TIMU ya JKT iliwashangaza wengi pale ilipoifunga timu ngumu ya Dar City kwa pointi 83-66 katika ligi ya kikapu mkoa wa Dar es Salaam (BD) iliyofanyika kwenye Uwanja wa Donbosco Oysterbay.
Dar City itabidi ijilaumu yenyewe kupoteza mchezo huo kutokana na kushindwa kutegua mfumo wa uchezaji uliotumiwa na timu ya JKT.
Mfumo uliotumiwa na JKT ulikuwa ni wa wachezaji kuimarisha ulinzi zaidi, hali iliyofanya wachezaji wa timu ya Dar City washindwe kupenya katika robo zote nne.
Kassim Jumbe, kocha wa kikapu kutoka Temeke, alisema wachezaji wa timu hiyo walipaswa kutegua mfumo huo kwa kurusha mpira katika maeneo ya mitupo ya pointi tatu (three point).
Kutokana na mfumo huo, wachezaji wa timu hiyo Dar City, Jamel Marbuary, Erick John, Ally Abdallah na Bramwel Mwombe na Haji Mbengu walishindwa kuonyesha makali yao.
Katika mchezo huo, Omary Sadiki aliongoza kwa kufunga pointi 17, aliongoza pia kwa kutoa asisti kwa wachezaji wenzake mara 6, huku kwa upande wa Dar City kinara alikuwa Jamel Marbuary aliyefunga pointi 13.
Kocha wa timu ya JKT, Chriss Weba, alisema aliwaambia wachezaji wake wacheze mfumo huo kutokan ana kuzisoma vyema mbinu na uwezo wa wachezaji wa timu ya Dar City.
“Kwa kweli tulifanikiwa. Mchezo tuliocheza kwa mfumo huu tutakuwa tunautumia katika mechi dhidi ya timu zenye wachezaji wenye uwezo mkubwa,” alisema Weba.