KOCHA Mkuu wa Geita Gold, Amani Josiah amesema anatambua baada ya usajili uliofanyika mashabiki wengi wamewawekea malengo makubwa, hivyo hataki kuwaangusha huku akiwaahidi watarajie ushindani mkubwa wa timu hiyo kwenye Ligi ya Championship na kurudi Ligi Kuu.
Klabu hiyo iliyoshuka daraja kutoka Ligi Kuu bara msimu uliopita sambamba na Mtibwa Sugar, leo Ijumaa itakuwa na tamasha la Geita Gold Charity Day ambapo itashiriki shughuli za kijamii kwa kufanya usafi, kutoa msaada kwa wagonjwa na watoto yatima na kucheza mechi ya kirafiki dhidi ya Kagera Sugar.
Mchezo huo utapigwa kwenye Uwanja wa Nyankumbu, mjini Geita na akizungumzia Ligi ya Championship itakayoanza Septemba 14, Josiah alisema anafahamu kiu ya mashabiki ni kuona timu hiyo inafanya vizuri, lakini wasiichukulie poa Championship kwa sababu timu nyingi zimejipanga na haitakuwa kazi nyepesi.
“Daraja la kwanza ni taswira nyingine ushindani uliopo msimu huu ni mkubwa kwahiyo hatuwezi kujihesabu tu sisi kama Geita timu nyingi ziko imara kwahiyo mpaka tufike kwenye hiyo ligi tutaangalia tumeshasogeza kutoka hapa kiasi gani,”€ alisema Josiah na kuongeza;
“Nafikiri Geita inaweza kuwa imara msimu huu lakini pia tutegemee ligi yenye ushindani na sisi kushindana zaidi kwa sababu watu wanatutaraji kwenye malengo makubwa na sisi inabidi tujiweke huko na hakuna kocha asiyependa kushinda.”€
Kocha huyo alisema baada ya ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Pamba Jiji katika mchezo wa kirafiki imewajengea kujiamini ambapo wachezaji na timu wanapaswa kuendelea na iamni hiyo, huku akifanya kazi ya kujenga timu yenye umoja na saikolojia imara.
“Tulicheza mechi na timu ya Ligi Kuu tulihitaji changamoto kutuonyesha makosa yetu na mahali tulipofikia kwahiyo tulikuwa tunahimiza vijana tuone kile tulichofundisha kinalipa, nimeona baadhi ya vitu chanya ambavyo tutaendelea navyo na vitu vya kufanyia kazi,” alisema.