Geita. Wanafunzi 162 kati ya 3,255 wenye uhitaji maalumu kutoka shule 15 za msingi katika Halmashauri ya Geita, wameacha shule kwa kipindi cha miaka mitatu.
Hata hivyo, imeelezwa kati ya hao 162, wanafunzi 115 wameacha shule mwaka huu pekee.
Taarifa ya ufuatiliaji wa elimu jumuishi katika Halmashauri ya Mji wa Geita, iliyofanywa na Shirika lisilo la kiserikali la Marafiki wa Elimu kuhusu utekelezaji wa muongozo wa kitaifa wa elimu jumuishi 2022/26, imebainisha asilimia 71 ya wanafunzi hao 115 wameacha shule mwaka huu wa 2024.
Katibu mlezi wanawake na watoto wa shirika hilo, Nurath Swalehe akisoma taarifa ya majumuisho ya ufuatiliaji huo leo Jumatano Septemba 4, 2024, amesema sababu kuu za wanafunzi hao kuacha shule ni ukosefu wa miundombinu rafiki, uhaba wa vifaa saidizi vya kujifunzia, pamoja na magonjwa ya muda mrefu.
Swalehe pia ameongeza kuwa baadhi ya wazazi hawana mwamko juu ya elimu ya watoto wenye mahitaji maalumu, hususan wale wenye changamoto za afya ya akili.
“Mfano, wazazi wengi wenye watoto wenye changamoto za afya ya akili ni wagumu kuamini changamoto hizo, na hata wanapopewa maelekezo ya namna ya kuwasaidia, hawako tayari,” amesema Swalehe.
Mbali na changamoto za wanafunzi kuacha shule, elimu jumuishi pia inakabiliwa na upungufu wa walimu wenye mafunzo maalumu. Kati ya shule 15 za msingi na 10 za sekondari, ni walimu 61 pekee kati ya 631 waliopata mafunzo ya elimu jumuishi ambao ni sawa na asilimia 9.6.
Pia kati ya walimu hao, walimu wenye taaluma ya elimu maalumu ni 16 pekee, hali inayowalazimu kufundisha wanafunzi wengi darasani, kinyume na miongozo.
Ofisa elimu wa elimu maalumu wa Halmashauri ya Mji wa Geita, Mery Venance akizungumzia utoro kwa wanafunzi hao, amesema upo, lakini kwa kiasi kikubwa unasababishwa na hali walizonazo wanafunzi hao.
“Inawezekana wanaonekana watoro, lakini hii inatokana na hali zao. Mfano, wanaotumia viti mwendo wakishindwa kupata mtu wa kuwasaidia kufika shuleni hawawezi kwenda, na pia si wote wanaoweza kuhudhuria masomo kila siku kutokana na hali zao,” amesema Venance.
Ameongeza kuwa licha ya changamoto hizo, wanaendelea kutoa elimu kwa wazazi, walezi na jamii kwa ujumla, ili waone umuhimu wa elimu kwa watoto wenye uhitaji maalumu na wasiwachukulie juu juu.
Mkuu wa dawati la jinsia na watoto kutoka Jeshi la Polisi Geita, Grace Kaijage amesema kesi nyingi zinazoripotiwa zinahusu watoto kukiuka sheria, ikiwa ni pamoja na vitendo vya uhalifu miongoni mwao.
“Kwa sasa kuna ongezeko la watoto shuleni kulawitiana au kuchezeana wao kwa wao, na wengine wanakumbana na ukatili kwa kurubuniwa na fedha kidogo. Mfano, unamhoji mtoto anasema alikutana na mtu aliyempa Sh200, akamlaza na kumfanyia mambo mabaya. Hii inaonyesha ni kwa jinsi gani watoto wanahitaji kulindwa, lakini bado hatutekelezi majukumu yetu ipasavyo,” amesema.
Mjumbe wa kamati ya Shule ya Msingi Kalangalala, amesema changamoto za makuzi na malezi kwa watoto zipo na baadhi ya wanafunzi badala ya kwenda shule wamekuwa wakijificha vichakani, huku wakijihusisha na vitendo viovu.
Kikao hicho cha majumuisho ya taarifa ya ufuatiliaji wa elimu jumuishi kimehudhuriwa na maofisa elimu wa halmashauri ya mji, maofisa elimu kata, walimu wakuu pamoja na wajumbe wa kamati za shule.