WMA YAHIMIZA MATUMIZI YA MIZANI ILIYOHAKIKIWA KWA WAFANYABIASHARA WA GESI

Afisa Vipimo, Wakala wa Vipimo (WMA), Mkoa wa ki-vipimo Ilala, Yahya Tunda akiwasilisha Mada kuhusu nafasi ya WMA katika uhakiki wa vipimo vya gesi za kupikia kwa wafanyabiashara wa nishati hiyo. Semina hiyo jumuishi iliandaliwa na Kampuni ya Gesi ya Oryx na kufanyika Segerea jijini Dar es salaam,

Na Pendo Magambo – WMA, Dar es Salaam

Wakala wa vipimo Tanzania (WMA) imewataka wafanyabiashara wa gesi kutumia mizani iliyohakikiwa na WMA ili kujiridhisha na usahihi wa uzito wa mitungi ya gesi kabla ya kuiuza kwa wateja.

Wito huo ulitolewa jijini Dar es Salaam na Afisa Vipimo Yahya Tunda kutoka WMA Mkoa wa kivipimo Ilala, wakati wa semina jumuishi iliyoandaliwa na kampuni ya Gesi ya Oryx kwa lengo la kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa wote.

Tunda alieleza kuwa WMA inatekeleza majukumu yake kupitia Sheria ya Vipimo sura namba 340, ambayo inasimamia matumizi ya vipimo sahihi na kwa upande wa wafanyabiashara wanaotumia mizani, sheria inawataka kutumia zile zilizohakikiwa na WMA ili kuleta usawa wa kivipimo kwenye maeneo ya biashara, afya, usalama na mazingira.

“Ninawashauri wafanyabiashara pindi wanapotaka kununua mizani kufika katika ofisi zetu ili wapate ushauri wa kitaalamu kuhusu aina inayofaa kulingana na biashara wanazofanya,” alisisitiza.

Akizungumzia kuhusu mizani inayotumiwa na wafanyabiashara kuhakiki uzito wa bidhaa, Tunda alisema kuwa sheria inaelekeza kuweka kibandiko kinachoonesha tarehe ambayo mizani ilihakikiwa pamoja na tarehe ya kurudia uhakiki wake.

Aidha, aliwataka wafanyabiashara wa gesi walioshiriki semina hiyo kuwa mabalozi kwa wengine.

Kwa upande wake, Msimamizi wa kampuni ya Oryx, Wilaya ya Ilala, Evarist Kisaka aliishukuru WMA kwa kuitikia wito na kutoa elimu ya matumizi sahihi ya vipimo kwa wafanyabiashara wa gesi na wadau mbalimbali wa nishati safi ya kupikia.

“Waliohudhuria leo wamepata maarifa mengi, nina uhakika wataenda kufanya biashara zao kwa mlengo chanya zaidi maana wamejua faida za kuwa na vipimo sahihi, suala ambalo litawajengea uaminifu kwa wateja,” alisema.

Pamoja na jukumu lake la msingi ambalo ni kumlinda mlaji na mfanyabiashara, WMA pia inachagiza matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa wote kwa kuhakikisha kuwa panakuwa na usawa katika vipimo vya bidhaa hiyo yanayoendana na thamani ya fedha katika biashara husika.

Related Posts