Dodoma. Wakati Bunge limezikataa sheria ndogo zenye dosari ya kuumiza wananchi kwenye halmashauri kadhaa nchini, Serikali imetoa maelekezo kuanzia sasa uandishi wa sheria ndogo lazima umshirikishe Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Mbali ya sheria ndogo za halmashauri zilizotakiwa kurekebishwa, pia zipo za wizara tisa zenye dosari.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Sheria Ndogo, Dk Jasson Rweikiza amesema hayo bungeni leo Septemba 9, 2024 alipowasilisha taarifa ya kamati kuhusu uchambuzi wa sheri ndogo.
Amesema sheria za nchi zinalazimika kuweka masharti yanayolinda na kuzingatia ipasavyo masilahi ya wananchi.
Dk Rweikiza amesema vipimo vilivyotumika kuchambua sheria ndogo hizo ni kama zina masharti yanayokizana na Katiba ya nchi, sheria mama au sheria nyingine za nchi.
Mengine ni kama zina dosari ya kutoendana na misingi ya uandishi wa sheria au zina masharti yasiyo na uhalisia, na kama zina dosari za kiuandishi wa majedwali.
Miongoni mwa sheria za halmashauri zenye dosari ni Sheria Ndogo ya (Udhibiti na Usimamizi wa Mifugo) ya Halmashauri ya Wilaya ya Moshi, 2024 (TS Na. 38/19 Januari, 2024).
Amesema kifungu cha 26 cha sheria ndogo hiyo kinataja makosa yanayokatazwa, likiwemo kosa kwa mtu yeyote kufanya shughuli za kisiasa ikiwa ni pamoja na kupandisha bendera ya chama cha siasa. Imeelezwa katazo hilo limewekwa pasipo kufafanua maeneo yanayoguswa.
“Kwa namna katazo hilo lilivyowekwa, inaweza kutafsirika kwamba, watu wote wanakatazwa kufanya shughuli za kisiasa, jambo ambalo ni kinyume cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Aidha, sheria ndogo kuwa na masharti yasiyoendana na Katiba kama ilivyo kwa sheria ndogo hii, ni dosari kubwa katika sheria za nchi. Madhara yake ni pamoja na sheria inayohusika kutokuwa halali, kukiuka misingi ya utawala wa shera na kuathiri vibaya masharti ya misingi ya demokrasia nchini. Njia pekee ya kusahihisha dosari hiyo ni kuirekebisha sheria ndogo iliyobainika kuwa na dosari,” amesema.
Mfano mwingine amesema ni Sheria Ndogo ya Usafi wa Mazingira ya Halmashauri ya Wilaya ya Kibondo, 2023 (TS Na. 920 22 Disemba, 2023). Kifungu cha 16 (e) cha sheria ndogo hii kinaweka katazo kwa mtu yeyote aliye ndani ya gari kudondosha taka ngumu nje ya gari likiwa ndani au nje ya kituo cha magari na sehemu yoyote ile ambapo gari hilo linapita.
“Sheria ndogo hii imekataza utupaji wa taka ngumu peke yake bila kujumuisha taka laini na nyinginezo. Kutokutajwa kwa taka laini na nyinginezo kunaweza kutafsirika kuwa ni ruhusu ya kutupa taka hizo. Hii inaathiri lengo la sheria kwa kushindwa kufikiwa lengo,” amesema.
Mbunge wa Nanyumbu, Yahya Mhata akizungumzia tangazo namba 217 la Halmashauri ya Mtwara kuhusu ushuru wa uvuvi na muda wa kufanya uvuvi, ukiwamo ushuru wa Sh200 wa kupaa samaki alisema:
“Wanakwenda kumtoza ushuru mtu ambaye anapaa samaki, ndugu zangu kwa wale ambao hamjui kupaa ni wale wanaosafisha samaki. Hivi kweli leo tumefikia hatua ya kwenda kutoza ushuru watu wanaopaa samaki. Unategemea kupata shilingi ngapi, wameandika hapa mpaa samaki anatakiwa alipe Sh200.
“Mwenye boti analipa ushuru, wavuvi wanalipa ushuru, kwenye mnada pale wanalipa ushuru, mtu ukichukua wale samaki ukianza kuwapaa wanakuambia ulipe ushuru, hii sasa hapa, hii hapa,” amesema.
“Hii tunawatengenezea kero, hawa vijana wameamua kujiajiri, badala ya kwenda kukaba wanafanya shughuli hii ndogondogo, hebu tuwaache vijana wetu wahangaike na hizi shughuli ndogondogo wajipatie kipato, kwanza hawapati zaidi ya Sh1,000,” amesema.
Mhata pia amezungumzia tangazao la Serikali namba 96 la Halmashauri ya Wilaya ya Magu mkoani Mwanza kwamba imetunga kanuni ya kuzuia watu kulima kwenye miteremko.
“Sisi wote tumesoma hapa kuna kilimo cha tambarare, kuna kilimo cha miteremko na kuna kilimo cha aina mbalimbali, kwa hiyo sheria hii imetungwa kuwazuia wananchi kustawi kiuchumi. Nilitarajia sheria hii itoe mbadala, kama unamzuia mtu asilime kwenye mteremko, alime nini endapo yeye anaishi kwenye mteremko,” amesema.
Amesema sheria hiyo inawarudisha nyuma wananchi na zinawaongeza katika umasikini.
Mhata amesema dosari nyingine iko kwenye tangazo la Serikali la Halmashauri ya Wilaya ya Mafinga mkoani Iringa, kanuni ikiwataka wenye vyombo vya usafiri wa umma kusimama kwenye vituo isiwe zaidi ya dakika tano.
Amesema sheria hiya ina ukakasi kwa kuwa haisemi unapopata dharura huwezi kuongeza dakika hata kama gari limeharibika, hivyo haina uhalisia.
“Halmashauri hii pia imetengeneza kanuni kwamba endapo mtu ataegesha gari maeneo yasiyoruhusiwa wanaweza kuja kulichukua gari, sasa kama watachukua gari na kuliharibu wakati wa kulichukua, sheria haisemi wao ndiyo watawajibika kulipa gharama.
“Sheria zisiwe kwa mabavu, ukikuta mtu kaegesha vibaya unapolichukua gari na likaharibika njiani, lazima ugharimie uharibifu ule. Ifanyiwe marekebisho kama kutakuwa na uharibifu basi agharimie uharibifu aliousababisha,” amesema.
Mbunge wa Nungwi, Simai Hassan Sadick amesema sheria ya Halmashauri ya Moshi mkoani Kilimanjaro inasema mfugaji yeyote atakuwa ametenda kosa ikiwa atafanya shughuli yoyote ya kisiasa, ikiwemo kupandisha bendera.
“Tatizo la hii sentensi haikujitosheleza, haikuanisha ni maeneo gani mfugaji amekatazwa kufanya hivyo. Wakati mwingine sisi tunaotunga sheria inawezekana tukawa chanzo cha tatizo,” amesema.
Mbunge wa Moshi Mjini, Priscus Tarimo amesema kuna halmashauri zimetunga sheria ya kukusanya ushuru wa mazao ya nafaka wakitaja asilimia kwa bei ya soko, bila kuonyesha bei ipi, ya Wizara ya Kilimo, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) au ni bei ya halmashauri yenyewe.
Amesema halmashauri nyingine zimeleta sheria ya ukamataji mifugo na wanapoikamata kama faini haitalipwa watapiga mnada.
“Kwa huo muda ambao wanakuwa na hao mifugo hawakuonyesha wajibu wa halmashauri kwenye kuhudumiwa mifugo hao chakula, maji na kama kwenye mnada watakosa wateja ni nani atasimamia hali za mifugo kwa hicho kipindi chote,” amesema.
Mbunge wa Lindi Mjini, Hamida Abdallah amesema Manispaa ya Mtwara, imeweka sheria ndogo ya kukamata mifugo, lakini hawakueleza endapo mifugo itakufa mmiliki atalipwa na nani.
“Mwenye mifugo pale itakapokamatwa na kufa, haki iko wapi, sheria iweke wazi mfugo akifa aliyekamata anabeba jukumu la kumlipa mwenye mfugo,” amesema.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), William Lukuvi amesema baadhi ya sheria hizo zinaleta usumbufu na taharuki kwa wananchi.
“Hapa mwisho tumemsikia mbunge juu ya wapaa samaki wa Mtwara, mimi naamini kule hata kama wanazitumia wataacha leo (Septemba 4), maana sheria kama hizi zinaleta bughudha na zinaleta maudhi kwa wananchi na nadhani wenzenu wengi, wale wanaotungatunga sheria kama hizi, kama wanasikia basi wajifunze kazi njema inayofanywa na kamati hii na wajue kamati hii haijalala,” amesema.
“Sheria zote ambazo zitakuwa zinaleta usumbufu, kero kwa wananchi zitafutwa na kamati hii. Bunge hili linaridhia kazi ya kamati hii.
“Nalihakikishia Bunge kwamba, sisi kama Ofisi ya Waziri Mkuu tutafuatilia na kusimamia wahusika wote kuzingatia maagizo ya Bunge. Tayari tumetoa maelekezo kwa mamlaka zote kwamba katika uandishi wa sheria zao ndogondogo ni lazima wamshirikishe Mwanasheria Mkuu wa Serikali,” amesema.
Lukuvi amewataka wanasheria walio chini ya ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) kwenye halmashauri wazingatie nia njema ya AG ambaye ndiye kiongozi wao ili sheria zinazokuja kuanzia sasa ziakisi nia njema ya bosi wao.
“Tamisemi ambao wana mrundikano wa sheria hizi ndogondogo sasa wanafanya vizuri, sisi tutaendelea kuwabana ili kuhakikisha zisiwepo kabisa sheria zinazokuja kutangazwa ambazo zina maudhui yanayokwenda kunyanyasa wananchi,” amesema.
AG, Hamza Johari amesema sheria tatu ziliwasilishwa kwake kwa ajili ya uhakiki, moja imehakikiwa na imetangazwa kwenye gazeti la Serikali na zingine zinaendelea kuhakikiwa.
“Sheria ndogo zinazokinzana na Katiba zimepungua kutoka 13 hadi mbili na zile zinazokinzana na sheria mama zimepungua kutoka 17 hadi 10, lakini sheria ndogo zinazokinzana na uhalisia zimeomgezeka kutoka tisa hadi 22, juhudi zaidi zinahitajika,” amesema.
Amesema watatengeneza mwongozo kuwasaidia wanasheria katika kutunga sheria ndogondogo na kutoa mafunzo yatakayosaidia kupunguza changamoto hizo.