Dar es Salaam. Abiria wanaotumia usafiri wa treni kupitia reli ya Tazara kutoka Dar es Salaam hadi Mbeya wameiomba Serikali kuingilia kati usimamizi wa shirika hilo ili kuondoa adha zinazowakumba.
Abiria hao wamesema changamoto haziishi kutokana na kukwama mara kwa mara kwa safari, wakieleza wanahisi hali hiyo inatokana na usimamizi mbovu.
Wamesema wamekuwa wakipata usumbufu ikiwamo kulala njiani kiasi cha kushindwa kuwahi wanakokwenda.
Wameeleza hayo baada ya abiria takribani 250 waliotakiwa kusafiri kwenda Mbeya kutokea Dar es Salaam kukwama kwa saa 24 katika stesheni ya Tazara mkoani Dar es Salaam.
Ofisa Uhusiano kwa Umma kutoka Tazara Tanzania, Regina Tarimo amesema kumekuwa na changamoto za mara kwa mara kutokana na uchakavu wa mabehewa.
“Si kwamba tunapenda kutesa abiria tuna changamoto ya uchakavu wa mabehewa na pia ni machache kiasi kwamba yanatakiwa kufanyiwa matengenezo mara kwa mara na wakati mwingine yanachukua muda mrefu,” amesema.
Regina amesema kilichotokea hadi abiria kukwama kuondoka jana Septemba 3, 2024 ni treni kuchelewa kufika Dar es Salaam.
Ameeleza ilitakiwa kuwa Dar es Salaam Jumapili Septemba mosi saa 11.00 jioni ili iondoke Jumanne Septemba 3 saa 7.50 mchana.
“Badala yake ilifika jana saa (Septemba 3) saa 7.00 mchana. Kutokana na kuchelewa kuwasili ilibidi mabehewa yapelekwe matengenezo na yamechukua muda mrefu. Huwezi kusafirisha abiria na mabehewa mabovu.
“Tulitegemea matengenezo yakamilike jana, ilishindikana hadi leo Septemba 4 asubuhi yalipomalizika. Treni kuelekea Mbeya imeondoka saa 5.30 asubuhi,” amesema.
Regina amewaomba radhi abiria wote kwa usumbufu uliojitokeza, akisema wanaendelea na uboreshaji ili kutoa huduma kwa abiria.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Mwananchi katika Stesheni ya Tazara, Dar es Salaam, baadhi ya abiria wamesema usafiri huo si wa uhakika kutokana na kukwama mara kwa mara.
“Binafsi nimechoka, Mei mwaka huu ilikwama Mbeya watu tulikaa stesheni kwa siku tatu. Kutoka jana tuko hapa hakuna wanachotueleza sababu zilezile. Tunaomba Serikali iingilie kati tunapata shida katika usafiri huu,” amesema abiria Joseph Mwakenja.
Amesema baada ya kukata tiketi aliripoti kituoni hapo jana Septemba 3, saa 6.30 mchana lakini treni haikuondoka na hawakupewa taarifa sahihi ya sababu za kutoondoka kwa wakati.
Amedai walipowafuata viongozi ofisi zao zilikuwa zimefungwa.
“Watu wana familia wamelala hapa nje sehemu ya wazi na hakuna abiria aliyeruhusiwa kulala ndani wote tulitolewa,” amesema Mwakenja.
Sakina John, amesema upatikanaji wa chakula ulikuwa changamoto, akisema hawakutendewa haki akieleza shirika lilipaswa kugharimia kutokana na adha hiyo.
“Tumepata shida, mazingira ya kulala umeniona hapa nina familia ya watoto watatu tunaenda Mbeya, lakini baada ya changamoto hii hatukurusiwa kulala ndani ya mabehewa abiria wote tulitolewa.
“Wengi tulilala sehemu hizi za wazi, kulikuwa na baridi kali na mbu wametung’ata usiku mzima. Uongozi uko kimya, ikitokea hali kama hii taasisi ilitakiwa igharimie kutulisha sababu ni wao si sisi,” amesema.
Abiria mwingine, Zacharia Mwakalinga amehoji iweje shida hiyo ijirudie na hawaoni mabadiliko.
“Hatusafiri bure tunatoa nauli sasa inafanya kazi gani tunaelezwa mabehewa yameharibika kwani hawana bajeti ya kufanya matengenezo, ni muhimu Serikali iangalie vinginevyo wapewe wanaoweza kuendesha na si kutesa abiria,” amesema.
Jumanne Novemba 21, 2023, abiria wa treni ya Tazara walikwama hadi Jumatano Novemba 22 kusafiri.
Alipotafutwa Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile kuzungumzia tatizo hilo mwaka jana, alisema kumekuwapo na changamoto ya treni, uchache wa vichwa na ubovu wa miundombinu.
Alisema mkakati wa muda mrefu, Serikali inafikiria kufanya maboresho makubwa kwa kushirikisha nchi ambazo wanashirikiana tangu wakati wanajenga reli hiyo.
“Tunaweza kuja na mpango mkubwa, nadhani kuanzia mwakani (2024) wa namna ya kufumua reli hiyo na kuiboresha pamoja na kuweka mfumo mzuri ikiwemo kuongeza mabehewa kupitia uwekezaji,” alisema.
“Serikali imejipanga kuja na muarobaini wa namna ya kumaliza tatizo na kupata ufumbuzi wa kudumu,” alisema.