Umakini mdogo waikosesha Stars Kwa Mkapa

TIMU ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars imebanwa nyumbani kwa kutoka suluhu kwenye uwanja wa nyumbani wa Benjamin Mkapa dhidi ya Ethiopia katika mchezo wa kwanza wa Kundi H wa kuwania Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 za  Morocco.

Stars iliyopo kundi moja na timu za DR Congo na Guinea, itajilaumu kwa suluhu hiyo ikiwa  nyumbani kwa kushindwa kutumia nafasi ilizotengeneza hasa kipindi cha pili.

Licha ya stars kuanza kwa kuonyesha kuhitaji pointi tatu za mchezo huo, lakini ilikosa utulivu maeneo yote na kujikuta inacheza zaidi eneo la kati ya uwanja.

Dakika 45 za kipindi cha kwanza timu hiyo ilipiga mashuti matatu tu ambayo hayakulenga lango kutokana na umakini wa mabeki wa Ethiopia na kuwanyima nafasi ya kufunga.

Eneo la ulinzi la timu ya taifa likiongozwa na kipa Ally Salim wanapo salama lilifanya kazi kwa usahihi, shida kubwa ni eneo la kiungo ambao wachezaji Feisal Salim, Himid Mao na Novatus Dismas wameshindwa kuendana na kasi ya Waethiopia  waliokuwa wametawala eneo hilo.

Clement Mzize, licha ya kuonyesha jitihada za kusaka nafasi ya kufunga alikosa wa kumtengenezea pasi za mwisho na kujikuta anahaha uwanja mzima akisaka mipira na kuwasaidia mabeki kukaba lango lisipate mashambulizi.

Kipindi pili, Stars ilianza kwa mashambulizi ya haraka wakisaka bao la kuongoza dakika ya 47 wamepata kona ambayo haikuwa na madhara kwa Ethiopia.

Pamoja na kuingia kwa kasi wakisaka bao wageni nao walionyesha pia utulivu kwa kucheza mpira wa kujilinda na kushambulia kwa pamoja.

Mabadiliko ya wachezaji watatu yaliyofanywa kwa kuwatoa Nickson Kibabage, Himid Mao na Edwin Balua na nafasi ikichukuliwa na Pascal Msindo, Mudathir Yahya na Wazir Junior yaliongeza uhai kikosini na kuifanya Stars ilibadili aina ya uchezaji.

Mashambulizi waliyoyaonyesha yalisaidia kupata kona mbili kipindi cha pili ambazo hata hivyo hazikuzaa matunda kwani uimara wa kipa na mabeki wa Ethiopia ulizuia Stars kupata ushindi kwenye uwanja wa nyumbani.

Stars sasa inajiandaa kuvaana na Guinea ikiwa ugenini katika mechi ijayo itakayopigwa Jumanne. Keshokutwa Ijumaa, Guinea itakuwa wageni wa DR Congo katika mechi nyingine ya kundi hilo.

Ally Salim, Nickson Kibabage, Ibrahim Abdullah ‘Bacca’, Dickson Job, Feisal Salum, Himid Mao, Clement Mzize, Mohammed Hussein, Lusajo Mwaitenda, Edwin Balua na Novatus Dismas

Related Posts