Moshi. Mkuu wa Wilaya ya Moshi, James Kaji ameagiza kukamatwa na kuchukuliwa hatua kwa watu waliohusika na uharibifu wa miundombinu ya maji yenye thamani ya Sh14 milioni katika Kijiji cha Sango kilichopo wilayani humo.
Uharibifu wa miundombinu hiyo ya maji unadaiwa kufanywa usiku wa kuamkia Septemba 4, 2024 na baadhi ya watu katika kijiji hicho ambao wanapinga kuwekewa mita za maji kwa madai kuwa hawawezi kulipia, maji ni yao.
Akizungumza baada ya kutembelea mradi huo na kujionea uharibifu uliofanyika, mkuu huyo wa wilaya amesema Serikali inatumia fedha nyingi katika kuhakikisha miradi ya maji inatekelezwa na wananchi wanapata huduma hiyo, hivyo hawatawavumilia wala kuwafumbia macho wanaokiuka sheria na kuharibu kwa makusudi miundombinu ya maji.
“Hakuna mwenye umiliki wa miundombinu ya maji, yote ni ya Serikali, haiwezekani Serikali inatoa mabilioni ya fedha halafu watu wawili watatu wanakuja kuhujumu, hakuna mtu anayeweza kusema maji haya ni ya kwangu. Serikali inatumia tedha nyingi kutekekeza miradi hii, leo shukrani tunakuja kufanya kitu kama hiki, haiwezekani.
“Nimepata taarifa kuna watu wanasema kuna maji sijui ya Lucy Lameck, sijui maji ni ya kwetu, hakuna mwenye haki hiyo, maji ni ya Watanzania wote, nitoe onyo, Serikali hii ni sikivu na asije mtu akajifanya mbabe mbele ya Serikali. Kama kuna tatizo tukae tujadiliane na Serikali ni sikivu, kuna viongozi, lakini unapojichukulia hatua mkononi, hapana.”
Kaji ameongeza kuwa: “Ninasikia kuna kikundi nimeshapata majina yenu, siwafichi nitaanza na nyinyi, inapofikia hatua ya kufifisha juhudi za Mheshimiwa Rais za kutoa huduma kwa wananchi, unachukua hatua mkononi hapana, OCD, taratibu za kisheria zifuatwe na wahusika wote waliofanya hivi, wakamatwe.”
Ametumia pia nafasi hiyo kuwaonya wanaotumika kisiasa katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi na kuwataka wananchi wote kushiriki kulinda miundombinu ya maji.
“Najua kuna wengine mnatumika, niwaonye jamani, msitumike na wanasiasa, kipindi cha uchaguzi kinakuja, tafadhali epukeni kutumika kwani unapohujumu miundombinu ya maji, unasababisha wengine kukosa huduma hiyo,” amesema.
Kaimu Mkurugenzi wa Muwsa, Tumaini Marandu amesema miundombinu iliyoharibiwa ni pamoja na mabomba waliyokuwa wameweka na chemba za kudhibiti kasi ya maji na kwamba jitihada zinazofanyika kwa sasa ni kurudisha miundombinu hiyo ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji.
“Tumefanya mradi kwa ajili ya kusaidia wananchi wa Kijiji cha Sango, Kata ya Kimochi na lengo la mradi huu ni kuboresha upatikanaji wa huduma ya maji, lakini kumetokea upinzani, kuna watu ambao hawataki tuwafungie mita, kwa hiyo wameanza kuharibu miundombinu wakiona itatufanya tusiwafungie mita na hawajui wanajihujumu wenyewe,” amesema.