Na Mwandishi Wetu, Michuzi Tv
WATU wanaoishi na Virusi vya Ukimwi wametakiwa kufuata maelekezo ya daktari wanapotumia dawa za kufubaza virusi hivyo ili kuepukana na tatizo la usugu wa vimelea kwenye dawa hizo.
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMRI) Profesa Said Abood ameyasema hayo leo Septemba, 4, 2024 jijini Dar es Salaam wakati wa kongamano la 11 la Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas).
Profesa Abood amesema matumizi ya dawa kiholela na kutofuata maelekezo ya daktari husababisha kirusi cha ukimwi kujenga usugu.
“Mgonjwa akitumia dawa kiholela yule kirusi anapata fursa ya kujenga usugu dhidi ya ile dawa anayotumia na matokeo yake ni kushindwa kufanya kazi,”amesema.
Kwa upande wake, Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Muhas, Profesa Emmanuel Balandya amesema kongamano hilo ni mwendelezo wa juhudi zao katika kuhakikisha wanashirikisha wadau mbalimbali kutoka wizara ya afya na sehemu nyingine kuangalia ni wapi wamefika katika kushughulikia tatizo hilo.
Kwa mujibu wa Profesa Balandya, asilimia tano ya wanaotumia baadhi ya dawa wana usugu ambapo pia, wapo wale wanaotumia dawa haziwasaidii na asilimia 90 wamegundulika wana usugu.
Naye, Mhadhiri Mwandamizi na Mtafiti wa Muhas, Dkt Doreen Kamori amesema mwaka 2020 walifanya utafiti katika mikoa 22 kuangalia ukubwa wa tatizo la usugu wa dawa za kufubaza na kupunguza makali ya VVU na kugundua kuwa wenye usugu wengi ni wale walioko kwenye matibabu.
Amesema dawa mojawapo inayojulikana duniani kuwa ni nzuri sana iliyoingizwa nchini 2019 ya dolutegravier licha ya kusifiwa kwa ubora na ufanisi wake wa kupunguza makali, wamegundua ina viashiria vya kuonesha kuna resistance dhidi ya dawa hiyo.
Dkt Kamori amesema wamegundua kuna watu asilimia 5.8 dawa hiyo ilishindwa kufanya kazi vizuri.
“Tunaona kama nchi tunapofikiria kubadilisha dawa au kuitambulisha katika nchi ni vyema kuweka miongozo na kujiandaa vizuri kwa kufanya tafiti kuangalia wingi wa virusi kwa watu walioko kwenye tiba na kujipanga taratibu kuingia kwenye dawa mpya, kuwafuatilia watu wanaoishi na virusi kubaini kama zina changamoto,”amesema.
Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo (Muhas) Profesa Emmanuel Balandya, akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati wa kongamano la 11 la Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas) katika kongamano hilo lilifanyika chuoni hapo leo Septemba 4,2024, pamoja na mambo mengine, wataalamu watajadili mikakati ya kukabiliana na tatizo la usugu wa dawa za ARV.
Mhadhiri Mwandamizi na Mtafiti wa Muhas, Dkt Doreen Kamori Akizungunza wakati wa Kongamano hilo.
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMRI) Profesa Said Abood akifafanua jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) mara baada ya kufungua kongamano la 11 la Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas) katika kongamano hilo lilifanyika chuoni hapo leo Septemba 4,2024, pamoja na mambo mengine, wataalamu watajadili mikakati ya kukabiliana na tatizo la usugu wa dawa za ARV.