AKILI ZA KIJIWENI: Zahera bado hayupo salama Namungo

MWINYI Zahera mwanzoni mwa wiki hii alipitia katika kikaango baada ya kuponea chupuchupu kutimuliwa na Namungo kutokana na mwenendo usioridhisha wa timu hiyo,

Baada ya Namungo kupoteza mchezo dhidi ya Fountain Gate kwa mabao 2-0 nyumbani, kocha huyo alikutana na kadhia ya mashabiki wa timu hiyo ambapo alirushiwa makopo kwenye Uwanja wa Majaliwa huko Ruangwa, Lindi na baada ya hapo mabosi kadhaa wa timu hiyo walikubaliana kuwa wamtimue.

Kabla ya hapo, Namungo ilikuwa imepoteza mechi ya kwanza ya msimu dhidi ya Tabora United kwa mabao 2-1 tena ikiwa nyumbani kwenye Uwanja huohuo wa Majaliwa.

Hata hivyo, huruma za kigogo mmoja mwenye nguvu ya kiuamuzi ndani ya Namungo zikamuokoa Zahera anayeendelea kuwa kocha mkuu wa kikosi hicho cha Wauaji wa Kusini.

Kuendelea kubakishwa katika majukumu yake, hata hivyo hakupaswi kumfanya Zahera abweteke na kujiona yupo katika mazingira salama ndani ya timu hiyo na badala yake anatakiwa afanye kazi ya ziada ili kuhakikisha timu inarudi katika mstari.

Uamuzi wa kumbakiza inawezekana umefanyika ili uongozi wa Namungo usije kuonekana una mihemko na unafanya uamuzi kwa kufuata kelele za mashabiki lakini kiuhalisia viongozi wa timu hiyo hawamtazami wala kumuelewa vizuri Zahera.

Kitendo cha viongozi hao kumuongeza aliyekuwa kocha msaidizi wa Coastal Union, Ngawina Ngawina katika mechi la ufundi ni ishara tosha kuwa imani ambayo walikuwa nayo kwa Zahera imepungua na wanadhani kuna kitu kimepungua ndio maana wakamleta msaidizi kutoka timu nyingine.

Na bahati mbaya kwa Zahera ni kwamba huyo msaidizi ambaye wamemletea ana Leseni ya ukocha Daraja A ya Shirikisho la Soka Afrika (Caf) ambayo inampa uhalali wa kusimamia benchi la ufundi la timu kwenye Ligi Kuu Bara.

Kwa sisi tuliosoma elimu ya Cuba, hapo tunafahamu fika kuwa wenye timu wanataka siku ambayo watachukua uamuzi wa kumuacha Zahera wasipate tena tabu ya kutafuta kocha wakati wana Ngawina ambaye anaruhusiwa kikanuni kuongoza benchi la ufundi lakini pia ana uzoefu na soka la Tanzania.

Related Posts