moto katika soko hilo, lililotokea Julai mwaka 2022 na kwa mujibu wao, Shirika la soko hilo liliorodhesha idadi ya watu 891 pekee kuwa ndiyo wanaostahili kurudi sokoni humo.

Hatua hiyo ilisababisha maandamano ya wafanyabiashara hao hadi zilipo Ofisi Ndogo za Makao Makuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dar es Salaam na baadaye kwa Chalamila aliyeamua kuunda kamati hiyo.

Kamati imekabidhi ripoti hiyo jijini Dar es Salaam leo Jumatano, Septemba 4, 2024 kwa Chalamila katika ukumbi wa mikutano wa Arnatoglo.

Akipokea ripoti hiyo, Chalamila amesema alilazimika kuunda kamati hiyo ili kujiridhisha juu ya mchakato uliotumika kupata orodha ya majina ya awali ya wafanyabiashara hao.

Hatua hiyo, imechochewa na kile alichoeleza, unyeti wa eneo la soko la Kariakoo kwa masilahi ya Jiji la Dar es Salaam na Taifa kwa ujumla.

Sambamba na kupokea ripoti hiyo, Chalamila alipokea maoni kutoka kwa wajumbe wa kamati hiyo, ili kuwa na uelewa wa pamoja.

Related Posts