DRC kupokea dozi 100,000 chanjo ya Mpox leo

Dar es Salaam. Shehena ya kwanza ya dozi 100,000 za chanjo ya ugonjwa wa homa ya nyani maarufu Mpox inatarajiwa kuwasili leo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Zaidi ya wagonjwa 17,500 na vifo 629 vimeripotiwa nchini humo tangu mwanzoni mwa mwaka huu, kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO).

Taarifa iliyotolewa jana Alhamisi, Septemba 4, 2024 na Kituo cha kudhibiti na kuzuia magonjwa barani Afrika (CDC) kimesema jumla ya chanjo 200,000 zikitarajiwa wiki hii.

Nchi hiyo kubwa ya Afrika ya Kati yenye watu milioni 100 ni kitovu cha mlipuko wa ugonjwa huo, ambapo idadi ya wagonjwa na vifo inazidi kuongezeka.

Mkuu wa CDC Afrika, Jean Kaseya ameiambia AFP, “Tumefurahishwa sana na kuwasili kwa shehena hii ya kwanza ya chanjo nchini DRC,” akiongeza kuwa zaidi ya dozi 99,000 zitawasili.

Ndege ya kwanza ya mizigo ikibeba dozi hizo za chanjo ya mpox iliondoka jana Jumatano jioni katika mji mkuu wa Denmark, Copenhagen na inatarajiwa kuwasili kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa mjini Kinshasa saa saba mchana saa za Afrika Mashariki.

Ndege nyingine inayobeba chanjo zinazosalia imepangwa kuwasili kabla ya mwisho wa wiki hii, CDC Afrika imethibitisha.

Chanjo hizo za kwanza ni kutoka maabara ya kampuni ya kutengeneza dawa ya Denmark, Bavarian Nordic.

Kwa mujibu wa WHO, serikali ya DRC inapanga kuanza kutoa chanjo hizo mwishoni mwa juma hili.

Related Posts