Matumaini Kombo kada wa Chadema kuachiwa kwa dhamana leo

Tanga. Leo Alhamisi, Septemba 5, 2024 ni siku nyingine ya matumaini kwa mwanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) mkoani Tanga, Kombo Mbwana, anayekabiliwa na kesi ya jinai, kurejea uraiani kwa dhamana.

Uamuzi huo unatarajiwa kutolewa na Mahakama ya Wilaya ya Tanga, kuhusiana na maombi ya Jeshi la Polisi kuomba mshtakiwa huyo asipewe dhamana kwa sababu za kiupelelezi wa kesi inayomkabili.

Kombo ambaye awali aliripotiwa kupotea kabla ya Jeshi la Polisi Tanga, kutangaza kumshikilia siku 29 baadaye, anakabiliwa na kesi ya jinai, akidaiwa kutumia vifaa vya mawasiliano ikiwemo kadi ya simu ya mkononi isiyosajiliwa na bila kutoa taarifa.

Licha ya mashtaka yanayomkabili kuwa na dhamana na Mahakama kutangaza kuwa dhamana yake iko wazi tangu alipopandishwa kizimbani na kusomewa mashtaka Julai 16, 2024, lakini dhamana yake imekuwa na vikwazo mbalimbali na hivyo kumfanya aendelee kusota mahabusu hadi leo.

Hata hivyo, leo Alhamisi, Septemba 5, 2024, Mahakama ya Wilaya ya Tanga inatarajiwa kutoa uamuzi wa zuio la dhamana yake lililowekwa na Jeshi la Polisi Tanga.

Uamuzi huo unaotarajiwa kutolewa na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Moses Maroa anayesikiliza kesi yake ndio utakaoamua hatima yake kama anarejea uraiani leo kwa dhamana au la.

Kama Mahakama hiyo katika uamuzi wake itatupilia mbali hoja za zuio la dhamana yake lililowekwa na Jeshi la Polisi, basi ana matumaini ya kurejea uraiani leo, kama atatimiza masharti ya dhamana yaliyotolewa awali na Mahakama kabla ya zuio la Polisi.

Hata hivyo, kama Mahakama itakubaliana na hoja za zuio hilo, basi sasa Kombo ataendelea kusota mahabusu kwa muda usiojulikana, mpaka hapo itakapoamuriwa vinginevyo pengine na Mahakama ya juu, kama itaombwa kuingilia kati suala hilo.

Katika kesi hiyo ya jinai namba 19759 ya mwaka 2024, Kombo anakabiliwa na mashtaka matatu chini ya Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta.

Katika shtaka la kwanza anadaiwa kushindwa kutoa taarifa za kutosha za akaunti ya kadi yake ya simu, kinyume na kifungu cha 126 cha Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta,.

Anadaiwa Julai 9, 2024 katika mtaa wa Hassan Ngwilizi wilayani na mkoani Tanga, alikutwa akimiliki laini (kadi ya simu) ya Tigo yenye namba (ICCID) 8925502042093621824, iliyosajiliwa kwa jina la Shukru Kahawa na kushindwa kutoa maelezo ya kutosha kuhusu umiliki wa laini hiyo.

Pia, anadaiwa kushindwa kusajili laini ya simu ambayo awali ilikuwa inamilikiwa na mtu mwingine na  kushindwa kuripoti kuhusu mabadiliko ya laini ya simu.

Kabla ya kupandishwa kizimbani, Kombo alitoweka tangu Juni 15, 2024, baada ya kuchukuliwa na watu wasiojulikana nyumbani kwake Kijiji cha Kwamsala, wilayani Handeni, mkoani Tanga na kupelekwa mahali ambako hata ndugu zake hawakupafahamu.

Julai 14, 2024, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Zakaria Bernard alitangaza anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma hizo, ndipo Julai 16 akapandiahwa kizimbani.

Baada ya kusomewa mashtaka hayo ambayo aliyakana, Mahakama ilisema dhamana yake ilikuwa wazi kwa masharti ya kuwa na wadhamini wawili watakaosaini bondi ya Sh2 milioni kila mmoja, wenye barua ya mtendaji wa mtaa wanakokaa pamoja na vitambulisho vya Taifa (Nida).

Hata hivyo, hakutimiza masharti hayo kwa kukosa wadhamini kwani alipopandishwa kizimbani saa 11 jioni kimyakimya, familia na ndugu zake hawakuwa na taarifa.

Kesho yake familia yake kwa kushirikiana na mawakili wake walifanya mchakato wa dhamana na walipokamilisha mahakama ilitoa amri ya kufikishwa mahakamani kwa ajili ya dhamana yake, mara mbili lakini Jeshi la Polisi halikutekeleza.

Julai 30, 2024 siku ambayo kesi hiyo ilitajwa, mawakili na ndugu zake walifika mahakamani hapo wakiwa wamejiandaa kukamilisha masharti hayo ya dhamana wakitarajia kuondoka naye.

Hata hivyo, dhamana yake iliyeyuka baada ya Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai mkoa (RCO) wa Tanga kuwasilisha mahakamani kiapo cha cha kuzuia dhamana hiyo.

RCO alieleza katika kiapo hocho kuwa bado wanaendelea na upelelezi na kwamba wanatarajia kuwaongeza washtakiwa wengine katika kesi hiyo, ambao wako katika maneo mbalimbali nchini

Mawakili wa mshtakiwa huyo waliokuwepo siku hiyo, Deogratius Mahinyila na Michael Rugina walipinga kuwepo kwa kiapo hicho kwanza kwa kuwasilisha kinyume na utaratibu wa kisheria.

Pili, walidai RCO hana mamlaka hayo ya kuzuia dhamana, tena Mahakama ikiwa imeshatoa uamuzi wa masharti ya dhamana.

Hata hivyo, Hakimu Maroa aliamua kutengua amri ya masharti ya dhamana na akapanga kusikiliza maombi hayo ya polisi ya zuio la dhamana Agosti 12 na akautaka upande wa utetezi kuwasilisha kiapo kinzani kujibu kiapo cha RCO, kabla ya tarehe hiyo.

Siku hiyo maombi hayo yaliposikilizwa upande wa mashtaka ulidai kuwa RCO anataka mshtakiwa asipewe dhamana kwa kuwa anaweza kuingilia upelelezi ambao bado unaendelea.

Mawakili wa Kombo walipinga hoja hiyo wakidai dhamana ni haki ya mshtakiwa na mashtaka yanayomkabili yanadhaminika.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote ndipo Hakimu Maroa akapanga kutoa uamuzi Agosti 22, lakini siku hiyo uamuzi huo ulipigwa kalenda tena mpaka leo, Kwa maelezo kuwa Hakimu Maroa hakuwepo.

Endelea kufuatilia Mwananchi kwa habari na taarifa zaidi

Related Posts