Tanzania kuanzisha madarasa wasiojua kusoma na kuandika

Dodoma. Serikali imesema itaanzisha madarasa ya watu wasiojua kusoma na kuandika ili kuondoa changamoto hiyo.

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Omary Kipanga amesema hayo leo Jumatano Septemba 4, 2024 wakati akijibu swali la nyongeza la mbunge wa viti maalumu, Shally Raymond.

Mbunge huyo amesema hadi sasa kuna wanafunzi wanaomaliza darasa la saba lakini hawajui kusoma wala kuandika.

“Kwa kuwa hilo ni takwa maalumu katika nchi yetu, je Serikali iko tayari sasa kurejesha ule mpango wa kutoa elimu na madarasa ya jioni kwa watu wazima ambao hawakufanikiwa kujifunza kusoma na kuandika katika shule ya msingi,” amehoji.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri Kipanga amesema katika matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 inaonyesha sasa hivi idadi ya watu wasiojua kusoma na kuandika nchini ni asilimia 17.

Amesema asilimia hiyo imeshuka kutoka 22 ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2012.

“Lakini tunasema asilimia hii bado ipo kubwa kulingana na maisha ya sasa hivi na karne ya sasa hivi. Lakini naomba nimuondoe hofu mbunge katika maboresho ya sera ya elimu pamoja na mitaa tuliyoyafanya mwaka jana jambo hili limezingatiwa,” amesema Naibu Waziri Kipanga.

Amesema katika halmashauri zote wameanzisha idara pamoja na vitengo vya elimu ya watu wazima kwa maana ya elimu ya msingi na sekondari kwa maana ya kuteuwa maofisa elimu katika pande hizo.

Amesema watakwenda kuanzisha madarasa katika kata na vijiji vyote na maofisa hao watakuwa wasimamizi wa elimu hiyo.

Katika swali la msingi, Shally amehoji kuna vituo vingapi vinavyotoa elimu ya watu wazima nchini na watu wazima wangapi wanapata elimu hiyo wakiwamo wanawake.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri Kipanga amesema Serikali imeendelea kuimarisha elimu ya watu wazima kupitia programu mbalimbali zilizo chini ya sekta ndogo ya elimu ya watu wazima na elimu nje ya mfumo.

Amesema kulingana na taarifa ya Tathmini ya Sekta ya Elimu (ESA, 2024), katika Programu ya Mpango wa Uwiano Kati ya Elimu ya Watu Wazima na Jamii (Mukeja), mwaka 2023, jumla ya watu 97,217 wamenufaika katika vituo 1,851.

Amesema kati ya idadi hiyo, wanaume ni 39,789 na wanawake ni 57,428.

Naibu Waziri amesema kupitia programu ya Mpango wa Elimu ya Msingi kwa Walioikosa (Memkwa), mwaka 2023, jumla ya wanafunzi 57,843 wamenufaika katika vituo 2,557.

Amesema kati ya idadi hiyo wavulana ni 32,141 na wasichana ni 25,702.

Naibu Waziri amesema katika programu ya Mpango wa Elimu Changamani Baada ya Elimu ya Msingi (IPPE), jumla ya wanafunzi 9,368 wamenufaika katika vituo 89.

Amesema kati ya idadi hiyo wanaume ni 5,036 na wanawake ni 4,332.

Aidha, amesema katika programu ya Mpango wa Elimu Changamani kwa Vijana Walio Nje ya Shule (IPOSA), jumla ya vijana 42,183 wamenufaika kupitia katika vituo 85.

Amesema kati ya idadi hiyo, wanaume ni 20,195 na wanawake ni 21,988.

Pia, amesema katika programu ya elimu ya sekondari kwa njia mbadala, wanafunzi 11,721 ikijumuisha wavulana 5,529 na wasichana 6,192 walidahiliwa kwa mwaka wa masomo wa 2023.

Amesema masomo hayo yalitolewa katika vituo 777 (vituo vya serikali 160, na vituo vya wadau binafsi 617).

Related Posts