Hisabati kuanza kutumika katika uchumi wa kidigitali

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imewataka Walimu wa Hesabu kuwaandaa wanafunzi na vijana kujikita katika masomo ya Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati (STEM) ili kupata fursa ya kushiriki maendeleo ya Dunia katika zama hizi za kidijiti.

Hayo yamebainishwa leo na mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Dr Jabir Bakari katika Mafunzo ya Muda Mfupi kwa Walimu wa Hisabati Tanzania Yaliyofanyika katika Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Mkwawa (MUCE) Mkoani Iringa.

“hesabu ni msingi wa sayansi na teknolojia, na katika ulimwengu unaobadilika haraka wa teknolojia, uchumi wa kidijiti unakuwa injini muhimu ya ukuaji wa kiuchumi.”amesema Dr Bakari.

Dk Bakari alibainisha kuwa mapinduzi ya kidijiti yameleta mabadiliko makubwa katika sekta mbalimbali, ikiwemo elimu ,Katika mazingira ya sasa, vifaa vya kufundishia kama vile kompyuta, programu za hisabati, na mifumo ya kujifunza mtandaoni vinatoa mbinu mpya na bora za kufundisha hisabati.

“Walimu wa hisabati wana fursa ya kujiendeleza na kutumia zana hizi za kidijiti ili kuwasaidia wanafunzi wao kuelewa na kupenda somo hili muhimu,” alisema.

Aliongeza kuwa walimu wanaoweza kutumia programu hizo kwa ufanisi wanaweza kusaidia wanafunzi wao kufikia viwango vya juu zaidi vya elimu na kuwa tayari kwa fursa za kiuchumi katika uchumi wa kidijiti.

Awali, Kaimu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Deusdedit Rwehumbiza, alisema walimu wa hisabati wanapaswa kuwa na jukumu la kuhakikisha kuwa wanafunzi wao wanapata maarifa hayo muhimu kwa ajili ya mafanikio ya baadaye.

Akitoa mfano, Profesa Rwehumbiza alisema uchanganuzi wa data unahitaji uelewa wa hali ya juu wa takwimu, algebra, na hesabu, ambazo zote ni sehemu kuu za hisabati.

Related Posts