Wadau wasimama kidete kukosoa kauli tata za viongozi kuhusu uchaguzi

Dar es Salaam. Kufuatia kauli tata zinazoendelea kuibuka zikihusu rafu katika chaguzi mbalimbali nchini Tanzania, wadau wa siasa wameibuka na kupinga vikali huku wakitaka muafaka kukomesha kauli hizo ili kuwezesha kuwapo kwa chaguzi huru na haki.

Wadau hao wamezichambua kauli zilizotolewa hivi karibuni na viongozi wa Serikali pamoja na Chama cha Mapinduzi (CCM), katika mjadala wa X-Space (zamani Twitter), ulioandaliwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL).

Mjadala huo uliokuwa na mada: ‘Kauli tata za viongozi kuelekea kwenye uchaguzi zinatafsiri gani?’ umefanyika leo Jumatano, Septemba 4, 2024 na kuwashirikisha wadau mbalimbali wakiwamo wasomi na wanasiasa.

Msingi wa mjadala huo ni kauli zilizotolewa kwa nyakati tofauti na aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Longido (DC) mkoani Arusha, Marco Ng’umbi, aliyekuwa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknoloaji ya Habari, Nape Nnauye na Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Mkoa wa Lindi, Palina Ninje kuhusu chaguzi.

Ng’umbi na Nape walitenguliwa uteuzi wao na Rais Samia Suluhu Hassan huku Kamati Kuu ya CCM chini ya uenyekiti wa Rais Samia ikimvua uongozi Palina.

Kauli za watatu hao, walizozitoa kwa nyakati na mazingira tofauti, ziliibua mijadala mikali katika mitandao ya kijamii na kuonesha hofu katika chaguzi zijazo za Serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 27, 2024 na Uchaguzi Mkuu 2025.

Mijadala hiyo mitandaoni ilikwenda mbali na kuonesha kauli hizo zinakwenda kinyume na falsafa ya 4R za Rais Samia ambazo amekuwa akizitumia kwenye utawala wake na kuwataka wasaidizi wake kuziishi.

Hata hivyo, CCM kwa nyakati tofauti imejitenga na kauli hizo na kueleza ni maoni yao binafasi. Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla alianza kuipinga kauli ya Nape aliyesema ushindi si lazima ndani ya boksi na kura na hii ya Ng’umbi aliyosema ni mtazamo wake kuwa si madiwani wote walishinda.

Katika mjadala wa leo Jumatano, Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT), Dk Revocatus Kabobe amesema kauli hizo zinarudisha nyuma maendeleo ya demokrasia hapa nchini.

Amesema kitendo cha kiongozi wa Serikali kuibuka hadharani na kusema kuhusu kubebwa kwenye uchaguzi uliopita kinajenga msingi mbaya katika chaguzi zijazo.

Dk Kabobe amesema kauli zinabagaza mfumo mzima wa uchaguzi pamoja na kufifisha juhudi za demokrasia imara.

“Inafanya watu watambue kumbe kuna mpango mwingine pembeni umeshaandaliwa. Inafufua machungu ya uchaguzi wa 2019 na 2020 kauli zinajenga msingi mbaya katika mazingira ya uchaguzi unaokuja,” amesema Dk Kabobe.

‘Hatua zaidi zichukuliwe’

Mwandishi wa habari mwandamizi, Luqman Maloto akichangia mada hiyo amesisittiza hatua zaidi zinapaswa kuchukuliwa ukiachana na kufukuzwa kwenye nafasi zao kwani inawezekana wako wengi wa namna hiyo.

“Nitashangaa kama vyama vya siasa vitaendelea na mchakato wa uchaguzi ikiwa kauli hizi hazijapatiwa majibu sahihi,” amesema na kushauri kuwe na muafaka juu ya kauli hizo hususani katika kipindi hiki kuelekea kwenye chaguzi zijazo ikiwamo Serikali ya mitaa.

Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Conrad Masabo amesema kukosa demokrasia ya kweli ni sababu ya viongozi waliohusika katika usimamizi wa uchaguzi uliopita kushindwa kuwajibika.

“Historia inaonesha kuna kauli nyingi tata zimekuwa zikitolewa na viongozi licha ya kuleta gumzo lakini hakuna aliyewahi kuwajibika, uchaguzi uliopita ulilalamikiwa viongozi waliosimamia walipaswa kuwajibika,” amesema. 

Kwa upande wake, Mwinyi Mtula amesema kutokana na kauli za wanasiasa wananchi wanapaswa kuwa makini katika ufikiri kwa kuwa wengi wanataraji kuona mabadiliko ya maendeleo.

“Wananchi wengi wanakabiliwa na changamoto hasa wa vijijini. Wananchi wamekuwa na changamoto ya kupata elimu ya siasa na hawapati majukwaa sahihi ya kusikiliza ili waweze kupanua ufikiri wao,” amesema.

Kuelekea katika uchaguzi, Mtula amevishauri vyama vya siasa kutoa elimu kwa wananchi kwa kuwaeleza bayana iwapo watashiriki ili wapate wigo mpanga wa kuchagua viongozi wanaowataka.

‘Tupige kura, tuzilinde’

Naibu Katibu Mkuu Bara wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma)-Bara, Eugene Kabendera amevisihi vyama na wananchi wote wakapige kura pia wakae tayari katika uchaguzi huo.

“Lazima tujipange kuhakikisha wanaopanga kuvuruga basi hawafanikiwi. Wananchi wanatakiwa wasimame kidete kwa kujitokeza kwa wingi,” amesema.

Mtangazaji Burton Mwemba, maarufu Mwijaku ameishauri Serikali kuona umuhimu wa kuwa na mfumo mzuri wa kuangalia aina ya upatikanaji viongozi kwa baadhi ya nafasi hasa zile za kuteuliwa na Rais au taasisi fulani.

“Kumteua mtu lazima kuwe na utaratibu wa aina mbili kwanza kwa kuangalia historia yake kwa kuzingatia anachokwenda kukifanya, wengi wanaingia kwenye siasa si eneo lao mtu amesoma kuanzia kidato cha kwanza hadi kidato cha nne hajawahi kuwa kiranja.

“Amekuja chuo hajawai kuwa kiongozi anakuja mbele anajua kuongea anaonekana na anapewa nafasi ya U-DC (mkuu wa wilaya) matokeo yake anashindwa kuchagua maneno ya kuzungumza, lakini tukitengeneza mfumo hata akichaguliwa na taasisi fulani tunarejea historia yake aliwahi kuwa hata kiranja?

“Tunapaswa kutambua viongozi wengi ni wateule kutoka kwa Rais anayewapa mamlaka na walio wengi wabinafsi anapoona hapati nafasi ya kuwa karibu na kiongozi fulani ndipo tunaanza kuona matamshi ambayo si mazuri kwa chama na Serikali yake.”

Katika hoja yake ya pili, Mwijaku amependekeza umuhimu wa kuangalia uwezo wake wa kufikiri kuna kauli zinaweza kutolewa na kiongozi na kubaki na maswali ya kujiuliza ni kiongozi au chawa?

“Ni muhimu tujue kutofautisha kati ya chawa na kiongozi, chawa anaweza kukaa na kusifia chochote lakini kiongozi akitoa kauli ajue ni uamuzi wa Serikali kwa kuwa umepewa sehemu ya kuwakilisha.”

Related Posts