Kocha Prisons amkingia kifua Mbisa

WAKATI mashabiki wa Tanzania Prisons wakinung’unika kuondoka kwa aliyekuwa kipa namba moja wa timu hiyo, Yona Amos, lakini benchi la ufundi la timu hiyo limewatoa hofu likieleza kuwa makipa waliobaki akiwamo Mussa Mbisa kuwa ni bora na kazi yao itaonekana.

Prisons iliondokewa na Yona aliyetimkia Pamba Jiji na kuwaacha makipa wawili Mbisa na Edward Mwakyusa ambao kwa sasa wanachuana kuwania namba kikosi cha maafande hao kinachonolewa na kocha, Mbwana Makatta.

Hata hivyo, katika mechi mbili ilizocheza Prisons haijaruhusu wala kufunga bao lolote, huku langoni akisimama Mbisa aliyejiunga na timu hiyo misimu miwili iliyopita akitokea Coastal Union, huku akiwahi pia kuitumikia Mwadui ilipokuwa Ligi Kuu.

Kocha Makatta alisema wanaowabeza makipa waliopo kikosini humo wasubiri kuona matokeo ya nyota wake akieleza kuwa timu hiyo haijawahi kufeli katika upande wa makipa na kwamba kikosi chake kitafanya vizuri.

Alisema katika mechi mbili walizocheza,  Mbisa amekuwa na kiwango bora kutokana na kutoruhusu wavu wake kuguswa na amekuwa akiokoa hatari nyingi langoni, hivyo matarajio yao ni kuona Prisons ikimaliza msimu bila kufungwa idadi kubwa ya mabao.

“Mbisa anao uzoefu na uwezo mkubwa, katika mechi mbili tulizocheza hatujaruhusu wavu wetu, kimsingi tunaendelea kufanyia kazi mapungufu kuhakikisha timu inamaliza msimu vyema bila idadi kubwa ya mabao,” alisema Makatta kipa wa zamani wa kimataifa aliyewahi kutamba na Tukuyu Stars na Yanga.

Kwa upande wa Mbisa, alisema matokeo waliyoanza nayo si mabaya sana licha ya kwamba hesabu zao ilikuwa ni kupata pointi sita ugenini lakini hata alama mbili.

Related Posts