MSHAMBULIAJI wa JKT Tanzania, Charles Ilanfya yamemkuta baada ya kuelezwa atalazimika kuwa nje ya uwanja kwa muda wa wiki mbili hadi uvimbe wa goti alionao upungue ndipo aanze vipimo ili kugundua tatizo linalomsumbua baada ya kuumia walipocheza dhidi ya Azam, Agosti 28, kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo.
Ilanfya alisema baada ya kupata maumivu goti lilianza kuvimba, alipkwenda hospital ikawa ngumu kupata matibabu, badala yake akapewa dawa ya kutuliza maumivu.
“Nilipelekwa hospitali na timu, lakini madaktari waliniambia damu imevilia kwenye goti, hivyo hawawezi kunipima hadi uvimbe upungue. Tangu niumie nimemaliza wiki imebakia wiki moja ili nirudi hospitali,” alisema Ilanfya na kuongeza:
“Kwa sasa nipo nyumbani, ingawa maendeleo yangu kila hatua daktari wa timu anakuwa anajua, maumivu yamepungua siyo kama mwanzo nilivyokuwa najisikia.”
Alisema chanzo cha kuumia alikuwa anakimbilia mpira akadondoka na kujikuta anapata maumivu makali ya goti na kuanza kuvimba.
“Sikuumizwa na mchezaji mwenzangu, ilikuwa kama ajali kazini, nilikuwa nauwahi mpira badala yake nikajikuta nipo chini, yote kwa yote naamini nitakaa sawa na nitaendelea na majukumu yangu,” alisema.