SERIKALI: THAMANI YA DHAMANA ZA MIKOPO ZISIZIDI MARA MBILI YA MKOPO

Na. Saidina Msangi, Kisarawe, Pwani.

Wananchi wa Kitongoji cha Homboza Wilayani Kisarawe, mkoani Pwani, wametakiwa kuhakikisha kuwa wanachukua mikopo katika taasisi za watoa huduma za fedha waliosajiliwa kisheria huku wakihakikisha kuwa thamani ya dhamana za mikopo wanazoweka zisizidi mara mbili ya mkopo wanaopewa.

Wito huo umetolewa na Timu ya Wataalamu kutoka Wizara ya Fedha waliofika katika kitongoji hicho kutoa elimu ya fedha kwa wananchi ili kuwawezesha kuepukana na mikopo umiza pamoja na kuwa na usimamizi mzuri wa fedha binafsi.

Akizungumza wakati akitoa elimu kwa wananchi wa kitongoji hicho cha Homboza, Afisa Usimamizi wa Fedha kutoka Wizara ya Fedha, Bw. Stanley Kibakaya, alisema kuwa suala la dhamana limekuwa likiwatatiza wananchi pale wanapotaifishiwa dhamana zao kwa kushindwa kurejesha mikopo kwa wakati.

‘‘Ni muhimu sana kufahamu kuwa dhamana ya mikopo haitakiwi kuzidi mara mbili ya mkopo unaochukua lakini pia hakikisha unapochukua mkopo mwenza wako awe na taarifa kwa sababu inasaidia kuwa na uwajibikaji wa pamoja na kuepusha migogoro ya familia,’’alisisitiza Bw. Kibakaya.

Aidha, aliwasisitiza kujiridhisha na riba za mikopo kabla ya kuchukua ili kuwa na uhakika kama inalingana na kiwango kilichowekwa na Benki Kuu ya Tanzania ambacho hakitakiwi kuzidi asilimia 3.5.

Naye Afisa Masoko na Uhusiano Mwandamizi wa Mfuko wa Uwekezaji wa UTT AMIS, Bw. Rahim Mwanga, akitoa elimu kwa wananchi hao alisisitiza kuwa ni muhimu kuzingatia matumizi sahihi wanapopata fedha ikiwemo kujiwekea akiba.

‘‘Lazima tupunguze matumizi yasiyo ya lazima ili kupata akiba ya kutunza ni muhimu kuzingatia matumizi kwa kutenganisha matumizi ya lazima na yale yasiyo ya lazima matumizi ya kwanza yawe akiba na kuhakikisha kuwa akiba hiyo unaiwekeza ili kutunza thamani yake,’’alifafanua Bw. Mwanga.

Alitoa rai kwa wananchi hao kutumia fursa ya uwekezaji wa pamoja kupitia Taasisi ya UTT Amis yenye mifuko mbalimbali kulingana na mahitaji ya uwekezaji ambapo mfuko huo una dhamana ya kuwekeza fedha hizo kwa pamoja na kuwezesha kila mwekezaji kupata faida kulingana na uwekezaji wake.

Kwa upande wake, Afisa Mtendaji wa Kitongoji cha Homboza, Bi. Maida Lugoya, aliishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kutoa elimu ya fedha kwa wananchi na kueleza kuwa elimu hiyo italeta matokeo mazuri na kuwarahisishia kazi kama watendaji kulingana na changamoto hasa ya watoa huduma za fedha ambao hawajasajiliwa.

Aliongeza kuwa elimu hiyo itawasaidia wananchi wa Kitongoji hicho katika shughuli zao za kiuchumi ili kuwawezesha kuepukana na changamoto ya mikopo umiza kutoka kwa taasisi za watoa huduma za fedha ambao hawajasajiliwa.

Aidha, alitoa wito kwa watoa huduma za fedha katika kitongoji hicho kuhakikisha kuwa wamesajiliwa kisheria na kuwa uongozi hautasita kumchukulia hatua yeyote atakayebainika kuendesha shughuli bila kuwa na leseni.

Timu ya Wataalamu kutoka Wizara ya Fedha ipo mkoa wa Pwani ambapo inazunguka katika wilaya za mkoa huo kutoa elimu ya fedha kwa wananchi ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango Mkuu wa Serikali wa kuhakikisha kuwa wananchi wanapata elimu ya fedha.
Afisa Usimamizi wa Fedha kutoka Wizara ya Fedha, Bw. Stanley Kibakaya, akitoa elimu ya fedha kwa wananchi wa Kitongoji cha Homboza, wilayani Kisarawe, mkoani Pwani, wakati Timu ya Maafisa kutoka Wizara ya Fedha ilipofika katika katika kitongoji hicho kutoa elimu ya fedha kwa wananchi.
Afisa Mtendaji wa Kitongoji cha Homboza wilayani Kisarawe mkoani Pwani, Bi. Maida Lugoya, akizungumza na wananchi wakati Timu ya Maafisa kutoka Wizara ya Fedha ilipofika katika kitongoji hicho kutoa elimu ya fedha kwa wananchi ili kuwawezesha kufahamu namna bora ya kutunza fedha pamoja na kujiepusha na mikopo umiza.

Afisa Masoko na Uhusiano Mwandamizi wa Mfuko wa Uwekezaji wa UTT AMIS, Bw. Rahim Mwanga, akiwaelekeza wananchi wa Kitongoji cha Homboza wilayani Kisarawe mkoani Pwani, jinsi ya kufungua akaunti za uwekezaji katika mfuko wa uwekezaji wa UTT Amis, baada ya mafunzo ya elimu ya fedha iliyotolewa na Timu ya Maafisa kutoka Wizara ya Fedha katika kitongoji hicho.

Baadhi ya wananchi wa Kitongoji cha Homboza, wilayani Kisarawe, mkoani Pwani, wakifuatilia mada zilizokuwa zikiwasilishwa na Maafisa kutoka Wizara ya Fedha waliowasili kutoa elimu ya fedha kwa wananchi wilayani humo.

Mmoja wa wananchi waliohudhuria mafunzo ya elimu ya fedha yanayotolewa na Wizara ya Fedha, Bi. Asia Mbegu, akiuliza swali baada ya kupata elimu ya fedha iliyotolewa na Timu ya maafisa kutoka Wizara ya Fedha waliofika kutoa elimu ya fedha kwa wananchi, katika kitongoji cha Homboza, wilayani Kisarawe mkoani Pwani.


Timu ya Maafisa kutoka Wizara ya Fedha (wenye sare ya fulana) wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wananchi waliohudhuria mafunzo ya elimu ya fedha iliyotolewa na timu hiyo katika kitongoji cha Homboza, wilayani Kisarawe mkoani Pwani.(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Kisarawe -Pwani)

Related Posts