Longido. Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Amos Makalla amesema mpaka wa Namanga ni eneo muhimu la kukuza biashara na ushirikiano kati ya Tanzania na Kenya akiwataka watendaji wanaohumudu eneo hilo kutekeleza majukumu yao vyema.
Makalla ameeleza hayo leo Alhamisi Agosti 5, 2024 alipofanya ziara ya ghafla katika mpaka huo uliopo wilayani Longido mkoani Arusha kwa lengo la kujionea utendaji kazi wa eneo hilo. Mwenezi huyo yupo katika ziara ya siku sita katika mikoa ya Arusha na Manyara.
Amesema miongoni mwa mambo wanayotakiwa kuyafanya watendaji hao ni pamoja na kuendeleza uhusiano mwema kati ya Tanzania na Kenya, kwa kuwa wapo mipakani ndiyo wanaoakisi dhamira njema ya viongozi wakuu wa mataifa ya Tanzania na Kenya.
“Mkifanya kazi vibaya mtaakisi sura ya Tanzania, lakini mkitelezea majumuku yenu vema mtaakisi dhamira njema ya Rais (Samia Suluhu Hassan), tunafarijika kwa namna mnavyochapa kazi kwa sababu maelezo yenu yamejitosheleza.
“Mmetuambia Tanzania inanufaika na mpaka huu kwa kupeleka bidhaa nyingi Kenya, kikubwa tuongeze kasi ya kuhakikisha mizigo inakwenda kwa haraka pasipo na foleni maana biashara ni fursa inayotegemea muda pia,” amesema Makalla.
Amewasisitizia watendaji hao kuondoa urasimu katika eneo hilo ili kuendana na maono ya Marais, Samia wa Tanzania na Dk William Ruto wa Kenya ambao kwa nyakati tofauti wamekuwa wakihimiza ujirani na ushirikiano mwema.
Makalla aliyewahi kuwa mkuu wa mikoa kadhaa alitumia nafasi hiyo, kumtambulisha mkuu wa wilaya mpya wa Longido, Salum Kali akiwataka watendaji kumpa ushirikiano wa kutosha katika kusimamia masuala mbalimbali ya wilaya hiyo.
Naye, Kali aliyechukua nafasi ya Marco Ng’umbi ambaye uteuzi wake ulitenguliwa na Rais Samia, amesema leo ndiyo ameripoti wilayani humo, lakini kupitia maelekezo yaliyotolewa na Makalla watahakikisha wanayasimamia kwa ushirikiano na watendaji wenzake pasipo kukiangusha Chama Cha Mapinduzi.
“Tutayasimamia yote ulioyaagiza, kama kulikuwa na mkwamo wa malori kujaa nakuhakikishia tutalifanyia kazi,” amesema Kali.
Awali, Ofisa wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), eneo la Namanga, Abdallah Mambi alimwambia Makalla na ujumbe wake kwamba hivi sasa utendaji kazi unakwenda vizuri, hakuna mkwamo wowote.
“Bidhaa nyingi zinakwenda Kenya na zingine zinaingia chini, tuna ushirikiano mzuri kutekeleza majukumu tuliopewa,” amesema Mambi.