Mwanza. Teknolojia ya kisasa ya utengenezaji wa bidhaa inatajwa kunogesha Maonyesho ya Wafanyabiashara Afrika Mashariki (MEATF) mwaka 2024 yatakayohusisha kampuni zaidi ya 200 kutoka Tanzania na 35 kutoka nje ya nchi.
Kampuni 35 zilizothibitisha kushiriki maonyesho hayo ya 19 ya MEATF zinatokea nchini Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Kenya, Uganda, India na China huku uzinduzi wake ukitarajiwa kufanywa na Waziri wa Viwanda na Biashara, Selemani Jafo.
Akizungumza leo Jumatano Septemba 4, 2024, Mwenyekiti wa Chemba ya Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) Mkoa wa Mwanza, Gabriel Kenene amesema maonyesho hayo yataanza Septemba , hadi 15 mwaka huu katika Viwanja vya Furahisha jijini Mwanza.
Kenene amesema washiriki kutoka ndani ya nchi watanufaika kwa kuchota ujuzi wa utengenezaji bidhaa mbalimbali zikiwamo za chakula kutoka wafanyabiashara na wazalishaji bidhaa kutoka mataifa bingwa wa teknolojia ya India na China.
“Kupitia maonyesho hayo tunaamini wafanyabiashara wa Tanzania watakuza mtandao wao wa biashara kwa kupata marafiki wapya katika sekta ya uzalishaji bidhaa na wateja wapya wa bidhaa zao. Pia, kukuza teknolojia yao kwenye uzalishaji,” amesema Kenene.
Amesema tofauti na watu 250,000 waliotembelea na kujifunza ujuzi mbalimbali katika maonyesho hayo mwaka 2023, watu zaidi ya 300,000 wanatarajiwa kutembelea maonyesho ya mwaka huu.
“Waonyeshaji wote kutoka nje ya ndani ya nchi wanaombwa kufuata taratibu za mauzo wakati kwa kutoa risiti halali kama sheria inavyoelekeza,” amesema Kenene.
Pia, amesema watakaotembelea maonyesho hayo watapata fursa ya kushuhudia wanyama pori wakiwamo simba, chui, fisi, ngamia na wanyama wengine, jambo alilodai linalenga kuongeza hamasa kwa wazawa na wageni kutembelea hifadhi za taifa.
Mfanyabiashara wa urembo eneo la Relini jijini Mwanza, Hasinath Juma ameiomba TCCIA, kuboresha utaratibu wa kuingia ili kuruhusu watu wa aina zote yakiwamo makundi maalumu kuingia na kujifunza ujuzi mpya wa utengenezaji bidhaa kwa wazalishaji wa ndani na nje ya nchi.
“Tumekuwa tukienda kutazama maonyesho ya MEATF kwa miaka iliyopita, lakini kwa watu wa makundi maalumu hususan viziwi hawawekewi watafsiri ili kuwawezesha kuelewa kinachoendelea kutoka kwa washiriki wanapotembelea mabanda,” amesema Hasinath.
Rosemary Bilinga ambaye ni mamalishe amesema maonyesho hayo ni fursa kwa wafanyabiashara na mamalishe wanaoishi na kufanya shughuli zao kuzunguka eneo la Furahisha kujiongezea kipato huku akiwasihi kuongeza ubunifu.
“Mara nyingi wafanyabiashara wanapokuja kutoka nchi mbalimbali duniani wanakuwa na hamu ya kujaribu ladha tofauti ya vyakula na utamaduni.