Shahidi wa 12 kesi ya ‘waliotumwa na afande’ akamilisha ushahidi

Dodoma. Shahidi wa 12 wa upande wa Jamhuri katika kesi ya kubaka kwa kikundi na kumwingilia kinyume cha maumbile binti mkazi wa Yombo Dovya, jijini Dar es Salaam amekamilisha ushahidi.

Shahidi huyo amekamilisha ushahidi leo Septemba 4, 2024 akitumia zaidi ya saa sita. Kesi hiyo iko mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Zabibu Mpangule.

Shahidi huyo ambaye ni mtambuzi kutoka idara ya utambuzi alianza kutoa ushahidi jana Septemba 3 lakini haukukamilika.

Kesi hiyo ilianza kusikilizwa leo saa saba mchana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma na kukamilika saa 12.20 jioni.

Akizungumza nje ya Mahakama, wakili anayewawakilisha washtakiwa, Godfrey Wasonga amesema shahidi huyo amekamilisha ushahidi na walipata nafasi ya kumuuliza maswali ya dodoso.

“Shahidi ambaye tumeendelea naye leo ni yule ambaye tumeanza naye jana. Amekuja kutoa ushahidi wa utambuzi namna gani hawa washtakiwa wametambuliwa. Ametoka kwenye idara inayohusika na masuala ya utambuzi na alikuwa kwa ajili ya gwaride la utambuzi,” amesema Wasonga.

Kesi hiyo inayosikilizwa faragha itaendelea kesho Septemba 5 kwa kusikilizwa mashahidi wengine wa upande wa Jamhuri.

Amesema kwa kasi ya kesi inavyoenda wanaweza kukamilisha ushahidi kutoka upande wa Jamhuri wiki hii.

Washtakiwa katika kesi hiyo ya jinai namba 23476 ya mwaka 2024 ni askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), MT 140105 Clinton Damas maarufu Nyundo, askari Magereza C.1693 Praygod Mushi, Nickson Jackson ‘Machuche’ na Amin Lema anayejulikana pia kwa jina la Kindamba.

Related Posts